Twiga
Stars imepoteza mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) baada ya leo kufungwa mabao 2-1 na Zambia
(Shepolopolo) kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.
Hadi
dakika 45 za kwanza zinamalizika katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi
Salma Mukansanga timu hizo zilikuwa suluhu.
Wenyeji
ndiyo walianza kupata bao lililofungwa na Hellen Mubanga dakika ya 75. Mfungaji
huyo aliyeingia kipindi cha pili nchini alimalizia wavuni mpira uliotemwa na
kipa Fatuma Omari.
Dakika
nne baadaye Zambia ambao walikuwa wakishangiliwa kwa nguvu na washabiki wao baada
ya kufunga la kwanza, walipata bao la pili ambalo nahodha wa Twiga Stars,
Sophia Mwasikili alijifunga mwenyewe.
Mwasikili
alikuwa akijaribu kutoa nje mpira uliopigwa na nahodha wa Shepolopolo, Mupopo
Kabange ambapo ulipishana na kipa Fatuma Omari kabla ya kujaa wavuni.
Bao
la Twiga Stars lilifungwa na Donisia Daniel dakika ya 90. Beki huyo wa kushoto
ambaye pia ni mchezaji wa Tanzanite alipanda mbele kuongeza mashambulizi ambapo
akiwa nje ya eneo la hatari alipiga shuti lililomshinda kipa Hazel Nali.
Akizungumza
baada ya mechi, Kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage alisema amebaini
upungufu katika kikosi chake ambao ataufanyia kazi kabla ya mechi ya marudiano
ili timu yake iweze kusonga mbele.
“Kwa
matokeo haya bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano
nyumbani na kusonga mbele,” alisema Kaijage.
Twiga
Stars iliwakilishwa na Fatuma Omari, Fatuma Bashiru, Donisia Daniel, Fatuma
Issa, Evelyn Sekikubo, Sophia Mwasikili, Vumilia Maarifa, Mwapewa Mtumwa/Amina
Ali, Asha Rashid, Etoe Mlenzi/Zena Khamis na Shelida Boniface.
Timu
hiyo inarejea nyumbani kesho kwa ndege ya Fastjet ambapo itatua kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7 kamili mchana.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Lusaka, Zambia
No comments:
Post a Comment