Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Young Africans wamekiri kuwa kwasasa ligi kuu imekuwa ngumu zaidi kutokana na timu zote kuwa katika uhitaji mkubwa wa pointi.
Afisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto ameuambia mtandao huu kuwa upinzani walioupata kutoka kwa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro unadhihirisha kuwa timu zinapambana sana ngwe hii ya lala salama ili kujiweka mazingira mazuri katika msimamo.
“Kila timu inahitaji pointi muhimu. Kuna timu zinawania ubingwa, nyingine zinakwepa kushuka daraja, wakati baadhi ya timu zinahitaji nafasi za juu. Hivyo kwa mazingira haya utagundua kuwa ligi lazima iwe na ushindani”. Alisema Kizuguto.
Afisa habari huyo aliwataka mashabiki wa Yanga kutokata tamaa kwani wana kiporo kingine dhidi ya Azam fc jumatano ya machi 19 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
“Timu iliyopo kileleni imetuzidi kwa pointi nne tu. Tukishinda mchezo ujao tutakaa nafasi nzuri. Tutazidiwa pointi moja na vinara, wakati bado tutakuwa na mchezo mwingine mkononi. Cha msingi tushikamane wakati huu ili tuweze kutetea ubingwa wetu”. Alisema Kizuguto.
Naye Afisa habari wa Mtibwa Sugar, Tobias Kifaru Lugalambwike ameueleza mtandao huu kuwa katika mchezo huo, Yanga walibanwa sana na Mtibwa sugar, lakini kadi nyekundu aliyopata mshambuliaji wao, Abdallah Juma mwanzoni wa kipindi cha pili ilipunguza kasi ya mashambulizi.
“Watu walifurika mno kutoka jijini Dar es salaam kuja kushuhudia cheche za Yanga waliosifiwa kuonesha soka zuri kule Misri. Kiukweli Yanga hawana na lolote. Wamewaudhi sana mashabiki wao. Tuliwabana mno na isingekuwa kadi nyekundu basi wangekiona cha moto”. Alitamba Kifaru.
Aidha alisema waamuzi wa leo walikuwa upande wa Yanga kwani kadi nyekundu mazingira yake hayakuwa sahihi.
“Mechi ya Simba nahodha wetu Shaban Nditi alipata kadi nyekundu na tukatoka 1-1, leo Juma ametapa nyekundu, lakini tumetoka suluhu. Tumedhahirishia kuwa sisi ni wakongwe na wameshindwa kuvunja rekodi ya kutokutufunga uwanja wa Jamhuri kwa miaka minne sasa”. Alisema Kifaru.
Katika mchezo mwingine uliopigwa uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam, Azam fc wameshinda mabao 4-0 dhidi ya Coastal Union.
Baada ya mchezo huo, Afisa habari wa klabu hiyo, Jafar Idd Maganga amesema uongozi mzima wa Azam fc umefurahishwa na ushindi mnono waliopata.
“Vijana wetu wamepambana na kuwafunga Coastal Union ambao walikuwa wagumu. Walikuja Ashanti tukawapa `foo` , nao Coastal wamekula `foo`,. Tunawapongeza sana vijana wetu kwa kuendelea kubakia kileleni huku wakigawa dozi nene kwa wapinzani”. Alisema Jafar.
Jafar alisisitiza kuwa wakati huu ni wa mapambano ya ubingwa, hivyo wamefurahishwa na matokeo ya Yanga leo hii, sasa hesabu zao ni kuelekea mchezo wa jumatano machi 19 dhidi ya wanajangwani hao.
Kwa upande wake Afisa habari wa Coastal Union, Hafidh Kido baada ya kufungwa bao 4-0 alisema ni matokeo ya mchezo na ni kawaida tu katika soka.
“Timu zinafungwa 5, 6 hadi 7 au 8. Kufungwa manne ni kawaida. Cha msingi tunaangalia mchezo ujao dhidi ya Simba”. Alisema Kido.
Akielezea mechi yao dhidi ya Simba, Kido alisema ni mlima mwingine wa kupanda kwani wapinzani wao wako sawa.
Tukielekea huko Kaitaba, Kagera Sugar waliwakaribisha Tanzania Prisons na kushinda mabao 2-1 katika dimba lao la Kaitaba.
Kocha msaidizi wa Kagera Sugar, Murage Kabange alisema mechi hiyo ilikuwa ngumu kwani Prisons walianza kuwafunga.
“Prisons walikuja kwa kasi. Hawakupoteza mchezo wowote mzunguko wa pili. Walianza kwa kutufunga, tukasawazisha na dakika za lala salama tuliwafunga bao la pili na la ushindi. Niwashukuru sana mashabiki wetu kwani wamekuwa wakitusapoti sana. Bado tuna mechi nyumbani, hivyo waendelee kutuunga mkono”. Alisema Kabange.
Kwa upande wa Prisons kupitia kuwa katibu wake mkuu, Sadick Jumbe walikiri kupoteza mchezo kwasababu Kagera walikuwa na mipango mzuri kuliko wao.
“Tulianza kuwafungwa. Tukafanya makosa mawili makubwa, wakatufunga kirahisi. Tumekubali kupoteza. Mapambano yanaendelea na kasi yetu ipo palepale hata kama tumepunguzwa leo”. Alisema Jumbe.
No comments:
Post a Comment