STRAIKA
wa Simba, Amisi Tambwe leo amefunga bao lake la kumi katika Ligi Kuu ya Bara,
lakini mkongwe Saidi Maulid ‘SMG’ amedhihirisha kwamba bado ni moto wa kuotea
mbali huku kipa Amani Simba akilimwa ‘red card’ iliyowaacha wengi midomo wazi.
Simba
ilikuwa ikicheza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Ashanti na
kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 lakini mchezaji wake Tambwe raia wa Burundi
amefikisha idadi ya mabao 10 na kuongoza katika orodha ya wafungaji wa ligi
hiyo.
Kabla
ya mchezo huo, Tambwe alikuwa ameshafunga mabao tisa akifuatiwa na Hamisi Kiiza
wa Yanga mwenye mabao manane. Wengine wanaofuatia ni Elius Maguri wa Ruvu
Shooting, Juma Liuzio wa Mtibwa Sugar na Kipre Tchetche wa Azam wenye mabao
saba kila mmoja.
Tambwe
alifunga bao lake dakika ya 46 akiunganisha pasi safi ya Ramadhan Singano
‘Messi’ ambaye aliwanyanyasa mabeki wa Ashanti upande wa kushoto kisha kutoa
pasi safi kwa mfungaji aliyefunga kirahisi.
Akizungumza
na mtandao huu mara baada ya mchezo huo, Tambwe alisema anashukuru kufunga
mabao 10 hadi sasa na anawashukuru wachezaji wenzake ndani ya Simba na benchi
la ufundi kwa ushirikiano waliompa hadi akafiksiha idadi hiyo ya mabao.
“Kazi
yangu siku zote ni kufunga, nadhani kama mchezaji natumia vyema nafasi
ninazopata kuweza kufunga na kufanya mambo kuwa mazuri kwa watu wote. Nafanya
haya (kufunga) kwa faida ya Simba na watu wote wanaoipenda klabu hii,” anasema
Tambwe.
Picha na Rahel Pallangyo.
SMG HATARI…
Winga
Said Maulid ‘SMG’ wa Ashanti United leo amedhihirisha kwamba bado yupo katika
kiwango chake baada ya kucheza vyema nafasi hiyo dhidi ya Simba na kufanya
vizuri.
SMG
aliweza kucheza vyema mbele ya beki Issa Rashid maarufu kama Baba Ubaya na
kuonyesha bado yumo kiasi ambacho alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na
mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo.
“Nadhani
nalinda kiwango changu kwa kufanya mazoezi mara kwa mara tofauti na wachezaji
wengine ambao wakiona umri umeenda anajibweteka na kuachana na soka,mimi sipo
hivyo ndiyo maana leo umeniona nacheza vile,” anasema SMG aliyewahi kuzichezea
Simba na Yanga kwa nyakati tofauti miaka ya mwanzoni ya 2000.
Katika
mchezo huo, SMG aliifungia Ashanti bao la pili dakika ya 52 akiunganisha vyema
krosi kutoka wingi ya kulia na kuamsha shamra shamra miongoni mwa mashabiki wa
Ashanti licha ya timu yao kuwa nyuma kwa mabao 3-2 kabla ya Betram Mombeki
hajaifungia Simba bao la nne.
AMANI SIMBA APIGWA RED CARD…
Kipa
wa zamani wa Simba, Amani Simba ambaye leo aliichezea Ashanti United,
alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 89 baada ya kuudaka mpira akiwa nje ya eneo
lake analoruhusiwa.
Mwamuzi
Andrew Shamba wa Pwani alimwonyesha Amani kadi hiyo baada ya kuudaka mpira
uliopigwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ wa Simba baada ya Simba kucheza
shambulizi la ghafla huku mabeki wa Ashanti wakiwa wamepandisha timu.
Messi
aliiwahi pasi ya kutoka kwa mabeki wa timu yake na kumiliki mpira kisha akawa
anamfuata Amani langoni kwake, lakini kwa kutambua hatari inayomfuata kipa huyo
akaliacha lango lake na kumfuata Messi ambaye aliunyanyua mpira lakini ghafla
Amani akanyoosha mikono yake na kujikuta ameudaka.
Baada
ya kuudaka mpira huo, Amani aliduwaa kwa sekunde kama mbili hivi kisha
akauachia na moja kwa moja akaanza kuvua grovu zake huku akijua lazima
ataonyeshwa kadi nyekundu kutokana kitendo chake hicho.
Mara
baada ya mchezo huo, Amani aliuambia mtandao huu kwamba, hakudhamili kuudaka
mpira ule lakini pia hakujua kama Messi angepiga juu kidogo na yeye kumfikia
mikononi.
“Mimi
nilijua atapiga chini halafu nilale ili nimzuie sasa wakati najipanga kufanya
hivyo yeye akapiga na mpira ukaja mikononi mwangu, sikuwa na jinsi n ndipo
nikaudaka na moja kwa moja nikavua glovu kwani nilijua lazima nionyeshwe kadi
nyekundu,” anasema Amani.
No comments:
Post a Comment