Search This Blog

Tuesday, March 25, 2014

BAADA YA KUWANYUKA SIMBA 1-0, WAGOSI WA KAYA WATANGAZA KIAMA MECHI ZILIZOSALIA!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


WAGOSI wa Kaya, Coastal Union wenye makazi yao jijini Tanga, wamepania kuvuna pointi zote 12 katika michezo minne iliyosalia ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Akizungumza na mtandao huu, Afisa habari wa klabu hiyo, Hafidh Kido amesema kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Chipo amekifanyia marekebisho kikosi chao ambapo amewaingiza vijana wadogo kwa lengo la kuleta kasi zaidi.
“Tumewafunga Simba bao 1-0 kwasababu kocha aliwatumia vijana wetu. Walicheza vizuri na kwa kasi nzuri. Tumebakiwa na mechi nne, tunajiandaa kushinda mechi zote”. Alisema Kido.
Kido aliongeza kuwa mashabiki wao wawaamini katika mechi zajazo kwani hawana cha kupoteza zaidi ya kutafuta ushindi ili kumaliza ligi katika nafasi nzuri.
Afisa habari huyo alisema kuwa wamebakiza mechi dhidi ya Mtibwa Sugar machi 30 mwaka huu katika uwanja wa Manungu Turiani mkoani Morogoro.
Pia watakuwa na mchezo wa aprili 6 mwaka huu dhidi ya ndugu zao Mgambo JKT katika uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga.
Baada ya mechi hiyo Wagosi hao wa Kaya watawakaribisha tena JKT Ruvu katika dimba lao la Mkwakwani.
Mechi ya mwisho itakuwa aprili 19 mwaka huu ambapo wataumana na Kagera Sugar katika dimba la Mkwakwani, Tanga.
Coastal Union amebakiza mechi moja ya ugenini, huku tatu itakuwa katika dimba la nyumbani.
Imekuwa shida kwa wageni kuvuna pointi tatu katika dimba la CCM Mkwakwani, hivyo mechi hizo zitakuwa ngumu kwa timu pinzani.
Kikosi cha wagosi wa kaya kwasasa kinaundwa na  wachezaji tofauti tofauti kama vile  Fikirini Suleiman, Hamadi Juma, Abdi Banda, Yusuf Chuma, Mbwana Kibacha, Razak Khalfan, Ally Nassor ‘Ufudu’, Behewa Sembwana, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Kenneth Masumbuko, Danny Lyanga.
Wengine ni pamoja na Mansour Alawi, Ayoub Masoud, Marcus Ndeheli, Ayoub Semtawa, Mohammed Miraji, Crispian Odula, na Mohammed Kipanga.
Katika msimamo wa ligi kuu, Coastal Union wapo nafasi ya saba baada ya kujikusanyia pointi 29 katika michezo 22 waliyoshuka dimbani.

No comments:

Post a Comment