Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MABINGWA watetezi wa kombe la Mapinduzi, klabu ya Azam fc imetamba kwenda kutetea taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo katika michuano inayoanza kutimua vumbi januari mosi mwakani.
Jafar Idd Maganga, Afisa habari wa klabu hiyo amesema panapo majaaliwa timu hiyo inatarajia kung`oa nanga jijini Dar e salaam januari 1 mwaka huu kuelekea visiwani Zanzibar tayari kuanza harakati za kutafuta kombe hilo.
“Michuano hii ni muhimu sana kwetu. Kocha mkuu Mcameroon, Joseph Marius Omog atakuwa na nafasi nyingine ya kupima kikosi chake na kuelewa wapi kuna matatizo ili kuiandaa timu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara na michuano ya kimataifa”. Alisema Jafar.
Jafar aliongeza kuwa tangu timu ipate kocha mpya, wachezaji wamekuwa wakipambana kutafuta nafasi katika kikosi cha kwanza.
“Mapinduzi Cup itawajenga wachezaji wetu. Kila mchezaji anataka kuonekana mbele ya kocha, ushindani umeongezeka zaidi, bila shaka baada ya kumalizika kwa michuano hii muhimu, Kocha Omog atakuwa amepata kikosi chake”.
“Kikosi kipo safi, wachezaji wanaonesha juhudi kubwa. Cha msingi wote wanaelewa nini cha kufanya, dira ya Azam fc ipo wazi kabisa kuwa inataka kupata mafanikio makubwa zaidi anga za kitaifa na kimataifa”. Alisema Jafar.
Mashaindano ya mapinduzi yatakuwa ya kwanza kwa kocha Omog, achilia mbali ile mechi ya kirafiki iliyocheza Alhamisi ya kujaribu mfumo wa Tiketi za electroniki ndani ya uwanja wa Chamazi dhidi ya Ruvu shooting.
Katika mchezo huo, Omog aliiongoza Azam fc kupata ushindi wake wa kwanza wa mabao 3-0 , ambapo mshambuliaji mpya kutoka Ivory Coast, Mouhamed Kone alifunga bao mojawapo, huku mengine yakifungwa na Jonh Raphael Bocco `Adebayor` na Kipre Herman Tchetche kwa mkwaju wa penati.
Kombe la Mapinduzi mwaka huu litajumuisha timu 12 kutoka ndani na nje ya nchi ambazo zimegawanywa katika makundi matatu yenye timu nne.
Kundi A: kuna timu za Pemba Combine, Chuoni, URA kutoka Uganda na Mbeya City, huku kundi B likiwa na klabu za Simba, KMKM, AFC Leopard ya Kenya pamoja na KCC kutoka Uganda.
Wana Lambalamba, Azam fc ambao ndio mabingwa watetezi wapo kundi C na timu za Tusker fc ambao ni makamu bingwa, Dar Young Africans na Unguja Combine.
Pazia la michuano hiyo litafunguliwa rasmi januari mosi ambao mechi ya kwanza itakuwa saa 10:00 jioni baina ya KMKM dhidi ya KCC, kwenye uwanja wa Amaan, mjini Unguja.
Mechi ya ufunguzi itapigwa saa 2:00 usiku ambapo wekundu wa Msimbazi, Simba Sc watakuwa na kibarua kizito dhidi ya AFC Leopard kutoka nchini Kenya na mgeni rasmi atakuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Italia, Cesare Prandelli.
Shughuli itaendelea januari 2 ambapo katika uwanja wa Amaan, Azam fc watashuka dimbani saa 10:00 jioni kukipiga na Unguja Combine, na usiku saa 2:00, Dar Young Africans watakuwa kibaruani dhidi ya Tusker fc.
Katika uwanja wa Gombani Pemba, URA watakabiliana na Chuoni (kundi C) majira ya saa 8:00 mchana, huku Mbeya City ikishuka dimbani dhidi ya Pemba Combine, saa 10:00 jioni katika mchezo wa kundi A.
Fainali ya michuano hii itapigwa siku ya sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, januari 12 na mechi ya fainali itapigwa saa 2:00 usiku katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.
No comments:
Post a Comment