Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KUTOKA TANGA
MGAMBO JKT VS YANGA SC UWANJA WA MKWAKWANI
Kuelekea katika mchezo huo, afisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto ameuambia mtandao huu kuwa hali ya wachezaji ni nzuri, wameshafanya mazoezi na wanasubiri mechi ya jioni.
“Timu zote za ligi kuu ni sawa na ndio maana zipo ligi kuu. Kikubwa ni kwamba tumejiandaa kufanya vizuri ili kuibuka na ushindi. Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kuishangilia timu kwasababu tuna imani ya kufanya vizuri”. Alisema Kizuguto.
Naye kocha msaidizi wa Mgambo JKT, Moka Shaban Dihimba alisema wataingia katika mchezo wa leo kwa lengo la kutafuta pointi tatu na si vinginevyo.
“Mechi iliyopita tumefungwa mabao 2-0 na Azam fc. Kupoteza mechi ya leo kutatuweka mazingira magumu zaidi ya kubakika ligi kuu, hivyo tutapambana bila kujali ubora wa Yanga ili kuibuka na ushindi”. Alisema Moka.
HAPA DAR ES SALAAM
AZAM FC VS SIMBA SC UWANJA WA TAIFA
Asha Muhaji, afisa habari wa Simba sc, amesema vijana wako na morali kubwa ya kuibuka na ushindi leo.
“Mchezo utakuwa ni mgumu kwasababu Azam ni timu bora. Benchi la ufundi limewaanda vijana kwa ajili ya kupambana, leo hii tunatarajia kutibua rekodi ya Azam fc ya kutofungwa msimu huu”.
“Cha msingi mashabiki wetu waje, kila mtu ana nafasi yake katika klabu. Waje kwa wingi kuishangilia timu yao ambayo itaingia kulinda heshima na kuwaonesha Azam fc kwamba wao ndio waliotangulia ligi kuu”. Alisema Asha.
Wao Azam fc wamesema kwamba, mechi na Simba SC leo hii itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao bado ni timu bora na watataka kurejesha heshima baada ya kucheza mechi tano bila kushinda.
Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa ‘Father’ amesema katika mahojiano na tovuti ya klabu kwamba, wanaiheshimu Simba SC kama moja ya timu za kihistoria nchini na pia ni timu bora, hivyo wanaamini wanaingia kwenye mchezo mwingine mgumu.
“Simba SC ni moja ya timu bora msimu huu, haipo kwenye mbio za ubingwa kwa sababu ya bahati tu, lakini si kama ni timu mbaya. Kumbuka tulikuwa na Simba SC katika Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu, sisi tukatolewa Nusu Fainali, wao wakaingia Fainali,”alisema Father.
KUTOKA MBEYA
MBEYA CITY VS TANZANIA PRISONS UWANJA WA SOKOINE
Kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi amesema wanamshukuru Mungu kwasababu vijana wamemalizia mazoezi ya mwisho jana na wapo tayari kwa mchezo wa leo.
“Ni mechi ngumu sana. Kama unavyojua wenzetu ni mahasimu wa klabu yetu na watachagizwa na matokeo ya kupoteza mabao 5-0 kutoka kwa Yanga, hivyo wataingia kujiuliza katika mchezo wetu. Mechi itakuwa nzuri kwasababu Mbeya City ni bora zaidi”. Alisema Maka.
Kwa upande wa Prisons, katibu mkuu wa klabu hiyo, Inspekta Sadick Jumbe amesema hawana majeruhi, vijana wapo katiki ari ya juu kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 na Mbeya City mzunguko wa kwanza.
“Matarajio yetu makubwa ni kushinda ili kujiweka katika mzingira mazuri. Leo lazima tukimbie katika mstari wa kushuka daraja. Kikosi chetu kimebadilika na kimekuwa na uwezo mkubwa. Jana jioni nimetoka uwanja wa ndege kumpokea mchezaji wetu hatari, Omega Seme akitokea Dar es salaam. Kikosi kimekamilika” Alisema Jumbe.
Naye Omega kwa upande wake alikiri kuwa mechi itakuwa ngumu, lakini watajitahidi kufanya vizuri kwasababu wametoka kufungwa na wamejiuliza wapi walikosea na kufungwa mabao 5-0 na Yanga katikati ya wiki.
KUTOKA KAGERA
KAGERA SUGAR VS RUVU SHOOTING UWANJA WA KAITABA
Kocha msaidizi wa Kagera Sugar,Murage Kabange amesema hesabau zao kubwa kwasasa ni kutafuta nafasi ya tatu au nne, na kwa kuanza wanajipanga kuwafumua Ruvu Shooting leo jioni uwanja wa Kaitaba.
“Timu iko vizuri. Hakuna majeruhi mpaka sasa. Kwa bahati nzuri tumetoka kushinda mechi iliyopita. Tunaheshimu uwezo wa Shooting, lakini tumejiandaa kutafuta ushindi. Niwaombe mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi leo hii”. Alisema Kabange.
Kwa upande wa Ruvu Shooting, afisa habari wake, Masau Bwire amesema hawajaenda Kaitaba kunywa supu ya senene, bali wameenda kuwaonesha Kagera Sugar namna mpira unavyochezwa.
“Kwasasa tunahitaji kujenga heshima iliyopotea hapo nyuma. Tunajua watu wanawaza kuwa Ruvu Shooting ni timu dhaifa. Leo hii tunawaonesha watanzania kuwa timu yetu ni bora na hatari zaidi. Wapiganaji wetu wapo katika morali kubwa”. Alisema Masau.
KUTOKA MOROGORO
MTIBWA SUGAR VS COASTAL UNION UWANJA WA MANUNGU
Afisa habari wa Mtibwa Sugar, Tobias Kifaru Lugalambwike amesema hali ya Manungu ni safi kabisa na wanajiandaa kuvuna pointi tatu muhimu.
“Tumekuwa na msimu mbaya, lakini tunahitaji ushindi ili kujiweka nafasi nzuri zaidi. Kocha wetu Mecky Mexime amefanyia kazi makosa yaliyokuwepo katika kikosi chetu mechi iliyopita. Tuna imani kubwa ya kuwafunga wagosi wa kaya, Coastal Union leo”. Alisema Kifaru.
Kwa upande wa Coastal Union, Afisa habari wake, Hafidh kido alisema malengo yao ni kushinda mechi zote zilizosalia kuanzia ile waliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Simba sc.
“Kikosi kimekuwa na mabadiliko, kocha amewajumuisha vijana zaidi na wamekiongezea kasi. Mtibwa watashindana sana, lakini sisi pia tutajidhatiti kuibuka na pointi tatu”. Alisema Kido.
KUTOKA CHAMAZI DAR ES SALAAM
JTK RUVU VS RHINO RANGERS UWANJA WA AZAM COMPLEX
Fredy Minziro, kocha wa JKT Ruvu amesema timu ipo tayari kupambana na maafande wenzao kutoka Tabora.
“Ligi imekuwa ngumu sana, mchezo wa leo utakuwa mzuri kwa timu zote. Kikubwa mashabiki wetu waamini kuwa tumejiandaa vizuri kuibuka na ushindi”. Alisema Minziro.
Naye, Jumanne Chale, Kocha mkuu wa Rhino alisema matumaini yao ya kubakia ligi kuu yamefifia kabisa, lakini si sababu ya kuingia kiunyonge katika mechi ya leo.
“Tumefanya vibaya na kupoteza matumaini, ila lazima tucheze mpira kwa kutafuta ushindi wa mechi zilizobaki. Mchezo wa leo utakuwa mgumu kwa timu zote kutokana na mazingira ya klabu zote. Tutajitahidi kushinda”. Alisema Chale.
Baadaye ungana nasi kupata matokeo ya mechi zote na mahojiano ya makocha na maafisa habari wa klabu zote.
No comments:
Post a Comment