Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KATIKA hali isiyo ya kawaida, Mabingwa wa Tanzania kwa mwaka 1999 na 2000, Mtibwa Sugar ya Manungu Turiani mkoani Morogoro wamekata tamaa ya kushika nafasi tano za juu katika msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Tobias Kifaru Lugalambwike, msemaji wa Mtibwa amesema kuwa kwasasa wanapigania nafasi ya sita au saba kwasababu hawana uwezo wa kupanda nafasi za juu.
“Mashabiki wetu watambue kuwa ligi imekuwa ngumu zaidi msimu huu. Mtibwa hatuna chetu kwasasa zaidi ya kung`ang`ania nafasi ya sita au saba. Nafasi ya kwanza, pili, tatu, nne, tano ni ngumu kwetu”. Alisema Kifaru.
Kifaru alisema mpaka sasa wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 27 katika nafasi ya 8, na kwa michezo waliyosaliwa nayo wanatarajia upinzani mkubwa kupata matokeo.
“Tumerejea nyumbani kuendelea na mazoezi kujiandaa dhidi ya Coastal Union. Wapinzani wetu wametoka kushinda dhidi ya Simba sc, sisi tulitoka sare ya 1-1 na Mgambo kule Tanga. Mipango yetu ni kupambana hapa kwetu kuchukua pointi tatu muhimu”. Alisema Kifaru.
Mtibwa Sugar wamebakiza mechi ya machi 30 dhidi ya Coastal Union katika dimba la Manungu, pia watasafiri mpaka mkoani Tabora kuwavaa vibonde, Rhino Rangers aprili 6 mwaka huu.
Baada ya Tabora, watarudi Manungu aprili 12 kuwakaribisha maafande wa Ruvu Shooting.
Watahitimisha msimu aprili 19 mkoani Arusha ambapo watawafuata maafande wa JKT Oljoro.
Nao Coastal Union kupitia kwa Afisa habari wake, Hafidh Kido wametangaza kiama kwenye mechi nne zilizosalia.
Akizungumza kwa kujiamini, Kido alisema kikosi chao kimechanganyika kwa wakongwe na damu changa, hivyo kukifanya kuwa na kasi kubwa.
“Uliona jinsi timu ilivyocheza dhidi ya Simba, hakika kumekuwepo na mabadiliko. Tunajiandaa dhidi ya Mtibwa Sugar kule Manungu, lazima tuibuke na ushindi”. Alisema Kido.
Afisa habari huyo alisema kuwa wamebakiza mechi dhidi ya Mtibwa Sugar machi 30 mwaka huu katika uwanja wa Manungu Turiani mkoani Morogoro.
Pia watakuwa na mchezo wa aprili 6 mwaka huu dhidi ya ndugu zao Mgambo JKT katika uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga.
Baada ya mechi hiyo Wagosi hao wa Kaya watawakaribisha tena JKT Ruvu katika dimba lao la Mkwakwani.
Mechi ya mwisho itakuwa aprili 19 mwaka huu ambapo wataumana na Kagera Sugar katika dimba la Mkwakwani, Tanga.
No comments:
Post a Comment