JE, ushawahi kusikia msemo wa kisoka
uitwao “Sexy Football”, ama kwa Kiswahili soka lenye mvuto wa kimapenzi?
Sasa BLOG yako inakukutanisha na mwanzilishi wa soka laini lenye mvuto,
soka ambalo limetumiwa vyema na mabingwa wapya wa kombe la dunia
Hispania, kujibebea ndoo za Ulaya na dunia kwa ujumla. Hapa namzumgumzia
si mwingine bali muholanzi Ruud Gullit.
hapa ilikuwa ni baada ya mazungumzo marefu na Gullit ( kulia ) pamoja na Steve Mcmanaman.
Lakini
mara nyingi umekuwa ukitamka kuwa hakuna mahala umewahi kufurahia
kuishi katika maisha yako ya kisoka zaidi ya jijini London. Ni kwa
sababu gani?
Sitokuja kusahau maisha ya London
na katika klabu ya Chelsea kwa ujumla kwani kwanza kocha Glenn Hoddle,
alikuwa akinisikiliza na kunichezesha nafasi niliyoizoea, pia nilipata
sapoti kubwa sana toka kwa wachezaji wenzagu kina Mark Hughes na Dan
Petrescu.
Hebu tuambie kuhusu staili hii ya uchezaji wa “total football” ama kama unavopenda kuiita “sexy Football”
Mimi nilikuwa mchezaji wa aina
yake kwani nilikuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi niwapo uwanjani.
Niliweza kucheza kama beki wa kati, beki wa pembeni kiungo mkabaji,
kiungo mshambuliaji na hata straika. Niliweza kufanya hivi sababu
nilikuwa na spidi, nguvu na uwezo mkubwa hewani. Sasa staili hii ya
uchezaji wangu ndio iliyowafanya makocha kuanza kuiga katika timu zao.
Ruud Gullit akiwa na Glenn Hoddle enzi hizo anachezea Chelsea.
Historia
yako kama kocha imejaa milima na mabonde toka enzi za Chelsea, lakini
tuko na mshawasha sana wa kujua kilichotokea Marekani na LA Galaxy?
Unajua
soka la kimarekani liko tofauti kidogo tukianza ma masuala yao ya
kuweka viwango vya mishahara na sheria za uhamisho na usajili wa
wachezaji. Mimi nilifika pale mwaka 2007 na malengo na mipango yangu ya
kuifikisha mbali LA Galaxy. Ila kulikuwa na wafitini ambao walidhani
mimi nimeletwa pale na Beckham na wala sikustahili hivyo walinipikia
jungu hadi ikasababisha niondoke.
Vipi kuhusu Celestine Babayaro?
Celestine alikuja Galaxy kwa
maombi yangu. Celestine alikuwa mchezaji mzuri sana na mwenye kipaji
lakini alikuwa akiandamwa na matatizo mengi sana nje ya uwanja hivyo
ilimuwia vigumu kuwa makini pale klabuni, ilibidi tu aondoke.
Sasa turudi kwenye “Sexy Football” unadhani staili hii ndio iliyowaangusha waholanzi katika fainali ya kombe la dunia 2010?
Siwalaumu vijana waliocheza mwaka
huu, siwalaumu hata kidogo. Timu ya Uholanzi mwaka huu tofauti na miaka
mingine haikuwa ikicheza soka lake la siku zote la kushambulia. Mwaka
huu kocha alifanya kitu sahihi kwa kuwafundisha vijana wake kucheza soka
chafu ili mradi ushindi. Kilichowaangusha ni kuwa Wahispania walikuwa
makini zaidi; ni hicho tu.
Nini kifanyike Waholanzi waache kuishia kufungwa tu katika fainali kila wakati?
Kwanza napenda kumpongeza kocha
Bert Van Marwijk, ametengeneza timu nzuri sana yenye vijana kama kina
Van Persie, Robben, Elia na wengineo. Vijana hawa ambao tayari wana
uzoefu wa mashindano makubwa ndio watakaojenga timu ya kesho ambayo
itakuwa tayari imekwishajifunza toka katika fainali ya mwaka huu.
Yanahitajika mabadiliko kidogo tu Uholanzi ni timu nzuri tayari.
Unaenjoy kuwa mchambuzi wa soka zaidi ya kucheza?
Nishakuwa mzee sasa hivi hata
danadana kumi sifikishi (anacheka). Nafurahia kila mara sababu inanipa
nafasi ya kutumia utaalamu wangu wa ukocha kuchambua mechi na kuwapa
burudani wapenzi wa soka. Pia inanifanya nisafiri sana na kukutana na
watu wengi tofauti kama nilivyokutana na wewe hapa Sauzi.
Ulifikiria nini kutoa ule wimbo uliokamata chati za muziki mwaka 1988?
Kipindi kile kulikuwa na vitendo
vingi sana vya ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa watu weusi. Hata mimi
mweneywe ilikwishanikumba uwanjani nikiwa nachezea Feyernoord wakati
huo tulikuwa katika mechi dhidi ya ST Mirren. Mashabiki walinizomea
sababu ya rangi yangu. Hii iliniuma sana. Nililia sana siku ile.
Ikichangiwa na vitu kama kufungwa kwa Mandela n.k niliona ni wakati
mzuri wa kutoa wimbo wa kupinga vitendo hivi.
Kwa kumalizia mzee nasikia una watoto sita ni kweli?
Yes! Nina watoto sita niwapendao
kuliko chochote hapa duniani. Wa kwanza anaitwa Felicity na mdogo wake
Charmayne hawa nilizaa na Yvonne de Vries. Wa tatu anaitwa Quincy na wa
nne Sheyenne hawa wana mama yao pia aitwaye Cristina Pensa. Mke wangu wa
sasa anaitwa Estelle Cruyff ambaye kama jina linavyoonesha ni mpwa wa
Johan Cruyff. Huyu tumezaa nae watoto wawili pia Maxim na Joelle. Maxim
nimekuja naye hapa Sauzi yuko hapo nje anacheza.
Shukrani sana Ruud Dil Gullit
Asante nawe pia, karibu Holland siku moja.
No comments:
Post a Comment