WAKATI inaanza Ligi Kuu
ya Bara, Ashanti United ya Ilala jijini Dar es Salaam ilianza vibaya baada ya kupata
matokeo yasiyo ya kuridhisha hivyo kujikuta ikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi
hiyo kwa muda mrefu kidogo, lakini nyuma ya pazia kuna vitu vilikuwa
vimejificha.
Kwa mujibu wa mmoja wa
wachezaji waandamizi wa klabu hiyo, kitu kikubwa kilichoifanya Ashanti isifanye
vizuri ni uwapo wa
WACHEZAJI WENGI WASIO
NA UZOEFU wa kucheza ligi kuu.
Tangu ilipopanda msimu
huu, Ashanti haikuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu wa maana kuweza kuhimili mikiki
mikiki ya ligi hiyo ambayo ina timu zenye wachezaji wa hali ya juu.
“Hatukuwa na wachezaji
wenye uzoefu wa maana kuweza kupambana na wachezaji wa kulipwa kama Haruna
Niyonzima au Didier Kavumbagu wa Yanga, pia hata Kipre Tchetche wa Azam, hivyo
tulikuwa tunacheza na watu ambao unawajibika kuwaelekeza kila mara kuhusu nini
cha kufanya.
“Hali hii ilitufanya kutofanya
vizuri katika mechi za mwanzoni lakini sasa naona tumetulia na mambo yanaenda
vizuri,” kinasema chanzo chetu.
WACHEZAJI HAWAKUWA WAKIMWELEWA KOCHA
Inadaiwa wachezaji
wengi wa Ashanti hawakuwa wakimwelewa kocha aliyeondoka Hassan Banyai kiasi cha
kushindwa kucheza ipasavyo katika kila mchezo waliokuwa wanacheza.
“Tulikuwa tunacheza
kila mechi kutokana na maelekezo ya mwalimu na kila mchezo ulikuwa na maelekezo
yake, sasa utakuta mchezaji anaelekezwa hivi halafu anapoingia uwanjani anacheza
vile, hili lilikuwa tatizo kwetu.
“Lakini sasa hali imetulia
kwani wachezaji wenyewe wametulia baada ya kukutana wenyewe kwenye kikao chao
na kuwekana sawa kuhusu mwenendo wa timu na mustakabali wake katika ligi.
“Siwezi kuzungumza sana
kuhusu POSHO kwani kuna wakati
wachezaji wanaweza kuona timu imeingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na
mapato ya milangoni lakini wao wanaambulia kiasi kidogo hapo lazima kutakuwa na
maneno, lakini sasa kila mchezaji anajua namna viongozi wanavyotumia fedha
nyingi katika kuiendesha timu na kuna wakati fedha inaingia lakini inalipwa
madeni.
“Ukitazama vizuri
utaona kuna mechi mbili tu ambazo tunaweza kuingiza kiasi kikubwa cha fedha,
hizo ni dhidi ya Simba na Yanga pekee lakini mechi zote zilizobaki hakuna fedha
ya maana inayopatikana, sasa wachezaji wanaelewa kuhusu hali hiyo na mambo
yanaenda vizuri,” kinasema chanzo chetu.
Wakati Simba ikishika nafasi ya nne ikiwa na
pointi 21 baada ya mechi 12, Ashanti yenyewe ina pointi 10 ikiwa katika nafasi
ya 11 baada ya kucheza mechi 12 pia.
Ashanti ni miongoni mwa
timu tatu zilizopanda msimu huu wa Ligi Kuu huku nyingine zikiwa ni Mbeya City
na Rhino Rangers ya Tabora.
No comments:
Post a Comment