Search This Blog

Monday, September 16, 2013

KIBADENI ALIDHISHWA NA KIWANGO SIMBA, MECKY MEXIME AKUBALI KIPIGO


Kocha wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amekubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na mtandao huu mara baada ya mchezo huo, Mexime ambaye ni nahodha wa zamani wa Taifa Stars amesema, timu yake ilicheza vizuri lakini uwezo ulioonyeshwa na Simba uliwafanya wastahili kupata ushindi.

Alisema kikosi chake kilijitahidi kadiri ya uwezo wake kuweza kupata ushindi lakini makosa mawili waliyofanya yaliiwezesha Simba kupata mabao mawili na kuibuka na ushindi.

“Nimekubali kwamba nimefungwa na Simba kihalali kabisa katika hali ya kawaida ya kimchezo, wenzetu walitumia vyema nafasi walizopata na kuweza kufunga mabao mawili yaliyowawezesha kupata ushindi.

“Timu yangu haikucheza vibaya japokuwa tumefungwa mabao mawili, kilichotokea ni hali ya mchezo ambayo inaweza kuikuta timu yoyote iliyo imara na kutokana na matokeo haya tunajipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo unaofuata ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi kwenye ligi,” alisema Mexime.

Kwa upande wake, Kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema kikosi chake kimecheza vizuri hadi kikaibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa hali inayompa faraja ya kuwa na kikosi bora msimu huu.

“Siyo siri nawashukuru vijana wangu kwamba wamejituma ipasavyo na kuweza kupata ushindi huu mnono dhidi ya timu hodari kama Mtibwa. Kila idara ilihakikisha inafanya kazi vizuri japokuwa kulikuwa na makosa madogo madogo ambayo natakiwa kuyarekebisha kabla ya mchezo mwingine,” alisema Kibadeni.

Matokeo ya mechi ya jana yameiwezesha Simba kufikisha pointi saba.

No comments:

Post a Comment