Search This Blog

Monday, October 28, 2013

KIBADENI AKUBALI YAISHE, MALARIA YAIPONZA SIMBA


MUDA mfupi tu baada ya timu yake kufungwa mabao 2-1 na Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni, amesema, “Nakubali tumefungwa kwa haki na ni moja ya sehemu ya mchezo.”
Kibadeni amesema kiukweli mabao yote ya Azam yalitokana na makosa waliyofanya lakini amewasifu vijana wake kuweza kucheza vizuri hasa kipindi cha kwanza japokuwa wamefungwa. Hii ni mara ya kwanza Simba kufungwa katika msimu huu wa ligi ikiwa chini ya Kibadeni.
“Nakubali matokeo haya, nadhani wote mmeona jinsi mpira ulivyochezwa, wenzetu wametumia makosa yetu na kupata ushindi. Katika soka ukipata nafasi ya kufunga unatakiwa kufanya hivyo kama walivyofanya Azam, sasa tunajiandaa na mchezo ujao,” alisema Kibadeni.
Naalipoulizwa kutokuwepo kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kama mabeki Gilbert Kaze na Nassor Masoud ‘Chollo’ ambao nafasi zao zilichezwa na William Lucian ‘Gallas’ na Hassan Khatib, Kibadeni alijibu; “Wachezaji hao ni wagonjwa, Kaze anaumwa malaria kama ilivyo kwa Chollo ndiyo maana leo hamjawaona uwanjani.
“Kiasi fulani kukosekana kwao kumeifanya mechi hii kuwa ngumu kidogo maana hawa vijana bado wadogo wanaohitaji muda kuweza kumudu michezo mikubwa kama hii.”
Kibadeni pia hakumchezesha mshambuliaji Amisi Tambwe ambaye hadi sasa anaongoza kwa ufungaji katika ligi hiyo akiwa amefunga mabao nane, akifuatiwa na Hamisi Kiiza wa Yanga, Juma Liuzio wa Mtibwa na Elius Maguri wa Ruvu Shooting ambao wote wana mabao saba.
Kocah huyo alisema, hakuweza kumpanga Tambwe kutokana na kuwa majeruhi wa goti lakini anaweza kucheza mechi ijayo endapo afya yake itaimarika ndani ya saa 72 zijazo.
Ushindi huo wa Azam unaifanya timu hiyo kuishusha Simba kileleni mwa ligi hiyo na kuketi yenyewe ikiongoza kwa pointi 23 ilizopata baada ya kucheza mechi 11 kama ilivyo kwa Simba ambayo inapoteza mechi yake ya kwanza tangu kuanza kwa ligi hii msimu huu.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 20 ilizopata baada ya kucheza mechi 11, ambapo imeshinda mechi tano na kutoka sare tano. Simba imefunga mabao 21 na kufungwa mabao 10.
Katika mchezo wake ujao, Simba itacheza na Kagera Sugar Oktoba 31 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Azam ikipambana na Ruvu Shooting Novemba 2 mwaka huu kwenye Uwanaj wa Azam Complex, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment