Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KUPOTEZA muelekeo kwa klabu ya Jeshi ya JKT Oljoro ya jijini Arusha kumemfanya kocha wake mpya, Hemed Morroco kuwa na kazi nzito ya kurudisha morali ya wachezaji wake ili warudi mchezoni katika mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara unaorajia kuanza januari 25 mwakani.
Akizungumza leo hii, kocha Morroco amesema kuwa ameipokea timu ikiwa nafasi ya 11 ikijikusanyia pointi 10 tu, hivyo kazi yake kubwa ni kuandaa kikosi cha mapambano na kuinusuru timu isishuke daraja.
“Nina changamoto kubwa sana, lakini ndio maana nipo hapa kuhakikisha timu inarudi nafasi nzuri. Kwasasa najaribu kubadili mfumo wa uchezaji na kurekebisha makosa yaliyokuwepo katika kikosi”. Alisema Morroco.
Kocha huyo aliyekuwa anaifundisha Coastal Union Mzunguko wa kwanza aliongeza kuwa usajili alioufanya dirisha dogo utamsaidia kurudisha makali ya JKT Oljoro na mpaka sasa wachezaji wote wapo kambini kujiwinda na ngwe ya lala salama.
Morroco aliwataja wachezaji aliowaongeza katika kikosi chake kuwa ni Jacob Masawe, Mansour Ali, Juma Mohamed, Amour Mohamed, Mohamed Ali, Mussa Nahoda, Benedict Ngasa, Seleman Makame, Shija Mkina, Ali Omar na Shaweji Yusuf.
“Ligi imekuwa ngumu sana, ushindani ni mkubwa. Nilikuwa na Coastal Union mzunguko wa kwanza, nilishuhudia namna timu zinavyoshindana. Nafikiri changamoto ni kubwa, lakini mimi ni Kocha, naikubali kazi hii na lazima niisaidie timu”. Alisema Morroco.
Aidha, Morocco alisema wachezaji wa Oljoro wanaonekana kuwa na ari kubwa licha ya kupoteza muelekeo katika mzunguko wa kwanza.
“Najaribu kuwarudisha mchezoni ili wafanye kazi kama walivyokuwa wanafanya awali. Hii inawezekana na ndio maana tupo kambini mapema kutafuta nguvu za kuanza nazo januari 25 mwakani”. Alisema Morocco.
Katika mzunguko wa kwanza, JKT Oljoro ilimaliza katika nafasi ya 11 ikijikusanyia pointi zake 10 kibindoni, sawa na Ashanti United waliopo nafasi ya 12, lakini tofauti yao ni wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Oljoro ilishinda mechi mbili tu (2), ikitoa sare nne (4), na kupoteza michezo saba(7), hivyo Morroco ana kazi kubwa ya kusaka ushindi zaidi ngwe .
Nafasi waliyopo Oljoro ni hatari tupu, kwani wakizembea watajikuta katika dhahama ya kushuka daraja, ingawa michezo 13 iliyosalia wanaweza kurekebisha mambo na kujiweka katika mikono salama.
No comments:
Post a Comment