Na Baraka Mbolembo
Mafanikio ndiyo kipimo sahihi cha
ubora. Timu ya Taifa ya Ethiopia imefuzu kwa hatua ya kumi bora, na sasa
watacheza michezo miwili ya play off kuamua timu tano ambazo zitaiwakilisha
bara la Afrika katika fainali zijazo za kombe la dunia, nchini Brazil. Ethiopia
ilipata ushindi muhimu ugenini dhidi ya timu ya Taifa ya Afrika ya Kati na
kufuzu mbele ya timu za Afrika ya Kusini, na Sierra Leone.
Chini ya kocha, Mzawa Sewnet Bishew,
ambaye alichukua nafasi ya kuinoa timu hiyo, oktoba, 2011 kutoka kwa Mbelgiji,
Tom Saintfiet, Ethiopia ilifanikiwa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika,
ambazo zilichezwa nchini Afrika ya Kusini, mapema mwaka huu, imetokea katika
mapito mengi.
Mafanikio ndiyo kipimo sahihi cha
ubora, ila naendelea kuwashangaa wapenzi wa soka nchini wanaomlaumu kocha wa
timu yetu ya Taifa, Taifa Stars. Wanasema kuwa anatakiwa kuzunguka hadi
mikoani, wilayani, na vijijini akatafute vijana wenye vipaji zaidi, badala ya
kuendelea kuchagua na kuwatumia wachezaji wa timu tatu tu, Simba, Yanga, na
Azam FC.
Katika hili, tunakuwa tunamkosea
heshima, kocha Kim Poulsen, tunazikosea heshima klabu ambazo zimekuwa na
mchango mkubwa katika timu yetu ya Taifa. Tunasahau kuwa kila kijana ndoto yake
ni kufika Dar es Salaam, na kucheza soka. Tunasahau kuwa asilimia kubwa ya
wachezaji wa klabu hizo wamekuwa wakitoka mikoani, wilayani, na katika vijiji
ambavyo tunahitaji, Kim aende kusaka wachezaji.
Kama wachezaji wa klabu hizo ni
wazuri na wana ubora wa kuiwakilisha Tanzania, wanatakiwa kupewa nafasi, ila
endapo kocha, Kim anakuwa anawajaza tu huku viwango vyao vikiwa ni vya chini na
kuwaacha wale walio katika ubora kwa kigezo cha U-simba, U- yanga, au U- azam
atakuwa anatukosea heshima.
Kama tungekuwa na wachezaji wa
kimataifa wanaocheza ng’ambo, ingekuwa ni nafuu zaidi kwetu, na hapo ndipo
tungekuwa na jukumu la kutozitegemea timu zetu kubwa kutoa wachezaji wengi
katika kikosi cha kwanza cha Stars. Kuna baadhi ya wachezaji katika miaka ya
karibuni walipata nafasi ya kucheza nje ya nchi, wapo waliopata nafasi,
ulaya, Asia na Marekani, lakini wote wakaishia kucheza timu za madaraja ya
chini, lakini ndiyo wachezaji wetu hao ni lazima tuwakubali, ndiyo wachezaji
wetu nyota hao.
Labda ubora mdogo wa timu yetu ya
taifa unatokana na mfumo wetu wa ‘ ubabaishaji’ katika soka, leo hii mchezaji
wa ligi kuu na anayepata nafasi katika timu ya Simba, au Yanga na Azam FC,
anaweza kuokotwa tu, mtaani huku akiwa hajaonekana kucheza ligi za madaraja ya
chini. Ni huyo baada ya mwezi mmoja akiwa Simba, Yanga ama Azam anaitwa timu ya
taifa kwa kuwa ameonesha kiwango kikubwa anachopewa sifa za Leonel Messi.
Wapo wachezaji ambao huruka moja kwa
moja kutoka katika soka la mtaani, lakini tayari amekuwa akitambua ugumu wa
ligi daraja la tatu. Ilikuwa ni wakati huo, nyota kama Abdallah King Kibadeni
alipoingia Simba akiwa na miaka 17 na kufanya mambo makubwa, au Mzee Hamis
Kilomoni ambaye alicheza mchezo wake wa kwanza akiwa mchezaji wa Simba dhidi ya
Yanga na kufunga mara nne, wakati huo akiwa na umri wa miaka 17. Miaka
imekwenda, na Pele atabaki kuwa mfalme wa kandanda duniani, kwa nini asiwe
hivyo? Alianza soka la kulipwa akiwa na miaka 16, na mwaka mmoja baadae
akafunga mabao sita katika fainali za kombe la dunia, lakini ni wachezaji Lukas
Podolsk, na Tomas Muller ambao wameweza kufunga mabao zaidi ya manne katika
fainali za kombe la dunia, wakiwa na umri mdogo. Podolski alifunga matano, 2006,
na Muller pia alifunga mabao matano katika ‘ Woza 2010’.
Lakini leo hii sisi tunamlaumu kocha
wetu kwa kuzaja wachezaji wengi wa klabu tatu katika kikosi. Simba na Yanga
kutoa wachezaji wengi si hoja ya msingi. Mfano, zitazame timu za Hispania,
Ujerumani, na Italia, klabu zao kubwa ndizo zilizopeleka mataji ya kombe la
dunia kwa vipindi tofauti. FC Barcelona, na Real Madrid kwa upande wa Hispania,
Bayern Munich na Borussia Dortmund kwa upande wa Ujerumani na Juventus, AC
Milan, na AS Roma kwa upande wa nchini ya Italia. Wapo wachezaji bora ambao
hupenya na kupata nafasi wakitokea timu nyingine, Fernando Torres na David
Silva ( Hispania), Mesut Ozil, na Sam Khedira ( UJerumani), Andrea Pirlo (
Italia).
Kinachokosekana moyo hasa wa
uzalendo, kwa wachezaji hawatambui thamani ya kuiwakilisha timu yao ya Taifa,
ni wavivu wa mazoezi, wanapenda starehe, na ni wachezaji ambao hawajipangii
muda wa kazi na muda wa kupumzika, inakuwaje mchezaji ambaye tayari anachezea
Simba, Yanga, au Azam ( nazitolea mifano timu hizi kwa kuwa ndiyo nguzo ya
mpira wetu kwa sasa), anacheza michezo ya ‘ ndondo’, mchezaji wa timu ya taifa
kucheza michezo ya ‘ maharage’ huko ni kutojitambua na kujithamini, hivyo mtu
kama hawezi kujithamini mwenyewe atathamini nini zaidi?.
Lakini sijui kwa nini
huamua kufanya hivyo wakati wanatambua ni makosa kwa waajiri wao, kama
hawachukuliwi hatua ni tatizo, ni inawezekana uongozi hauwatendei haki katika
baadhi ya mambo ya siri yaliyomo katika mkataba na kuamua kuwaonesha kwa mtindo
huo.
Kama lawama ni lazima tuzitupe
kwanza kwa wachezaji wetu wenyewe, kwa viongozi wa juu wa klabu zetu kubwa kwa
kushindwa kwao kuwaendeleza wachezaji wa timu ya taifa katika mfumo tulionao.
Miaka miwili iliyopita niliwahi kushangazwa na jambo Fulani. Unajua uzalendo wa
maslai ni mbaya sana, mtu anapenda kwa sababu anatambua kuna faida nje ya
mapenzi aliyonayo. Nilikuwa nimekaa mimi na baadhi ya watu, tulikuwa kama sita-
hadi nane hivi, na ndani yake walikuwepo watu wawili wa mpira ambao kama
ningewarekodi na kuwaonesha video ya walichokuwa wanafanya husingemuamini tena
hata kama wakati mwingine angeweza kuzungumza ukweli juu ya jambo au kitu
Fulani.
Wakati, mchezo wa Stars na Jamhuri ya Afrika ya Kati ulipigwa Machi, 2011 katika uwanja wa taifa na Stars kushinda kwa bao la dakika za majeruhi kupitia kwa Mbwana Samatta. Katika mchezo ule, Stars ilianza kufungwa, katika dakika ya saba tu, tulikuwa tukifuatilia mchezo ule kupitia matangazo ya redio, tulikuwa na majukumu Fulani ya kikazi. Ajabu nikawaona, aliyekuwa kiongozi wa juu wa TFF, Yule wa klabu moja kubwa nchini wakishangilia. Niliiuzika sana, sikupenda nikajikuta kutokana na hasira nikasema, ‘ Tutawafunga tu’, kweli wakati Samatta anachomoa wananiuliza, ‘ Stars imefungwa la pili’, nikawajibu ‘ Samatta kawachinja’ wakashika mikono juu. ‘ Unajua walikuwa wakizungumza nini? Acha ni siri yangu ni heshima ambayo nitabaki nawatunzia daima.
Lakini unategemea kama viongozi wa juu wanakuwa na tabia kama hizi? Nitaishangilia Ethiopia nchini Brazil mwakani, ni mfano wa kuigwa kwa ukanda wa Cecafa, play off hazina mwenyewe ila timu yetu ya taifa ya Tanzania ni ya Simba, Yanga, na Azam kwanza, nyingine nyongeza tu. Bado tuna uhaba wa wachezaji wa nafasi muhimu katika soka letu. Tuwe wazalendo
0714 08 43 08
Swadaqta kaka umenena,players wetu wanatuangusha hawataki kujituma uvivu tu umewajaa.
ReplyDelete