Kikosi cha Afrika Kusini kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Tanzania (Tanzanite) kinatua nchini Alhamisi (Desemba 5 mwaka huu).
Afrika Kusini ambayo itafikia hoteli ya Sapphire itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) itatua saa 8 kamili mchana kwa ndege ya South Africa Airways.
Mechi hiyo itachezeshwa na refa Nabikko Ssemambo kutoka Uganda wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Gebreyohanis Trhas kutoka Ethiopia. Waamuzi wengine ambao pia wanatoka Uganda ni Nakitto Nkumbi na Irene Namubiru.
Kamishna wa mechi hiyo ni John Muinjo kutoka Namibia. Muinjo pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Namibia (NFA) na mjumbe wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Viingilio katika mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi (Desemba 7 mwaka huu) kuanzia saa 10 kamili jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 1,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na orange, sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A watalipa sh. 10,000.
Tanzanite chini ya Kocha Rogasian Kaijage inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume na ule wa Taifa kujiandaa kwa mechi hiyo. Kambi ya Tanzanite hivi sasa imehamia Msimbazi Hotel kutoka Ruvu mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment