Mshambuliaji wa Yanga, Hamisi Kiiza amesema hana mpango wa kuwania tuzo ya
ufungaji bora yaani kiatu cha dhahabu katika Ligi Kuu ya Bara badala yake
anajipanga kuhakikisha timu yake inatetea ubingwa wa ligi hiyo.
Kiiza ambaye
hadi sasa amefunga mabao saba, ikiwa ni moja nyuma ya Amisi Tambwe wa Simba ambaye
hadi sasa ameshafunga mabao manane.
Baada ya kufunga
bao moja moja katika mechi dhidi ya Azam, JKT Ruvu na Kagera Sugar, Kiiza
alifunga mabao mawili mawili katika mechi dhidi ya Simba na Rhino Rangers.
Akizunguma na
mtandao huu jijini Dar es Salaam, Kiiza amesema licha ya kuwa na mabao saab
hadi sasa, hana mpango wa kutolea macho nafasi ya ufungaji bora kwani
anachofanya sasa ni kufunga mabao kwa ajili ya timu yake ili iweze kutwaa
ubingwa.
“Kuwa mfungaji
bora bila ya kutwaa ubingwa hakuna maana yoyote, badala yake mimi najipanga
kuhakikisha nafunga mabao muhimu yatakayoiwezesha timu yangu kutwaa ubingwa. Ufungaji
bora bila ubingwa unakuwa si lolote,” anasema Kiiza.
Kiiza raia wa
Uganda amesema anafurahia akicheza na mchezaji yeyote katika nafasi ya
ushambuliaji ndani ya Yanga kwani wote hufanya nao mazoezi na ndiyo maana
ameweza kufunga akiwa na wachezaji tofauti tofauti.
Yanga ambayo
sasa ina pointi 19 katika mechi 10 ilizocheza, Jumanne ijayo inatarajiwa
kucheza na Mgambo JKT katika muendelezo wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam. Yanga inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo yenye
timu 14.
No comments:
Post a Comment