Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewahakikishia
Watanzania kuwa uchaguzi wa kupata Kamati mpya ya Utendaji ya shirikisho
utafanyika Oktoba 27 mwaka huu kama ilivyopangwa.
“Wazungu
wanasema ije mvua au jua, uchaguzi utafanyika. Isipokuwa tunachotaka
kuhakikisha ni kuwa unakuwa uchaguzi huru na wa haki,” amesema Rais Tenga
wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana
(Oktoba 7 mwaka huu).
Amesema
mchakato unakwenda vizuri kilichobaki ni revision (mapitio) na rufani, masuala
ambayo yako mbele ya Kamati ya Rufani ya Maadili na Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi.
Rais
Tenga amesema lengo la hatua hizo si kuzuia watu wasigombee kwani ni lazima
mambo ya msingi ikiwemo sifa za wagombea yaangaliwe, lakini kwenye haki ni
lazima kuhakikisha inatendeka hata kama ni kwa mtu mmoja.
Mchakato
wa uchaguzi ulivutia waombaji 58 ambapo watatu wamekata rufani Kamati ya Rufani
ya Uchaguzi kupinga kuondolewa na Kamati ya Uchaguzi wakati wengine wanane
masuala yao yamepelekwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa njia ya mapitio
(revision) ili kupata mwongozo wa utekelezaji.
Mwongozo
huo umeombwa na Sekretarieti ya TFF kwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa vile
Kamati ya Maadili iliwaona waombaji wanane wa uongozi waliofikishwa mbele yake
kwa makosa ya kimaadili kutokuwa na hatia, lakini wakati huo huo ikitambua
kuondolewa kwao kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kulikofanywa na Kamati ya
Uchaguzi.
MRADI WA
FOOTBALL FOR HOPE KUFUNGULIWA OKTOBA 13
Mradi
wa Football for Hope kusaidia watoto na wasiojiweza kupitia mpira wa miguu
uliofadhiliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) mkoani Iringa
utafunguliwa rasmi Oktoba 13 mwaka huu.
FIFA
hutoa mradi huo kwa baadhi ya nchi kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo
utawala bora, lakini kwa kupitia taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) ambapo kwa
Tanzania umepatikana kupitia taasisi ya Iringa Development of Youth, Disabled
and Child Care (IDYDCC).
Rais
wa TFF, Leodegar Tenga ameishukuru FIFA kwa msaada huo, kwani ni mkubwa na kuongeza
kuwa ni matumaini yake utatumika kwa lengo lililopangwa.
Amesema
mradi huo wa FIFA ambao ni wa kusaidia watoto kielimu na wasiojiweza kwa
kupitia mpira wa miguu haukupita moja kwa moja TFF ni mzuri kwani moja ya mambo
uliofanikisha ni kuwepo jengo na sehemu ya watoto kucheza.
Ni
wastani wa nchi kumi tu duniani kwa mwaka zinapata mradi huo kutoka FIFA, jambo
ambalo Rais Tenga amesema linachangiwa pia na uhusiano na ushirikiano uliopo
kati ya Tanzania na shirikisho hilo.
KAMATI YA
WANAWAKE, TWFA YAPONGEZWA
Kamati
ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na
Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) wamepongezwa kwa
kuhakikisha akina mama wanacheza mashindano mbalimbali.
Pongezi
hizo zimetolewa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambapo amesema timu za wanawake
zimekuwa zikishiriki katika mashindano mbalimbali licha ya ukweli kuwa hadi
sasa hakuna udhamini kwenye mchezo huo.
Amesema
mpira wa miguu unaendeshwa na udhamini na kuchangia, jambo ambalo
linafanikishwa kwa kiasi kikubwa na uwazi katika matumizi ya fedha, jambo ambalo
hivi sasa lipo ndani ya TFF.
Rais
Tenga amesema baada ya kuanzisha Kamati ya Ligi, hivi sasa TFF inapata asilimia
4.5 tu ya mapato ya mechi za ligi kutoka asilimia 33 iliyokuwa ikipata wakati
anaingia madarakani mwaka 2004.
Amesema
asilimia hiyo 4.5 haiwezi kuendesha mpira na ndiyo maana nguvu zinaelekezwa
katika kutafuta wadhamini na kuchangia. Pia TFF inatoa zaidi ya asilimia 15 ya
Fedha za Msaada wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FAP) kutoka FIFA kwenye mpira
wa miguu wa wanawake ambapo ni nchi chache zinazofikia kiwango hicho.
Hivyo,
ametoa mwito kwa kampuni kujitokeza kudhamini au kuchangia timu za Taifa za
mpira wa miguu za wanawake ambazo zinashiriki mashindano mbalimbali mwaka huu,
kwani gharama za kuziendesha ni kubwa.
Timu
ya wakubwa (Twiga Stars) inacheza mashindano ya mchujo ya Fainali za Afrika
(AWC) zitakazofanyika mwakani nchini Namibia wakati ile ya chini ya miaka 20
inacheza mashindano ya Dunia ambayo fainali pia zitachezwa mwakani nchini
Canada.
MECHI YA
YANGA, MTIBWA YAINGIZA MIL 97/-
Mechi
ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) iliyochezwa jana (Oktoba 6 mwaka huu) Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam kati ya Yanga na Mtibwa Sugar imeingiza sh. 97,557,000.
Watazamaji
waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 46 lililochezeshwa na Isihaka
Shirikisho kutoka Tanga walikuwa 17,313. Yanga ilishinda mabao 2-0.
Viingilio
katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku
kila klabu ikipata mgawo wa sh. 23,453,748.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) iliyolipwa ni sh. 14,881,576.27.
Mgawo
mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 11,925,635.06, gharama ya
kuchapa tiketi ni sh. 3,171,190 wakati gharama za mchezo ni sh. 7,155,381.04.
Kamati
ya Ligi sh. 7,155,381.04, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,577,690.52
na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,782,648.18.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment