Hatimaye muda umefika. Al Ahly tayari wapo jijini. Kwa
mashabiki wa Yanga, ni wakati wa hisia mchanganyiko. Furaha iliyojichovya
kwenye woga wa kukutana na timu kubwa. Kwa upande mmoja wasingependa kukutana
na wababe wao katika raundi ya kwanza. Kwa upande wa pili, timu kubwa kama
Alhly hupandisha mzuka kwa mashabiki.
Ni fursa nyingine tena kwa Yanga, aidha kufungua ukurasa
mpya kwa kuwafunga wamisri kwa mara ya kwanza au kuendeleza uteja kwa waarabu.
Mechi sita, vipigo vinne, kapu la magoli 14 huku
wakijitutumua kwa kufunga bao moja ni historia ambayo kila Mwanajangwani
asingependa iendelee hio Jumamosi.
Mara ya mwisho, timu hizi zilipokutana, Al Ahly walimaliza
biashara kwenye mechi ya kwanza tu kwa ushindi wa 3-0 huko Cairo. Kipigo cha
‘tatu bila’ kilipelekea kocha wa Yanga wa wakati huo, Dusan Kondic kuinua
mikono na kukiri ‘kiroho safi’ tu kuwa Al Ahly wapo anga zingine na Yanga
hawawezi kushinda hata mechi ya marudiano nyumbani.
Mechi ya marudiano hapa Dar, ilishuhudia, udhaifu wa safu ya
ushambuliaji ya Yanga ukirahisha pambano kwa Al Ahly na kuondoka na ushindi wa
1-0. Si tu bao la Flavio Amado liliowaumiza Yanga, kitendo cha mashabiki wa
Simba kuishangilia Al Ahly kwa mtindo wa kuhesabu pasi kiliwafanya Yanga wawe
wanyonge Zaidi.
Kwa mara nyingine tena, hata kabla ya pambano kuchezwa,
hukumu ya kihistoria inafanya ulimwengu wa kandanda wa bara la Afrika usiwape
uzito Yanga kuitoa Al Ahly. Hata hivyo Jangwani, tofauti na miaka ya nyuma,
wana imani kubwa kuwa maandalizi waliyoyafanya yanawapa nafasi nzuri ya
kuwaduwaza wamisri.
Baada ya kuwashuhudia Al Ahly wakiwafunga CS Sfaxien kwenye
Super Cup, kocha msaidizi, Boniface Mkwasa, alisema jamaa wanafungika. Sababu
kuu mbili zinaweza kuwa zilimpa Mkwasa ujasiri wa kutamka Al Ahly wanafungika
kinyume na alivyofanya Profesa Dusan Kondic mwaka 2009.
Moja, kikosi cha Yanga kimeboreka kulinganisha na kikosi cha
mwaka 2009. Pili, kikosi cha Al Ahly cha mwaka huu ni dhaifu kiasi
ukilinganisha na kikosi chao cha mwaka 2009. Machafuko ya kisiasa yaliyotokea
mwaka 2011 na kusababisha kusimamishwa kwa ligi yamewadhoofisha ndani ndan je
ya uwanja.
Kwa Yanga, usajili wa Emmanuel Okwi kumeiongezea nguvu safu
ya ushambuliaji. Mwaka 2011, Yanga walitolewa na Zamalek kwa sababu ya udhaifu
wa safu yao na hata mwaka 2009, wangeweza angalau kupata sare au kuondoka na
ushindi hapa Dar.
Pili tofauti na miaka ya nyuma, matumaini ya Yanga yanabebwa
na safu ya ushanbuliaji hasa ukizingatia udhaifu wa idara za kiungo na ulinzi.
Kasi ya Okwi na Ngassa wakichagizwa na uwepo wa Hamisi Kiiza
ndani kumi nane ndio silaha kuu ya Yanga katika kulitia misukosuko lango la Al
Ahly. Hata hivyo, makali ya ushambuliaji wa Yanga yatategemea Ngassa atapangwa
wapi, kati au pembeni.
Ingawa alipangwa kati kama kuingo mchezeshaji dhidi ya Ruvu
Shooting na kuonekana kung’aa, Ngassa anahitaji eneo kubwa Zaidi linalopatikana
pembeni kutumia vizuri Zaidi kasi yake. Dhidi ya Al Ahly, tofauti na Ruvu Shooting,
Ngassa atapewa nafasi ndogo kukimbiza
mpira na muda mchache sana kufanya maamuzi ya wapi aupeleke mpira. Ni vigumu
kwa Ngassa kukupa ubora wake wote akipangwa katikati. Labda Pluijm anaweza
kumrudisha Ngassa pembeni na kumuacha Niyonzima kucheza kati.
Golini, kuna kasheshe la Kaseja na Munishi. Nani atapangwa?
Kocha Pluijm ataamua aidha kuchagua uzoefu wa Kaseja katika michuano ya
kimataifa au kiwango cha juu cha sasa cha Munishi? Uzoefu au Kiwango?
Tatizo ni kuwa Kaseja kwa sasa hajapata mechi za kiushindani
za kutosha kurudisha kiwango chake. Pili, Kaseja ana tatizo la kuchelewa kuruka
licha ya kuwa ana uwezo mkubwa wa kuchupaa na kuelekea upande sahihi wa uelekeo
wa mpira (Timing weakness, excellent reflex).
Safu ya ulinzi ya Yanga ina leta wasiwasi Zaidi. Nadir
Haroub na Kelvin Yondani, licha ya ukakamavu wao wanapata shida wanapokutana na
washambuliaji wanaopendelea kukokota mpira miguuni. Alichowafanyia Ramadhani
Singano kwenye mtani Jembe, waarabu wanaweza kukifanya maradufu Zaidi. Pia safu
ya ulinzi inabidi kutuliza vichwa hasa wanapokutana na mashambulizi mfululizo.
Nadir Haroub anatakiwa ajaribu kutulia na kujua ni wapi aupeleke mpira.
Utulivu, umakini na uangalifu wa Mbuyu Twite utahitajika
sana kwenye pambano hili. Tofauti na walinzi wenzake, Twite anajua ni wapi
afanye tackling na tackling ya aina gani kwa wakati upi. Kwenye kiungo, msalaba
wa Yanga utabebwa na uwezo wa kukimbia na pia umakini wa kuwa katika sehemu
sahihi kwa wakati sahihi wa kiungo Frank Domayo. Tofauti na viungo wengi
nchini, Domayo si tu anazidi kuimarika, bali anajua kucheza bila mpira. Anajua
kukaba nafasi kwa kuwahi kufika katika eneo hatari inapoelekea. Ataibeba roho
ya Yanga katikati.
Kwa upande wa Al Ahly, kikosi chao ni dhaifu ukilinganisha
na vikosi vyao vya zamani. Hata hivyo, Al Ahly wanajua kuwa ni dhaifu, wanajua
kuwa maadui wanalijua hili hivyo wanajiandaa kwa mashambulizi ya adui anayekuja
na matumaini ya ‘kuiua Al Ahly dhaifu’. Wengi wameangamia kwa kutaka kutumia
udhaifu wa Al Ahly ndio maana Al Ahly dhaifu imeweza kutetea ubingwa wao wa
Afrika. Orlando Pirates waliingia mkenge na kujikuta wakiambulia kipigo kwenye
fainali.
Kwa sasa Al Ahly ni kama Simba mzee, anafahamu udhaifu wake
na kuutumia udhaifu huo kama silaha yake. Wanaweza kukuachia utambe na mpira na
kuwasumbua huku wenyewe wakihitaji nafasi chache sana kuuweka mpira kimiani.
Kama alivyo Simba aliyezeeka, pigo lao kubwa ni timing na kutumia nafasi chache
kutoa pigo takatifu.
Kustaafu kwa Aboutreika ambaye amekuwa nguzo yao kwa
takriban muongo mzima, kunaacha pengo Fulani. Hata hivyo, bado wana kikosi
kilichosheheni mchanganyiko wa vipaji vya kutosha kuisumbua klabu kigogo
chochote cha soka barani Afrika, sembuse na Yanga.
Kwa wacheza Kamari na mashabiki wanaliangalia pambano bila
utumwa hisia za unazi, ushabiki na uzalendo, ni dhahiri kuwa Al Ahly wana
nafasi kubwa ya kusonga mbele. Hata hivyo, maandalizi ya kuridhisha, safu ya
ushambuliaji na nguvu ya mashabiki vinaipa nafasi nzuri na uwezo Yanga wa
kuwaduwaza wamisri na kufungua ukurasa mpya.
Je,Yanga watakomesha ubabe wa Wamisri kwa timu za ukanda wa
Afrika Mashariki unawaofanya miaka nenda rudi waanzie huku? Mwaka jana walianza kampeni yao na Tusker ya
Kenya na kuchukua ubingwa, mwaka huu wamesogea kwetu dhidi ya Yanga. Au, je,
Yanga watakubali kufanywa ngazi ya waarabu kuelekea hatua ya makundi?
On paper, Al Ahly are still heavy favorites to progress to
the next round. They are the defending Champions, have a winning squad of
players who can do the job anywhere. But in Ngassa, Okwi and Hamisi Kiiza Yanga
have the necessary offensive power to upset the Egyptian giants.
Tukio la kukumbukwa ni kwamba timu hizi zilipokutana katika mchezo wa marudiano mwaka 1982 Uwanja wa Taifa(sasa Uhuru) na kutoka sare ya bao 1-1 bao la Yanga lilifungwa na Charles Boniface Mkwasa ambaye hivi sasa ni kocha msaidizi wa Yanga.Aidha katika mechi hii ilibidi Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania(FAT) kimfungulie golikipa Hamisi Kinye,ambaye alikuwa amefungiwa kwa utovu wa nidhamu, ili aweze kucheza mechi hii badala kipa Juma Mhina aliyedaka mechi ya kwanza mjini Cairo na yanga kufungwa 5-0
ReplyDeletepamoja sana
ReplyDeleteUnaziii....shaffih
ReplyDelete