Search This Blog

Wednesday, October 2, 2013

KIKOSI CHA WATEULE 11 BORA LIGI KUU BARA


Na Baraka Mbolembole

Ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara imefikia raundi ya sita na timu ya soka ya Simba ikiwa inaongoza ligi hiyo, ikifuatiwa kwa karibu na timu za Azam FC, Kagera Sugar, Coastal Union na mabingwa watetezi, timu ya Yanga.

Leo, nimejaribu kupanga kikosi cha wachezaji 11 bora ambao wamefanya vizuri zaidi katika michezo sita iliyopita ambayo kila timu imeshacheza. Upangaji wa kikosi hiki umezingatia uwezo wa mchezaji husika katika nafasi yake, namna alivyoweza kuisaidia timu yake, nidhamu kujituma na kuwa tayari kuookea majukumu anayokuwa akipewa na walimu wake.

SHAABAN KADO- KIPA
Ningeweza kumpanga golikipa wa timu ya Mbeya City, David Baruani lakini nilihitaji kipa imara zaidi ambaye anaweza kuisaidia timu kupata walau pointi moja hata kama haina uwezo wa kufunga mabao ya kutosha. Kwa, Kado sikuwa na shaka kwamba ni kipa aliyeifanya timu yake kuwa mahali ilipo sasa, Coastal hawajafunga mabao ya kutosha ila mikono mizuri ya Kado imeweza kuifanya timu hiyo kuwa ngumu kufungika. Alifanya vizuri kwa kila dakika aliyokuwepo katika kikosi cha kwanza. Ameboresha kiwango chake katika kutema mipira na uchezaji wa krosi.

WAkati kipa aliyeshinda tuzo ya kipa bora msimu uliopita, Ally Mustapha ' Barthez' akiwa ameshafungwa mabao saba katika michezo sita iliyopita, Kado amekuwa bora zaidi ya kipa huyo wa Yanga hadi sasa. Kiongozi mzuri wa safu nzima ya ulinzi ya Coastal, anaweza kurejea tena timu ya Taifa kama ataendeleza uchezaji wake usio na mfanowe.

'' Ushindani wa msimu huu ni wa kiwango cha juu katika ligi kuu, nashukuru kupewa nafasi hiyo" anasema Kado nilipofanya naye mawasiliano.

MABEKI

Nitampanga, William Lucian katika upande wa ulinzi wa kulia na kumpanga Abdi Banda upande wa kushoto. Katika safu ya kati, nitawapanga, Juma Nyosso na Joseph Owino. Kwa nini ninahitaji safu hii ya ulinzi?

Utayari wa kupokea majukumu mapya na kuyatekeleza kutoka kwa kiungo, Lucian wa klabu ya Simba ni kitu kilichonifanya nimpe kipaumbele cha kwanza, japo walinzi kama Erasto Nyoni wa Azam FC, Mbuyu Twite wa Yanga wameonekana kufanya vizuri katika siku za karibuni. Lucian alianza kucheza upande wa kulia baada ya kutokea majeraha kwa nohodha Nassorro Chollo na Haruna Shamte kukutwa na majeraha.

Lucian amecheza mechi tano kati ya sita za timu yake huku timu ikiwa imerehusu mabao manne tu, na kufunga mabao 15 na mengi yakitokea upande wa kulia anaweza kufanya vizuri zaidi endapo kutakuwa na ' balansi sawa' ya kupokezana majukumu ya kushambulia na mlinzi chipukizi wa kushoto, Banda. Akiwa amecheza michezo mitano ya timu yake Babda amenipa shauku ya kumjumuhisha katika kikosi hiki kutokana na bao lake la mkwaju wa mbali katika mchezo dhidi ya JKT Oljoro.

Wakati vijana hao wakipokezana majukumu yao pembeni ya uwanja, nitapenda kuona uwezo wa walinzi wa kati, Owino na Nyosso ambao misimu mitatu iliyopita walikuwa sehemu muhimu ya kikosi kisichoshindika cha Simba kilichotwaa taji bila kufungwa mchezo wowote. Baada ya kupona majeraha yake Owino ameweza kutuliza tatizo la safu ya ulinzi la Simba, huku Nyosso akionesha kiwango cha juu katika mchezo wake, nidhamu ya kiwango cha juu huku akiwa kiongozi wa pili katika safu ya ulinzi ya Coastal. KWa pamoja na Owino, Lucian na Banda walinzi hawa wanne wanaweza kumfanya Kado kuwa imara zaidi.

VIUNGO

" Timu zinapambana ndiyo maana kumekuwa na matokeo chanya, kama hali hii itaendelea na waamuzi kuchezesha bila kufuata maelekezo, basi kutakuwa na mabadiliko makubwa katika nafasi tano za juu mwishoni mwa msimu" anasema kiungo na nahodha wa timu ya Mtibwa Sugar, Shaaban Nditti.

Katika mfumo wa 4-4-2 ambao ni rahisi zaidi kwa wachezaji wa Kitanzania nitawapanga viungo hawa wanne. Nditti, kama kiungo wa ulinzi- namba sita, Saimon Msuva katika wingi ya kulia, Steven Mazanda- kiungo mshambuliaji, na Haruna Niyonzima katika nafasi ya kiungo wa kushoto.

Nditti, atakuwa na jukumu la kuchukua mipira na kuitawanya upande wake wa kulia na Mazanda akifanya hivyo upande wa kushoto. Hii ni kwa kuwa kuna walinzi wazuri katika nafasi za pembeni- Lucian na Banda- ambao wana uwezo mzuri wa kupiga krosi nzuri za mwisho.

Msuva ni mchezaji mwenye spidi kali, na unaweza kumfananisha na Aaron Lenon, yule winga wa Tottenham, kasi yake inaweza kumfanya kuwa na wakati rahisi wa kumsumbua mlinzi mgumu kupitika ( rejea alivyoshindwa kumpita Banda- Yanga vs Coasta, na akajikuta akipita kadi nyekundu). Kocha wa Yanga kila mbinu zake zinapokwama amekuwa akimuachia Msuva uhuru wa kukimbia zaidi na zaidi mchezo ili wapate matokeo. Atafanya vizuri zaidi kwa kuwa atakuwa na mlinzi ' shapu', Lucian katika upande huo.

Kwa, Niyonzima atakuwa ni kama namba 11, lakini si mpigaji wa krosi bali mchezesha timu ambae anatambua mbele kuna washambuliaji ambao wakipata nafasi tu wanafunga. ' Niyo' ni kiungo asiye na mfano katika upigaji wa pasi za mwisho, ubunifu na kiwango cha hali ya juu cha umakini, ni kiongozi wa ziada katika timu na ninaamini atanipatia kile ambacho anacho siku zote, kiwango kisicho na mwisho.

WASHAMBULIAJI
Nitawachukua washambuliaji wawili raia wa Burundi ambao kwa pamoja wamefunga mabao 10 katika michezo sita iliyopita. Hamis Tambwe, na Didier Kavumbagu, washambuliaji hawa wa klabu za Simba na Yanga wanaweza kufunga kwa vichwa, wakiunganisha krosi kwa miguu kwa mtindo wa aina yake. WAna nguvu na uwezo wa kupokea mipira na kugeuka nayo, pia wanaweza kucheza kama washambuliaji pekee katika safu ya mashambulizi.

Nikiwa na Msuva na Lucian, ambao watapiga krosi zikitokea upande wa kulia nitamwambia, Tambwe ajaribu kuupiga kila mpira kwa usahihi ili tuweze kupata mabao, mabao mengi aliyofunga ameunganisha krosi ambazo zimekuwa zikipigwa na Haruna Chanongo, itakuwaje kwa krosi za Msuva? Kavumbagu anaweza kufanya hivyo pia ila ukimchunguza anafunga mabao mengi akitumia mipira inayotoka upande wa kushoto. Huku atakuwa akikutana na pasi za Haruna, au krosi za Banda atafunga zaidi na zaidi.

Mazanda ni kiungo mchezesha timu hatari sana, anafikiria na mchezaji ambaye anaweza kufanya kitu kikubwa kwa ajili ya timu yake. Mpigaji mzuri wa pasi za kupenyeza na uwepo wa Tambwe na ' Kavu' katika mashambulizi anaweza kuwa mpigaji mzuri wa pasi za mwisho, Nditti atakuwa mkabaji mzuri na huo ndiyo uzaifu wa Mazanda, si mkabaji ila ni mchezesha timu mahiri.

MAKOCHA;
Timu nyingine zinabidi zioene aibu kuongozwa na Simba ya mpito. Kocha Abdallah Kibadeni ameweza kuifanya Simba kuwa vinara wa ligi hadi sasa. Timu yake aina kasi hii inawezekana kutokana na mazoezi ya muda mrefu ambayo waliyafanya kabla ya kuanza msimu. Wakati akitambua hilo, amehakikisha timu yake ikipata ushindi wakati miili ya wachezaji wake ikianza kufunguka taratibu. Ni mfuasi mzuri wa wachezaji vijana na amekuwa akitoa nafasi kwa wale wazoefu wenye kujituma.

Kuwa na kikosi hiki ni lazima uwe na bajeti kubwa, ila endapo King angekuwa na wachezaji hawa 11 bila shaka angekuwa amekusanya pointi 18 katika michezo sita iliyopita. Atasaidiwa na Juma Mwambusi kocha ambaye ameweza kuifanya Mbeya City kutofungwa mchezo wowote kati ya sita waliyocheza hadi sasa

Wewe, msomaji wa mtandao huu una fikiri nani na nani walipaswa kuunda timu bora hadi sasa katika ligi kuu yetu.

0714 08 43 08

2 comments:

  1. big up kwa Banda katika kikosi chako, ila kwa kavumbagu kwanini sio Mombeki? na sijaelewa kwanini Gallas maana amecheza nafasi hiyo mara moja tu na sio dk90 kama sijakosea

    ReplyDelete
  2. Kuhusu makocha sina ubishi King na Mwambusi
    Goal keeper : 1. Yule Ruvu Shooting 2.Twite 3. Baba Ubaya.
    4. Baki four Ruvu Shooting 5. Owino 6. Mkude 7.Neimer 8.Noyonzima 9.H.Chanongo 10.Amis Tambwe 11. Hamis Kiiza .

    Ni hayo tu na huo ndo mtazamo wangu ila nina uwakika kila timu itakayo tia mguu goal ndogo 3.

    ReplyDelete