Na Baraka Mbolembole
AL AHLY NI KLABU YA DARAJA LA JUU...
Ni moja ya klabu tatu, Ulimwengu kutwaa mataji mengi zaidi ya Kimataifa. Al Ahly imetwaa mataji 16 ya kimataifa, inashika nafasi ya tatu nyuma ya timu za Boca Junior ya Argentina, yenye mataji 17, na AC Milan ya Italia yenye mataji 18. Pia, timu hiyo ya Misri ndiyo timu iliyofanikiwa kucheza mara nyingi zaidi michuano ya klabu bingwa ya dunia, Disemba, 2013 walishiriki kwa mara ya tano michuano hiyo. Hizo ni rekodi za kipekee kwa timu hiyo tajiri barani Afrika. Imeshatwaa mara nane taji la Ligi ya Mabingwa, huku mara mbili za mwisho wametwaa mfululizo taji hilo, 2012 na 2013. Ni klabu bora ya karne ya FIFA, barani Afrika. Imetwaa jumla ya mataji 125 katika miaka yake 106 tangu ilipoanzishwa.
HISTORIA ZILIWEKWA ILI KUVUNJWA.......
Al Ahly imetwaa mara nane ubingwa wa Ligi ya mabingwa Afrika, na ndiyo wanaoshikilia taji hilo kwa miaka miwili mfulizo. Yanga, mabingwa mara 24 wa ligi kuu ya Tanzania Bara, imeshatwaa mataji 36 hadi sasa tangu kuanzishwa kwake, mataji matano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na kati na mengine manne ya iliyokuwa michuano ya kombe la Tanzania ambayo mshindi wake alikuwa akiiwakilisha nchi katika michuano ya washindi barani Afrika. Pia wametwaa taji la Ngao ya Jamii mara tatu, huku rekodi hizo za mataji zikiwa bila yale ya vikombe vya Tusker.
Tangu, mwaka 1997, Yanga imeshiriki mara nane katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika, ilitolewa katika raundi ya awali, mwaka huo na timu ya Express ya Uganda, baada ya sare ya kutofungana jiji Dar es Salaam, timu hiyo iliondolewa kwa bao 1-0 jijini Kampala. Mwaka uliofuata, 1998 ulikuwa mwaka mzuri sana kwa Yanga kwa kuwa ilikuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufuzu kwa hatua ya nane bora. Achana na matokeo mabaya ya timu hiyo katika hatua ya makundi, Yanga ilitia fora baada ya kuziondosha Rayon Sports ya Rwanda, kwa sheria ya bao la ugenini, walipata sare ya mabao 2-2, Kigali na kufungana 1-1 jijini Dar.
Yanga wakafuzu kwa raundi ya pili na wakaichapa Coffee FC ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 8-3. Ikiwa na kikosi kikali, Yanga ilikwenda jijini Addis Ababa huku wakijua timu hiyo ya Ethiopia ilikuwa imetoka kuitoa mashindano Al Ahly ya Misri. Yanga walipata sare ya mabao 2-2 na kisha wakaichapa timu hiyo mabao 6-1 jijini Dar na kufuzu kwa hatua ya juu zaidi kwa upande wao na hadi sasa hawajafanikiwa kufika hapo. Wameishia katika raundi ya pili katika miaka ya 2001, na 2007, wametolewa katika raundi ya kwanza mwaka 2009 na washindani wao wa mwaka huu, na mwaka 2006 walitolewa katika hatua ya awali. Wameishia mara mbili mfululizo katika raundi ya awali katika miaka ya 2010, na 2012.
Katika miaka ya nyuma timu hiyo ya Yanga iiliweza kucheza robo fainali katika miaka 1969, na 1970 wakati michuano hiyo ikifahamika kama Klabu bingwa barani Afrika. Katika mfumo wa zamani Yanga ilicheza mara 11 michuano hiyo na jumla yake hadi sasa wameshacheza mara 19, na sasa wapo katika michuano yake ya 20 ya klabu bingwa Afrika.
YANGA vs AL AHLY MARA YA MWISHO ( AGGR. YANGA 0- 4 AL AHLY)
Ilikuwa ni mwaka 2009 wakati Yanga ilipokubali kipigo cha mabao 3-0 nchini Misri na kisha kufungwa bao 1-0. Baada ya kumalizika kwa mchezo wa kwanza jijini, Cairo, aliyekuwa mwenyekiti wa timu ya Yanga, Iman Madega aliingia katika mzozo mkubwa na aliyekuwa kocha wao, Dusan Kondic ambaye aliweka wazi kuwa timu yake haikuwa na ubavu wa kuwafunga Al Ahly. Baadae zikavuma tetesi kuwa kocha huyo alicheza mchezo mchafu, huku kipa Mserbia, Obren akionekana na kocha wake usiku mkubwa katika moja ya hotel wakiwa wamelewa kuamkia siku ya mchezo.
Kipa huyo afungwa mabao ambayo alizushiwa kuuza timu yake, haikuwahi kuwa kweli ila mchezo wa pili katika uwanja wa Taifa, ulionesha kuwa Yanga walikuwa wamepata matokeo wasiyostahili ugenini. Walipoteza kwa bao 1-0 ila waliweza kuonesha soka la uhakika siku hiyo. Mwaka, 2012 walitolewa kizembe na timu dhaifu ya Zamalek kutoka nchini Misri pia kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kufungana bao 1-1 jijini, Dar, Yanga walilala 1-0 ugenini na kuondolewa mashindanoni.
TIMU KUBWA AFRIKA ZINA MCHEZO MCHAFU....
Mmoja kati ya watu ambao walikuwa katika msafara wa timu ya Simba SC, nchini Misri, aliwahi kuniambia kuwa . Simba ilipitia mitihani mikubwa kabla ya kuwavua ubingwa Zamalek, mwaka 2003 katika uwanja wao wa nyumbani. Licha ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika uwanja wa nyumbani, Simba walifanya mipango mikubwa sana, pengine ilikuja kufanikiwa baada ya ujasiri wa aliyekuwa kocha James Siang'a.
Kwanza, waliondoka nchini mapema, na walipokuwa na kambi ya muda nchini Oman, walifanya mipango ya kupata maandalizi na mapokezi ya uhakika nchini Misri, kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini Misri, Simba waliweza kupata sapoti kutoka kwa watu wa Al Ahly, ambao ni wapinzani wakubwa wa Zamalek na timu hizo zilikuwa hazipendani kwa kuwa Zamalek ilikuwa ikitawala soka la Afrika,.
Simba walifika, Cairo na kupokelewa na mashabiki wa Al Ahly . Kwa mujibu wa rafiki yangu huyo, siku chache kabla ya mechi, Aliyekuwa kiongozi mmoja wa timu hiyo alimfuata kocha Siang'a na kumwambia kuwa kuna jambo anahitaji kuzungumza nae. James, aliitikia wito huo ila alikuwa kama mbogo mara baada ya kuambiwa ujumbe mmoja ambao hakuupenda kabisa. Alimuuliza kiongozi huyo, kama alikuwa anahitaji yote hayo hawakuwa na sababu si tu ya kufanya maandalizi makubwa ya mchezo huo bali wasingeenda kabisa Cairo. Kiongozi alimfuata kocha akamwambia, ' Jamaa wametoa millioni..., wanaitaka gemu hii' si dhihaka, ni kweli kabisa.
Siang'a akawaita wachezaji wake na baadhi ya viongozi ambao hawakuwa wamepata habari hiyo na kutoa mkwara mzito kuwa mtu yoyote ambaye atamuona karibu na kiongozi huyo, hasijiusishe kabisa katika mchezo huo. Wachezaji wakafungwa kuhusu dili hilo, wakaingia uwanjani pasipo kujua chochote na kupigana kiume na kufuzu nane bora mbele ya mabingwa watetezi. Wakati mwingine timu zetu zinakuwa na vikosi vya kushindana nje, ila mambo kama hayo yanakuwa yakikwamisha. Mara ngapi timu dhaifu zimekuwa zikizitoa Simba au Yanga pasipo kutegemewa. Unajua kwa nini Juma Kaseja alilia sana wakati Simba iliposhindwa kulinda ushindi wa mabao 3-0 katika dakika 45 mbele ya Al Ahly Shandy ya Sudan, mwaka uliopita.
Kamati zetu za mipango na ufundi katika timu hazina watu waaminifu sana. Ni kweli, Yanga walistahili kutolewa na Zamalek, mwaka juzi?. Mimi siamini sana kuhusu hilo ila naweza kusema kuwa mpira unahitaji kuongozwa na watu wenye tamaa ya mafanikio zaidi ndani ya uwanja na nje ya uwanja kiuchumi. Timu kama TP Mazembe ya DRC imekuwa ikizishinda timu za Kiarabu iwe nyumbani au ugenini, kwa kuwa wamekuwa hawanunuliki, nao wanahitaji kutwaa mataji makubwa. Tazama timu za Kenya, Rwanda, Uganda wakati mwingine zinatolewa kidhaifu sana hata kama zikianza na ushindi mzuri katika viwanja vya nyumbani. Huwa zinakuwa dhaifu katika ardhi ya kiarabu, huo si udhaifu wa kimpira au uwezo uwanjani. Ni udhaifu wa viongozi kuingia uwanjani wakiwa na lengo la kuuza mechi kwa timu hizo ambazo malengo yao si kufika robo fainali bali kutwaa kabisa taji.
Kwa, Yanga wanaweza kujifunza kutokana na makosa yao na kuvunja mwiko kwa Waarabu ila kamati zao za maandalizi zikiingia katika biashara watachapwa na kuondoshwa mashindanoni. Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kuulizwa swali na Wazungu....Walimuuliza amewezaje kuwaongoza wananchi wake katika utaratibu ambao akiwaambia kitu wanamsikiliza na kumtii..., Mwalimu, alikuwa mtu wa utani sana...., Akacheka kidogo, sijui ilikuwa ni kicheko cha dhihaka au vipi..., Akawaambia wageni wake, naombeni muinuke katika viti vyenu..., Wale wageni wakainuka..., Akawambia tena, naomba mtabasamu kidogo..., wakatabasamu,,,, Akawambia, naombeni mcheki kidogo..., wote wakawa wanacheka..., Akawaambia wakae, Chini, wote wakakaa.... Mwalimu, bwana ( mungu amrehemu). Mwisho akawajibu wale Wazungu, ' Raia wangu wananisikiliza na kuniheshimu kama ninyi', Kila, alichowaambia si wamefanya.
Tafakari, kwa nini kikosi cha millioni 500 cha Kondic kilikuwa ' nyanya' kwa Al Ahly, 2009. Na Simba walivukaje mbele ya Zamelek... Bora ' kunyongwa' na waamuzi kuliko viongozi wetu wenyewe.
No comments:
Post a Comment