Na
Happiness Shayo-Utumishi
Baada ya kutamba kwa muda
mrefu kwamba haiwezi kufungwa katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya
Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), timu ya netiboli ya Ofisi ya Waziri Mkuu
TAMISEMI imepewa kipigo takatifu na timu ya netiboli ya Ofisi ya
Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kufungwa mabao 38-28 katika mechi ya
robo fainali iliyofanyika leo katika viwanja vya Jamhuri mjini Dodoma.
Mchezo huo ulioanza kwa
kasi ya aina yake huku timu zote zikiwa zimekamia kutwaa ushindi, ulianza
kumilikiwa na timu ya TAMISEMI katika dakika 15 za mwanzo ambapo ilifanikiwa kufunga
mabao 9 kupitia mfungaji wake Jema Mdemu (GS) huku Utumishi ikifunga mabao 6 kwa
kutumia mfungaji wake Anna Msulwa (GA).
Kipindi cha pili cha mchezo,
TAMISEMI iliongeza mashambulizi kwenye goli la Utumishi na kufunga mabao 9 huku
Utumishi ikifunga mabao 10 na kuifanya timu ya TAMISEMI kuongoza kwa mabao 18
huku Utumishi ikiwa na mabao 16.
Hata hivyo mchezo
ulibadilika ghafla katika kipindi cha tatu baada ya Utumishi kufunga mabao 6
huku TAMISEMI ikifunga mabao 3 na kuifanya Utumishi kuongoza kwa bao 1.
Timu ya Utumishi iliongeza
kasi katika dakika za lala salama za mchezo huo na kuifunga TAMISEMI mabao 16-7
na kuifanya timu hiyo kujinyakulia ushindi katika mpambano huo.
Mashindano ya SHIMIWI yapo
katika hatua ya robo fainali ambapo Timu ya netiboli ya Utumishi imevuka robo
fainali na inatarajiwa kupambana na timu ya Wizara ya Ujenzi katika mechi ya
nusu fainali kesho katika viwanja vya Jamhuri mjini Dodoma.
Timu ya mpira wa Pete ya Ofisi ya Rais, Menejmenti ya Utumishi wa Umma "Kombani queens" ikifanya mazoezi mepesi kabla ya kuingia uwanjani kupambana na TAMISEMI katika mashindano ya SHIMIWI Kiwanja cha Jamhuri mjini Dodoma.
Timu ya mpira wa Pete ya TAMISEMI ikifanya mazoezi kabla ya kupambana wenzao wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma "Kombani Queens" .
Timu ya mpira wa Pete ya TAMISEMI ikisalimiana na timu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma "Kombani Queens" kuashiria mwanzo wa mpambano wao wa Mpira wa Pete kuwania kuingia nusu Fainali za SHIMIWI.
Mchezaji wa timu ya mpira wa Pete ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma "Kombani queens" Monica Aloyce (GK) (aliyeruka juu) akiondoa hatari kutoka kwa wachezaji wa timu ya TAMISEMI wakati wa mpambano dhidi ya timu hizo.
Mchezaji wa timu ya mpira wa Pete ya TAMISEMI Defroza Otilia (GA) akijaribu kutoa pasi wakati wa mpambano na Utumishi mjini Dodoma, mbele yake akikabwa na mchezaji wa Utumishi Monica Aloyce (GK) .
Mchezaji wa timu ya mpira wa Pete ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma "Kombani queens" Elizabeth Fussi (C) akitoa pasi wakati wa mpambano dhidi ya TAMISEMI katika mashindano ya SHIMIWI mjini Dodoma. Mbele yake ni mchezaji wa TAMISEMI Imelda Hango (C) akijaribu kumzuia .
Fatma Ahmed (GS) wa timu ya mpira wa Pete ya ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma akichukua pasi kutoka kwa Anna Msulwa (GA) (aliye mbele yake) katika mashindano ya SHIMIWI mjini Dodoma. Utumishi iliifunga TAMISEMI mabao 38-28.
No comments:
Post a Comment