United ilipata kipigo cha saba msimu huu katika uwanja wa Stamford Bridge mbele ya Chelsea, na watakuwa na michezo dhidi ya timu za Cardiff City katika uwanja wa Old Trafford, jumanne ya wiki ijayo, na kusafiri hadi katika uwanja wa Brittannia kucheza na Stoke City siku ya tarehe mosi mwezi februari, na kurudi nyumbani kucheza na Fulham, jumapili ya tarehe 9. Ni mwezi ambao watacheza pia na Arsenal tena zikiwa siku tatu tangu watoke kucheza na Fulham. Arsenal iliyo katika kiwango cha juu kwa sasa itaikaribisha United, usiku wa jumatano katika uwanja wa Emirates. United wacheza pia na C. Palace katika mwezi ujao kabla ya kuwavaa mahasimu wao City katika uwanja wa Old Trafford, tarehe moja mwezi machi.
Baada ya kufungwa na Chelsea, United ni kama tayari wametupwa nje ya nafasi ya kutwaa ubingwa, kwa asilimia ndogo wanaweza kuamsha presha kwa timu zilizopo juu, ila si kwa mwenendo huu ambao timu imeonekana kuwa nyanya, huku kiwango cha kujiamini, kujituma, kikiwa kimeshuka mno kutoka kwa wachezaji ambao walimaliza msimu uliopita kwa tofauti ya pointi tisa dhidi ya timu iliyokuwa imemaliza katika nafasi ya pili. Mafanikio ya Alex Ferguson kama kocha wa klabu hiyo hayakutokana na uzuri wa wachezaji waliofanya nae kazi, bali aliwafanya kila mchezaji kujua jukumu lake kwa uhakika. Wakati anaondoka alisema kuwa si vigumu kuziba pengo lake huku akijiamini kuwa ameacha mkusanyiko mzuri wa timu yenye wachezaji vijana na wazoefu. Na alipotangazwa David kurithi nafasi yake akasema kuwa United ilihitaji ' mtu wa manchester' hasa.
David Moyes beki wa kati wakati wa uchezaji wake, aliigeuza Everton kuwa timu ngumu kufungika katika ligi ya England. Hii ni sehemu ambayo alikuwa na uzoefu nayo mkubwa. Viungo walipangwa vizuri katika maeneo ya kujilinda, na hicho ndicho pekee alichofanikiwa kufanya akiwa Everton, na ndiyo maana alifanikiwa. Ana umakini na hisia za ndani za kutokubali kushindwa. Nadhani, David atafanya vizuri hata kama United inafanya vibaya katika siku za karibuni. Makocha imara hufanya mabadiliko bila hofu na si wale dhaifu. David si kocha dhaifu ila alishindwa kuwa imara katika hilo katika uteuzi wa timu iliyopaswa kuanza mchezo dhidi ya Chelsea. Mabadiliko yake ya kwanza yalikuwa ni yale ya dakika ya 51, Chriss Smalling alipoingia kuchukua nafasi ya Patrice Evra ni wakati ambao United walikuwa nyuma kwa mabao 3-0.
Dakika tano baadae akamuingiza uwanjani, mshambuliaji Javier Hernandez kuchukua nafasi ya Ashley Young. Yalikuwa ni mabadiliko mazuri kwa kuwa United ilirudi katika mfumo wake halisi wa 4-4-2, Hernandez akaenda kucheza sambamba na Dany Welbeck, huku Antonio Valencia na Adnan Januzaj wakicheza sehemu za pembeni. Japo walionekanma kucheza mchezo wa kasi katika dakika 10 za mwanzo, United ilionekana kukosa mtu sahihi wa kusimama na kufunga mabao. Welbeck aliyepewa jukumu hilo aliishia kucheza kama kiungo mshambuliaji na kuwa anarudi zaidi hadi katikati na kucheza pasi. Hakukuwa na mtu kila mpira ulipopenyezwa katika eneo la namba tisa. Akaanza kuchoka, akawa mzigo.
David alipaswa kumuanzisha Hernandez pamoja na Welbeck, na Smalling katika nafasi ya ulinzi wa kulia ili kuisogeza timu mbele. Matokeo yake nafasi hizo wakapewa Young, na Rafaer Da Silva. Young aliishia ' kunawa' mipira aliyokuwa akipasiwa na wenzake na Rafael hakupiga krosi hata moja kwa muda wote wa mchezo. Evra alikuwa uchochoro, na Chelsea walitengeneza mabao yao yote kupitia upande wake. Shinji Kagawa na Darren Fletcher walikuwa katika benchi kwa dakika zote kumpisha Young ambaye ameonesha kiwango kingine cha chini. David alichemsha vibaya kwa mara nyingine katika uchaguzi wa wachezaji wa mechi kubwa.
Mkanganyiko uliopo sasa sio suala la mbinu gani ambazo, David anapaswa kutumia na nani hasa anapaswa kucheza au kuihama timu hiyo. Maswali mazito baada ya kipigo kutoka kwa Chelsea yanahusu kuhusu utaratibu wake wa mafunzo, mabadiliko anayofanya katika safu ya ulinzi, kiungo na mashambulizi, na mahusiano yake na wachezaji. Ukarimu aliokuwa nao Ferguson katika kutatua matatizo ya vipigo ni tofauti kabisa na David. Fergie hakusita kuhoji waziwazi kama wachezaji wake wanajituma pale wanapofanya vibaya. Wapo wanaotilia shaka mbinu za David kwa kuwa hakuna maelewano katika ukabaji, na hali hiyo ilidhihirika walipochikwa mabao matatu na Samuel Eto'o hata hivyo kupoteza mechi saba tu katika michezo 22 ni dalili kuwa David anafanya vizuri.
Huu ni wakati mbaya zaidi katika kazi yake, bahati mbaya presha anayoipata ni kutoka katika timu kubwa duniani. UNited inakosa nini? Sababu ni nyingi, majeraha ya wachezaji, kushuka viwango kwa baadhi ya wachezaji, na hasa suala la mbinu za kuzikabili timu kubwa. Waliadhibiwa bao la kwanza katika dakika ya 16, mpira wa pili kupigwa na mchezaji wa Chelsea katika lango lao, wakafungwa bao la pili katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza, na wakafungwa bao la mwisho katika dakika ya nne baada ya kuanza kipindi cha pili. Hiyo inamaanisha kuwa timu hiyo aina mipango mizuri kiufundi. Viungo wake Michael Carrick na Phill Jones walionekana kupiga pasi ndefu za Kiingereza, ila mbinu za Jose Mourinho ambaye aliamua kuanza na Wabrazil wanne katika idara ya kiungo, huku watatu kati yao wakiwa na asili ya ukabaji, ulikuwa ni mtihani mkubwa kwa David na ni hapo ndipo ambako unaweza kuona umuhimu wa Kagawa na Fletcher kuanza mchezo.
United waliteswa na David Luiz, ambaye aliwalinda walinzi wake wa kati na yule wa upande wa kushoto, William ambaye alicheza pembeni kidogo upande wa kushoto, na Ramirez upande wa kulia wote hawa waliipandisha timu kwa nguvu na hata mipira yao mingi iliyokwenda kwa Oscar na Eden Hazard ikiwa ni mizuri. Viungo hao wa mashambulizi walikuwa na kasi na waliamu kupitia kwa Evra kila mara baada ya kuona ugumu kidogo wa kufanikisha mipango yao upande wa Rafael. United inatakiwa kusajili, ila nani mchezaji wa Manchester sokoni?. Unaambiwa mtu avukae nguo, asipochutama hujitukanisha mwenyewe kwa kwenda uchi mbele za watu. David anatakiwa kuchutama sasa na kurudi katika mbinu za Ferguson.
No comments:
Post a Comment