Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya tatu kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa timu zote 14 kushuka viwanjani huku masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar na ile kati ya Mbeya City na Yanga.
Simba inaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma. Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.
Pia Azam TV itautumia mchezo huo kwa ajili ya mazoezi (broadcast training) kwa wafanyakazi wake. Hivyo mechi hiyo haitarekodiwa au kuoneshwa moja kwa moja.
Katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, shughuli itakuwa kati ya mabingwa watetezi Yanga na wenyeji wao Mbeya City SC. Mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna wa mechi hiyo James Mhagama kutoka Songea.
Mechi nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Ruvu Shooting na Mgambo Shooting (Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani), Oljoro JKT na Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Kagera Sugar na Azam (Uwanja wa Kaitba, Bukoba), na Ashanti United na JKT Ruvu (Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam).
WACHEZAJI 620 WATHIBITISHIWA USAJILI FDL
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imethibitisha usajili wa wachezaji 620 kati ya 624 wa timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza kutimua vumbi kesho (Septemba 14 mwaka huu).
Wachezaji wanne ambao usajili wao umezuiwa mpaka watakapokamilisha taratibu ni Emmanuel Simwanza Namwando wa African Lyon, Godfrey Bonny Namumana (Lipuli FC), na Enyinna Darlington na Chika Keneth Chukwu wote wa Mwadui FC ya Shinyanga.
Darlington na Chukwu ambao wote ni Wanigeria wamezuiwa mpaka watakapowasilisha vibali vya kufanya kazi nchini kutoka Idara ya Uhamiaji wakati Namumana aliyekuwa akicheza nchini Nepal bado hajapata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Nayo African Lyon imetakiwa kufikia muafaka na AYOSA Academy ambayo Namwando anatoka juu ya usajili kabla ya kuanza kumtumia mchezaji huyo.
Klabu ambazo zimemaliza nafasi zote 30 usajili katika FDL ni Friends Rangers FC ya Dar es Salaam, na Stand United FC ya Shinyanga wakati iliyosajili wachezaji wachache zaidi ni Burkina Faso FC. Klabu hiyo ya Morogoro imesajili wachezaji 19 tu.
Vilevile Kamati hiyo vilevile imethibitisha usajili wa wachezaji wanane wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) waliosajiliwa katika hatua ya pili ya usajili iliyoanza Agosti 14 hadi 30 mwaka huu.
Wachezaji hao ni Samir Ruhava na Amani Simba (Ashanti United), Robert Machucha na Said Ndutu (Yanga U20), Ayoub Masoud na Abdallah Selemani (Coastal Union U20), Ramadhan Kipalamoto (Simba U20) na Henry Joseph (Simba) ambaye tayari Hati yake Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imeshawasili.
No comments:
Post a Comment