Search This Blog

Tuesday, November 12, 2013

KUMBUKUMBU YA MIAKA 19 YA KIFO NA SHEREHE YA KUZALIWA UPYA KWA METHOD MOGELLA 'FUNDI'......

Leo Tanzania inakumbuka kumbukumbu ya miaka 19 ya kifo cha mmoja wa mashujaa wake katika soka, huyu si mwingine bali ni Method Mogella ‘Fundi’ ambaye alifariki Dunia Novemba 12, 1994.
Lakini pia siku hiyo hiyo ya kifo chake Method Mogella alizaliwa upya....Fuatilia tamthilia hii ya kusisimua

Method anakumbukwa zaidi kwa kuwa mmoja wa wanasoka waliocheza soka la mafanikio kwa ngazi ya klabu kiasi cha kuonekana mfano wa kuigwa akimudu vyema kucheza nafasi ya kiungo mchezeshaji.
Hadi leo Tanzania ingali haijapata kiungo aliyefanana naye japokuwa wapo vijana wengi wanaojaribu kufuata nyayo zake ambao sasa tunadhani wanaweza kufikia makali ya Method.
Katika kikosi cha Yanga kilichoifunga SC Villa ya Uganda mabao 2-1 na kutwaa ubingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame), Method alikuwepo kikosini na alitoa mchango mkubwa wa ushindi huo.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Edibily Lunyamila na Said Mwamba ‘Kizota’, na hayo ni miongoni mwa mafanikio ya Method alipokuwa akiitumikia Yanga.

BABA YAKE ALIMKATAZA KUCHEZA SOKA

Method aliyezaliwa mwaka 1965 mkoani Morogoro, alionyesha ana mapenzi makubwa na mchezo wa soka tangu alipokuwa anasoma katika shule ya msingi ya Msimbazi Boys wilayani Ilala jijini Dar es Salaam wakati familia yake ilipokuwa inakaa Buguruni. 

Katika miaka ya mwanzoni mwa 1980, nyota ya Method iliendelea kung’ara alipokuwa akisoma katika sekondari ya ufundi ya Mtwara akicheza nafasi ya kiungo na hata katika timu ya mtaani kwake Buguruni iliyofahamika kama Jay Ambe, alikuwa mwiba mkali kwa timu pinzani walizokutana nazo.Lakini wakati Method akielekea kupata mafanikio haya katika soka, baba yake anayefahamika kwa jina la Martin Kunambi alikuwa hataki mwanaye ajiusishe na soka badala ya masomo hivyo alimpiga marufuku kucheza soka. 

Hata hivyo juhudi za wanafamilia wengine akiwemo dada yake mkubwa aitwaye Angelina, zilisaidia kugeuza mtazamo wa baba yake kuhusu mwanaye kucheza soka.Wakati Method akielekea kumaliza elimu ya sekondari baba yake alimruhusu kucheza soka kwa sharti la kujitengea muda wa masomo na michezo.


                   Method Mogella alivyokuwa utotoni mwake....


MEJA JENERALI MAKAME RASHID AMPELEKA SIMBA

Muda mfupi baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Method alijiunga na Chuo cha Ufundi Arusha ambako aliendelea kucheza soka kiasi cha kuitwa na timu za mitaani kama Namanga ili aweze kuzisaidia katika michuano mbalimbali.

Kutokana na kushiriki katika klabu mbalimbali za mtaani, Method aliweza kujulikana karibu katika eneo kubwa la Arusha kutokana na umahili wake katika kucheza soka.
Alipomaliza chuo na kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kama ilivyokuwa wakati huo kabla ya kurejeshwa kwa utaratibu huo hivi sasa, Method alijiunga na JKT kwa mujibu wa sheria ambako aliendelea kucheza soka akiwa huko pia.
Akiwa katika kambi ya JKT, Meja Jenerali Makame Rashid alimuona Method akicheza soka na kuvutiwa naye ambapo haraka aliamua kumpeleka Dar es Salaam kujiunga na klabu ya Simba mwaka 1989.

Method aliichezea Simba kwa mafanikio makubwa kwani mwaka 1991 aliisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuifunga SC Villa kwa mabao 3-0 katika michuano iliyochezwa nchini.


AJIUNGA NA YANGA, ALAZIMISHA MDOGO WAKE ASAJILIWE.
Baada ya kuichezea Simba kwa mafanikio kwa miaka mitatu, mwaka 1992, Method alijiunga na Yanga kwa ushawishi mkubwa wa aliyekuwa mfadhili wa timu hiyo marehemu Abbas Gulamali ambaye alimsajili kwa mbwembwe.
Usajili huo unaelezwa ulifanywa kwa majigambo baada ya Gulamali kuwa katika ushindani na aliyekuwa mfadhili wa Simba wakati huo, Azim Dewji. Watu wengi wa familia ya Method walikuwa na mapenzi makubwa kwa klabu ya Yanga hivyo usajili wake ulibarikiwa na kila mtu.

Baada ya kufanya vizuri akiwa na Yanga katika msimu wa 1992, msimu uliofuata ilibidi Method aongeze muda wa mkataba wake. Hapo Method alitoa sharti moja ili asajiliwe ambapo alimueleza wazi Gulamali kwamba, ili yeye asaini Yanga ni lazima klabu hiyo imsajili pia mdogo wake aitwaye Philothei.
Kweli Gulamali alikubali ombi hilo na moja kwa moja Philothei aliichezea Yanga kwa mafanikio makubwa ndani ya msimu huo sambamba na Mwanamtwa Kihwelo ambaye naye usajili wake ulifanyika sambamba na ule wa mdogo wa Method.
Philothei hakuweza kufikia umaarufu wa kaka yake licha ya kuwa alikuwa akicheza kiungo namba sita na namba nane.


WAKATWAA UBINGWA NA MDOGO WAKE, WAPELEKA NYUMBANI TV MBILI KWA MARA YA KWANZA
Akiwa na mdogo wake katika kikosi cha Yanga, Method alikuwa mmoja wa wachezaji wa kikosi cha timu hiyo kilichoshiriki kwa mafanikio michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1993.

Philothei hakuwa akipata nafasi mara kwa mara katika kikosi cha Yanga lakini Method alikuwa ‘injini’ ya timu wakati huo na alichangia kwa kiasi kikubwa Yanga kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwenye Uwanja wa Nakivubo huko Kampala Uganda.
Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, huku mabao yake yakifungwa na Kizota na Lunyamila. Muda mfupi baada ya kutwaa ubingwa huo, uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na mfadhili Gulamali uliamua kutoa zawadi ya seti ya televisheni na deki kwa kila mchezaji kama shukrani kwao kwa kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa huo.

Hivyo waliporejea nchini kutoka Uganda wawili hao walizipeleka televisheni hizo nyumbani kwao Buguruni, hiyvo kuwa nyumba pekee yenye seti mbili za televisheni ambazo wakati huo zilikuwa adimu mitaani.
Hapo ndipo baba mzazi wa Method na Philothei alipoona faida ya soka kwa wanawe na tangu hapo alikuwa akiwasisitiza kupenda kufanya mazoezi binafsi pindi wanapokuwa nje ya Yanga.



KICHWA CHAMUNDOA DUNIANI
Wakati akiwa bado mchezaji wa Yanga, Method alipatwa na maradhi ya kichwa Novemba 1994 wakati akiishi peke yake Mwenge jijini Dar es Salaam. Kutokana na kuumwa mara kwa mara ugonjwa huo, baba yake aliamuru aende kwao Buguruni ili akapate uangalizi wa karibu.
Hiyo ilikuwa Novemba 11, 1993, ambako jioni alipelekwa Buguruni na alipofika huko alilala usiku mmoja tu kwani kesho yake asubuhi aliamka salama huku akiendelea kuuguza maumivu ya kichwa.

Kesho yake Novemba 12, 1993 alipoamka asubuhi wakati anajuliwa hali na mama yake, Method aliomba apikiwe viazi kama kifungua kinywa chake. Muda mfupi baadaye mama yake alitoka chumbani alimokuwa Method na kuhangaikia kupika viazi.
Mama wa Method aliporejea chumbani kwa mwanaye alimkuta amelala huko povu likimtoka mdomoni, haraka aliwaita watu waliokuwamo nyumbani hapo na kuwapeleka chumbani kumpa huduma ya kwanza Method.
Baada ya kuona hali si nzuri familia ilimtuma Philothei kufuata gari ili kumuwaisha hospitali Method na walipofika katika hospitali ya Amana Ilala, daktari waliyemkuta zamu aliwaambia; “HUYU AMESHAFARIKI TAYARI.”
Kiichofuatia baada ya hapo ni familia kuanza kuhangaikia mazishi ya Method na ilibidi kila ndugu wa karibu apigiwe simu ili aweze kushiriki taratibu hizo.


 Dada yake Method Mogella Angelina akiwa na kijana wake Method Aniceth ambaye leo anatimiza miaka 19 ya kuzaliwa kwake,aliyemzaa siku ya kifo cha mdogo wake.

DADA YAKE AJIFUNGUA MTOTO BAADA YA KIFO CHA METHOD, AMPA JINA METHOD.

Muda mfupi baada ya Method kufariki, dada yake aitwaye Angelina ambaye alikuwa na ujauzito alipatwa na uchungu na kujifungua salama mtoto wa kiume aliyekuwa na afya njema.
Angelina alijifungua mtoto huyo baada ya kupata mshtuko wa kifo cha mdogo wake ambaye walikuwa wameshibana vya kutosha hivyo taarifa za kifo chake zilimshtua kiasi cha kupoteza fahamu.
Wakati ndugu wengine wakishughulika na taratibu za mazishi ya Method, wengine walichukua jukumu la kumpeleka Angelina hospitali ambako alipofikishwa tu alijifungua mtoto wa kiume.

MTOTO APEWA JINA LA METHOD, AHAIDI KUFUATA NYAYO ZA MJOMBA
Saa chache baada ya kujifungua salama mtoto wa kiume, Angelina aliamua kumpa jina la Method mtoto huyo ambaye pia anatumia jina lingine la Aniceth.
Mama wa mtoto huyo anasema, amefanya hivyo kwa kumbukumbu ya marehemu mdogo wake ambaye walikuwa wameshibana sana. “Sikuwa na jinsi kwani niliamua tu kumpa mwanangu jina hilo kwani nilifahamu kwamba jina hilo litanifanya nimkumbuke ndugu yangu mara kwa mara,” anasema Angelina.

NAAM, USIKOSE KUSOMA SEHEMU YA PILI YA MAKALA HII KUJUA JINSI METHOD MTOTO ANAVYOCHEZA SOKA KWA SASA NINI MATARAJIO YAKE…..PIA MARAFIKI WA ZAMANI WA METHOD WATAMZUNGUMZIA.

2 comments:

  1. nafikiri picha ya method akiwa mtoto sio ya kwake tunaomba utafiti ufanyike kwa umakini kabla ya kufanya posting kwenye social media

    ReplyDelete
  2. daaah ni story ya kusikitisha sana nimeisikia sportsextra moja kwa moja nikajua itakuwepo humu!!!!!!!!!!!!! mungu aileza roho yake pema pepon ameen

    ReplyDelete