Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
VIBONDE wa ligi kuu soka Tanzania bara, Mgambo Shooting ya mkoani Tanga imeanza mazoezi ya kujiandaa na mikikimikiki ya kukwepa mkasi wa kushuka daraja msimu wa 2013/2014.
Akizungumza leo baada ya mazoezi ya timu hiyo, kocha msaidizi , Moka Shaban Dihimba amesema wameongeza wachezaji wanne katika dirisha dogo la usajili, hivyo watakuwa na nguvu mpya.
“Tulikuwa na mapungufu mengi, wachezaji walikuwa na hofu kubwa, ndio maana tulifanya vibaya na kushika mkia. Tumewasajili Suleiman Khatib, Bolly Ajali, Amri Sambinga na Issa Ali ambao watatusaidia kupambana kufa na kupona”. Alisema Dihimba.
Dihimba alisema mazoezi yanakwenda vizuri chini ya kocha mkuu, Ramadhan Kampira na kikubwa wanachofanya kwa sasa ni kutafuta kasi na kumiliki mpira ili kuzikabili timu pinzani kwa umahiri.
“Timu za ligi kuu si kwamba zina mpira mkubwa sana, zote zinacheza soka la kawaida na sisi tunaweza kuwamuda kabisa. Nakuhakikishia kuwa kwa mechi 13 zilizobaki, tutabaki ligi kuu”. Aliongeza Dihimba.
Kocha huyo alikiri kufanya vibaya zaidi mzunguko wa kwanza kwasababu walishinda mchezo mmoja tu, wakatoa sare tatu na kufungwa mechi tisa, hivyo kujikusanyia pointi 6 tu katika nafasi ya mwisho.
Alipoulizwa kwanini timu imekuwa na matokeo mabaya hata msimu wa mwaka jana, Dihimba alieleza kuwa wachezaji wao wanakosa uzoefu na wanatawaliwa na hofu hasa wanapokutana timu kubwa.
“Tunakaa na wachezaji kwa muda mwingi na kuwaelekeza nini cha kufanya, lakini wamekuwa wakifanya makosa makubwa yanayoigharimu timu. Wana makosa ya kiufundi na tumeyaona, lakini kwa sasa tumejipanga vizuri kushindana”. Alitamba Dihimba.
No comments:
Post a Comment