BEKI wa kati wa Simba, Gilbert Kaze amefurahi kufunga bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ya Bara pia kuisawazishia timu yake bao la tatu dhidi ya Yanga jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kaze raia wa Burundi aliyezaliwa Januari 25, 1992 ambaye amejiunga na Simba msimu huu akitokea Vital’O ya Burundi, aliifungia Simba bao la tatu na kuisawazishia klabu yake dakika ya 83 kufanya matokeo kuwa mabao 3-3.
Katika mahojiano yake muda mfupi baada ya mchezo huo, Kaze beki mrefu mwembamba anayezungumza kwa taratibu, aliuambia mtandao huu kwamba, anajisikia fahari kufunga bao hilo na kuifanya timu yake kupata matokeo ya sare wakitoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa mabao 3-0.
“Sikujua kama nitafunga bao, lakini nikauona mpira upo peke yake nami nikajituma na kuuwahi mpira wa faulo uliopigwa na Chollo, nashukuru kufunga bao langu la kwanza katika ligi hii pia kuifunga Yanga timu ambayo ni pinzani na hii ninayoichezea.
“Nashukuru jinsi mashabiki wa Simba walivyotuvumilia wakati tulipokuwa nyuma kwa bao 3-0 na hata makocha walifanya kazi nzuri ya kutuweka sawa kisaikolojia wakati wa mapumziko na tukaweza kufanya vizuri na kusawazisha mabao yote,” anasema Kaze.
Kuhusu ligi kuu ya bara...
Kaze anasema Ligi Kuu ya Bara ni ngumu kuliko ligi ya Burundi aliyoichezea msimu uliopita na kukiri kila timu anayokutana nayo ni nzuri na inayoonekana imejiandaa kwa kucheza ligi.
Anasema kila mechi alizocheza katika ligi kuu ya bara anakutana na washambuliaji na viungo hatari na wenye nguvu nyingi hivyo analazimika kutumia nguvu nyingi na yeye wakati mwingine ili aweze kuendana na wapinzani wake.
“Unajua ligi hii ya Tanzania ni ngumu kulinganisha na ile ya Burundi niliyocheza msimu uliopita, hapa kila timu inaonekana imejiandaa kupambana na sioni kama wanakamia bali ndivyo wanavyocheza na ndiyo maana hata wakati mwingine tunashinda kwa taabu sana,” anasema Kaze.
Vipi anaonekana hana nguvu uwanjani..
Katika mechi nyingi alizoichezea Simba, Kaze amekuwa akionekana kama mchezaji asiye na nguvu na kushawishi washambuliaji wa timu pinzani ‘kumtamani’ na kumfuata kutaka kupambana naye tofauti na beki mwenzake Joseph Owino.
Lakini mwenyewe anakiri kuwepo kwa hali hiyo lakini anawataka wadau wa soka kutofautisha nguvu na kucheza polepole, kwani yeye hachezi kwa kasi sana kulingana na aina ya wachezaji au timu pinzani anayocheza nayo.
“Naweza kuonekana sina nguvu, lakini si kweli. Unajua hata Ulaya si kweli kwamba wachezaji wote wana nguvu sawa. Sasa kama naonekana nina nguvu kidogo hicho ni kitu cha kawaida kwani pamoja na hali hiyo mbona nacheza na kocha anashukuru kwa kazi yangu.
“Mimi wakati fulani huwa nacheza taratibu kutegemea na mchezo ulivyo, huwezi kucheza kwa papara mbele ya wapinzani wenye akili ya mpira na nguvu pia. Kuna wakati beki unatakiwa kucheza kwa akili zaidi kuliko nguvu,” anasema Kaze.
‘Partinership’ yake na Owino
Katika kikosi cha Yanga, nafasi ya beki wa kati wapo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani, hawa wamecheza muda mrefu na wanamudu kucheza sambamba ndani ya kikosi cha Yanga na wakati mwingine katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Hata Arsenal kwa sasa wapo Per Mertesacker na Laurent Koscielny, ukienda Manchester United utakutana na Nemanja Vidic na Rio Ferdinand, ndani ya kikosi cha Simba kwa sasa wapo Kaze na Joseph Owino.
Tofauti na safu zote hizo, Kaze na Owino wanaonekana hawaelewani na pia wanacheza bila kuwasiliana na ndiyo maana wanaruhusu mabao mengi rahisi, lakini Kaze anasema ni hali ya kimchezo tu inayofanya wafungwe na siyo kutoelewana kwao.
“Ukuta wetu ni mpya, nasi hatujakaa kwa muda mrefu na ndiyo maana hadi leo tunacheza. Tatizo langu lililokuwepo ni kutokaa pamoja kwa muda mrefu lakini nadhani si tatizo sana kwetu,” anasema Kaze.
Mjomba hayo ni mawazo yako ya unazi wako kwa yanga! Eti owino na Kaze hawaelewani! Na unasema Nadir na Kelvin wanaelewana!! Kumbuka Simba ni miongoni mwa vikosi ambavyo havijapoteza mechi!!Ukitaka kuwa mchambuzi mzuri acha Unazi.Huyo mzee wa butua butua zanzibar heroes washamtema timu ya challenge kiwango duni bado mzee Kim wa Stars kumtema!!
ReplyDeleteKaze kazaliwa January 25, 1992. Hahahahahaha. Nina miaka 28 now lakini huwa kila nikijiangalia muonekano wangu na wachezaji ambao wadai ni wadogo huwa nashangaa sana.
ReplyDelete