WAKATI nasoma shule ya Msingi miaka ya nyuma, familia yangu ilifurahia sana matokeo yangu ya mitahani kwasababu mara nyingi nilikuwa nashika nafasi ya kwanza kwenye darasa la wanafunzi zaidi ya 80.
Nakumbuka furaha ilikuwa inaongezeka zaidi pale ninaposhika nafasi ya kwanza katika mitahani ya ujirani mwema iliyonikutanisha na zaidi ya shule mbili.
Hata mimi nilikuwa nafurahia mafanikio yale na kusahau kuwa kuna upande wa pili wa shilingi. Ikafika wakati mambo yakaenda vibaya sana, nikashuka uwezo kutokana na kuvimba kichwa na kuacha kujisomea kama awali.
Kilichonipa kiburi ni kwamba, kuna
siku nilienda kufanya mtihani bila hata kusoma, nilipasua `pepa` vizuri sana.
Nikapunguza kasi ya kujisomea na kujiamini zaidi. Balaa lilitokea baadaye ni
siri yangu, lakini nikajipanga upya na kurudi mchezoni.
Mbali na kuacha kujisomea, wanafunzi
wenzangu kumbe walikuwa wananionea wivu sana, hakika walikuwa wanapiga kitabu
sana ili kunishusha. Walifanikiwa kwa kipindi kifupi sana.
Kwa kipindi kile, baba yangu
alichukia sana kushuka kiwango katika masomo. Alinigombeza kila wakati kwanini
nimebadilika. Niliumia na kumwona kama `anazingua` tu.
Baadaye alinivumilia na kunipa muda
wa kurekebisha makosa yangu, nikajipanga vizuri zaidi kurudi kwenye
mchezo ule wa ushindani na kufanikiwa.
Kutokana na hali ile, nikajifunza
kuwa mimi nilikuwa sawa na mchezaji niliyopo kwenye kiwango cha juu. Familia yangu
iliyokuwa ikifurahia mafanikio yangu ni sawa na mashabiki wa soka. Wanafunzi
waliopambana na mimi ni timu nyingine za ligi.
Nikiyakumbuka haya, nafananisha
matokeo ya klabu ya Mbeya City waliyoyapata ligi kuu soka Tanzania bara
mzunguko wa kwanza.
Hakika timu hii ilikonga nyoyo za
watu kutokana na kasi yake, morali kubwa kwa wachezaji na mfumo bora wa kocha
wake Juma Mwambusi kuwaamini vijana wadogo ambao baadhi ya timu zisingethubutu
kutoa nafasi kwao.
Wakiwa katika kiwango cha juu,
walifanikiwa kumaliza mzunguko wa kwanza bila kufungwa mchezo wowote. Walifanya
vizuri ugenini na nyumbani , hivyo kujikusanyia pointi 27 katika nafasi ya tatu
sawa na Azam fc katika nafasi ya pili, huku kileleni akiwepo Bingwa mtetezi,
Dar Young Africans kwa pointi 28.
Kutokana na ubora wa Mbeya City
kuanzia wakati inacheza ligi daraja la kwanza mpaka inapanda ligi kuu kwa msimu
huu kwa mara ya kwanza, timu hii ilijizolea umaarufu na mashabiki wengi mkoani
Mbeya na nje ya Mbeya.
Kama ni mshale kusoma, basi idadi ya
mashabiki ilikuwa inaongezeka kwa kasi ya mwanga wa rad, lakini hali hii
ilitokana na mafanikio ya klabu kwa wakati ule.
Niliwahi kufanya mahojiano marefu na
makocha wa timu hii, yaani kocha mkuu Juma Mwambusi na msaidizi wake, Maka
Mwalwisyi.
Mwambusi kwa upande wake aliwahi
kunieleza kuwa Mbeya City ni timu yenye falsafa mpya kabisa kulinganisha na
timu nyingine.
Nilipomuuliza ni falsafa gani?,
alijibu kirahisi sana kuwa wanaamini katika soka la vijana na kutengeneza mfumo
wa kuibua makinda na kuwapandisha timu A ambayo pia huwezi kusema ni ya wakubwa
kwani imejaza vijana.
Nilichukuu moja ya nukuu muhimu
kutoka kwa Mwambusi ambayo ni;
“Mchezaji yeyote unayemsikia duniani
iwe kitaifa au kimataifa, anawika kwasababu aliaminiwa na kupewa nafasi
ya kucheza mpira”. “Najua ni ngumu na inahitaji kuvumilia kutokana na makosa
makubwa ya wachezaji vijana, lakini lazima uwape nafasi ili sikuikifika
waje kuitwa wachezaji wenye uzoefu”.
Yalikuwa maneno mazito kwangu na
ndipo nilipoanza kukichunguza kikosi chake. Niligundua ni kweli amewapa nafasi
vijana wadogo sana ambao hawana majina. Mfano,; Alex Seth, Deus Kaseke, Hassan
Mwasapili, Peter Richard, Jeremiah John, Kenny Ally, Deogratius Julius na
wengine wengi.
Pia nikagundua kuwa kilichokuwa
kituo cha cha soka la vijana cha `Forest Youth Soccer Academy` (FOYSA) chini ya
mkurugenzi wake Maka Mwalwisyi ambaye kwa sasa ndiye msaidizi wa Mwambusi ,
kilibadilishwa na kuwa mradi wa Mbeya City. Vijana wa kituo hiki wameunda
kikosi B cha Mbeya City na sasa klabu imekuwa na uhakika wa kupata vijana kwa
wakati wote.
Kwasababu vijana waliaminiwa na
kocha Mwambusi, basi nao waliucheza mpira na kumlipa fadhila wakati wa mzunguko
wa kwanza.
Imani kubwa na kujitoa mhanga kwa
Mwambusi ndiko kulimfanya awe maarufu zaidi, ingawa alikuwa maarufu kutokana na
rekodi yake akiwa na Tanzania Prisons pamoja na timu ya mkoa wa Mbeya,
Mapinduzi Stars iliyokuwa inashiriki kombe la Taifa ambalo kwasasa
halipo.
Baada ya kupata mafanikio ngwe ya
kwanza, mashabiki waliongezeka zaidi na kuanza kumpenda kocha huyu na timu
yake.
Lakini kuna wakati nilikuwa Uwanja
wa sokoine kushuhudia mchezo wa ligi kuu baina ya Mbeya City dhidi ya Ruvu
Shooting uliomalizika kwa ushindi wa 2-1 kwa Mbeya City. Katika mchezo huu City
walipata bao la ushindi dakika za mwisho.
Kabla ya bao hilo, mashabiki
walikuwa wanazomea wachezaji na kusogea eneo la benchi la ufundi na kumwimbia
Mwambusi nyimbo za kejeli wakimtaka mchezaji anayeitwa Kenny Ally, huku
wakisema kama atatoa sare hapataeleweka na wengine wakisema wachezaji watakula
mboko.
Niliporejea kwenye orodha ya
wachezaji wa kikosi cha kwanza na wa akiba, niligundua Kenny hakuwepo kabisa
katika mipango ya mwalimu katika mechi ile.
Nilishituka sana kwasababu ilikuwa
mapema sana. Baadaye Mwambusi aliwaita mashabiki wanywa pombe na hawatumia
akili. Wengi walimshangaa kocha huyu kwa kitendo kile cha kuonesha ishara ya
kuwaambia hawatumii akili.
Baadaye timu ikapata ushindi,
walewale waliokuwa wanazomea wakageuka kuwa wa kwanza kushangilia na kumsifu
Mwambusi.
Binafsi nilipata fundisho kubwa kuwa
inawezekana mashabiki wa Mbeya City ni watu wa kufurahia mafanikio kama
ilivyokuwa kwa familia yangu wakati nasoma shule ya Msingi.
Utoafuti ni kwamba wazazi wangu
walinigombeza kwa lugha nzuri na kunipa matumaini, lakini si kama wao kuzomea
na kutishia kuwapiga wachezaji kama watapata sare nyingine nyumbani.
Kama walichukia sare mapema vile na
timu yao ilimaliza vizuri mzunguko wa kwanza, endapo mambo yatageuka kwao
, watavumilia kweli?.
Mashabiki wa Mbeya City unaweza
kusema wamezoe kushangilia matokeo na hawajapata zahama kama ilivyokuwa kwa
wenzao, Rhino Rangers na Ashanti United ambao walichezea vichapo vingi.
Sisemi Mbeya City watafanya vibaya,
lakini najaribu kutafakari kama watavumilia matokeo mabaya kwa timu yao au ndio
itakuwa mwisho wa kukodi mabasi madogo ya abiria na kusafiri kuifuata timu yao
popote pale.
Wataendelea na kasi ile au
watachoka?, Majibu ni magumu kupata kwani kitendo kile kilichotokea kwenye
mchezo wa Shooting kilinipa shida na mpaka sasa wasiwasi ni mkubwa
kwangu.
Sina hakika kama mashabiki hawa
wanaelewa kuwa mpira wa miguu ni mchezo unaobadilika. Leo unaweza kufurahi,
kesho ukainamisha kichwa chini.
Sawa na mashabiki wa Manchester
United waliozoea ushindi wakati wa Sir Alex Ferguson, lakini kwa sasa mambo
yamebadilika wakati wa David Moyes. Kwa wale wenye mioyo laini, wameshakata
tamaa, lakini mashabiki wa kweli bado wanaendelea kuishabiki timu yao.
Vipigo kwenye soka vipo. Ulijua
Arsenal kwa ubora wao wangelala 6-3, au Tottenham Hotspurs kula 5-0 kutoka kwa
Manchester City?. Ndio mpira ndugu zangu na huwa iko hivyo.
Kwa hawa mashabiki wa Mbeya City
ambao wanafura na hasira kama mbogo pale timu inapoelekea kupata sare
tena mechi za mwanzo kabisa tangu waingie ligi kuu, hakika ninakuwa na wasiwasi
mkubwa kuwa wanaweza kusambaratika kipindi timu yao ikianza kula vipigo.
Sitaweza na sitawahi kuitabiria
mabaya timu yoyote, lakini kwa utamaduni wa mashabiki wa Tanzania kushindwa
kutoa muda kwa wachezaji wao na kukosa uvumilivu katika ujenzi wa timu, nakuwa
na wasiwasi kama mashabiki wa Mbeya City watavumilia endapo wataanza kufungwa.
Labda wafanye kitu kimoja.
Wanatakiwa kukaa pamoja na kuelezana, kupeana semina, kujengana kisaikolojia
kuwa si kila wakati watakuwa wanapata matokeo ya ushindi.
Wakubali kuwa soka lina kupanda na
kushuka. Wajifunze kuwa na subiri na kujenga imani kwa wachezaji wao pamoja na
makocha wao.
Mipango ya Mwambusi na Mwalwisyi iko
wazi, wanatakiwa kupewa muda wa kutosha kwani wanaonekana kuwa na mawazo
tofauti na timu zetu za Simba ambazo hazina uvumilivu.
Kinachotakiwa ni kujiandaa kwa
lolote lile, kama mipango yao itashindikana mzunguko wa pili, mashabiki
wanatakiwa kuendelea kuisapoti timu kwa namna ile ile ya Chamazi kwenye mechi
ya mwisho mzunguko wa kwanza dhidi ya Azam fc iliyomalizika kwa sare ya mabao
3-3, huku Mwagane Yeya akipiga matatu `Hat- Trick`.
Kama wataendekeza fitina na
majungu, maneno makali kwa makocha na wachezaji, itabaki kuwa historia tu kuwa
waliwahi kutamba. Mashabiki waelimishwe na kubadilu fikira za kufurahia ushindi
na kusahaua upande wa pili wa shilingi.
Bado nina imani na kikosi cha Mbeya
City kuwa kinaweza kufanya vizuri mzunguko wa pili. Lakini rekodi ya
kutofungwa `unbeaten` sina hakika kama itaendelea.
Naamini mipango yao ni sahihi,
wapo katika maandalizi mazuri. Kikosi ni kile kile, hakuna mabadiliko
yoyote. Wachezaji wakiendelea kujituma na kucheza kwa kasi ile ile, bila shaka
wataweza kupambana kwa wakati wote.
Wachezaji watatakiwa kuendelea
kuucheza mpira bila kujali kelele za kushangiliwa au kuzomewa. Ije kuwa mwiko
kwao kucheza na jukwaa huku wakilewa sifa za mzunguko wa kwanza kwani ni ngumu
kwao kuja kutambua timu nyingine zimeandaaje majeshi yao.
Kuna siku aliyewahi kuwa kocha
msaidizi wa Yanga, Fredy Felix Minziro aliniambia mzunguko wa pili Mbeya City
watayeyuka mithiri ya barafu juani.
Akaniambia timu nyingine ikiwemo
Yanga, zitaingia kwa kasi, zitapambana na Mbeya City kwa kufuta fikira kuwa ni
timu changa na ngeni katika michuano ya ligi kuu.
Maneno ya Minziro yalimaanisha, timu
zenye uzoefu zilikuwa zinaingia uwanjani kwa kuzidharau timu mpya za Mbeya
City, Ashanti United na Rhino Rangers.
Kwa Ashanti na Rangers timu zenye
uzoefu zilifanikiwa kushinda, lakini Mbele ya Mbeya City, mambo yalikuwa magumu
zaidi na hakuna timu iliyofua dafu.
Kama Mbeya City wamekaa chini na
kugundua kuwa watakuwa na changamoto kubwa mzunguko wa pili, basi
yawezekana maneno ya Minziro yakabaki kuwa ndoto.
Lakini kama wamebweteka na kujiona
wameweza, basi yanaweza kuwakuta ya JKT Oljoro ambao walikuja kwa kasi misimu
ya nyuma na kuongoz aligi, lakini wakageuka kitowea mpaka sasa.
Cha msingi mashabiki, wachezaji,
benchi la ufundi na viongozi wakae pamoja kuunda nguvu ya kuanza nayo mzunguko
wa pili.
Kama watashindwa kukaa na kujipanga,
halafu wakaingia kirahisi na kufungwa zaidi, hapo ndipo hofu yangu inaibuka
kuwa Mbeya City inaweza kupotea.
Vizuri zaidi, makocha wake
wameonekana kugundua kuwa wapo katika changamoto kubwa na ndio maana waliingia
kambini mapema na sasa wanaenda kucheza kombe la Mapinduzi huko Zanzibar.
Tusubiri wakati ufike, ili
tujiridhishe na uwezo wao na maneno yao. Mpira sio siasa za mdomoni bali
unachezwa hadharani Uwanjani.
Aliyewahi kuwa kocha wa
mabingwa wa zamani wa Afrika, timu ya Taifa Zambia, Chipolopolo, Mfaransa,
Herve Renard, wakati akijiandaa na mchezo wa fainali ya AFCON dhidi ya
Ivory Coast alisema mpira wa miguu ni mipango, mwenye kujipanga na kuwa makini
anaweza kuibuka na ushindi.
Akasema Ivory Coast na Zambia hakuna
ushindani ukiangalia majina ya nchi katika viwango vya ubora vya FIFA , hata
aina ya wachezaji waliopo, lakini akasema anaenda kutafuta matokeo mbele
yao. Kweli walifanikiwa.
Hata Mbeya City licha ya uchanga wao
wanaweza kupambana na klabu za Simba sc, Yanga na Azam fc katika
kinyang1anyiro cha ubingwa na kutwaa taji kwa mara ya kwanza, hivyo kuvunja
rekodi ya Tukuyu Stars iliyowahi kupanda ligi kuu na kutwaa ubingwa msimu huo
huo.
No comments:
Post a Comment