Mshambuliaji aliyetokea kukonga mioyo ya mashabiki wa Simba kwa
kufumania nyavu, Betram Mwombeki amekwaa kisiki katika usajili wake
kuichezea timu hiyo baada ya kuwekewa pingamizi na klabu yake
aliyoichezea msimu uliopita, Pamba ya Mwanza.
Awali iliripotiwa kuwa Mwombeki amesajiliwa na
timu hiyo akitokea nchini Marekani, hata hivyo Pamba wamepinga taarifa
hizo na kusema kuwa mchezaji huyo aliichezea timu yao Ligi Daraja la
Kwanza na kufunga mabao mawili msimu uliopita.
Mwenyekiti wa Pamba, Kazimoto Miraj Muzo aliiambia
Mwananchi kuwa Mwombeki alikuwa Marekani miaka ya nyuma na mwaka jana
alijiunga na Pamba wakati wa dirisha dogo la usajili na kucheza mechi
kadhaa tofauti na taarifa kuwa ametokea Marekani.
Muzo alisema kuwa hakuweza kucheza mechi nyingi
kutokana na kukabiliwa na maumivu ya goti. “Si kweli kuwa ametokea
Marekani, tupo hapa na aliichezea timu yetu. Tuliwaambia Simba,
wakabisha na sasa tutakutana mbele ya sheria,” alisema Muzo.
Alifafanua kuwa walizungumza na Makamu Mwenyekiti
wa Simba, Joseph Itang’are kuhusiana na usajili wa mchezaji huyo, lakini
hakuonyesha kujali taarifa hiyo.
“Tumewasilisha vielelezo vyetu TFF, tunasubiri
matokeo ya kikao cha Kamati ya Alex Mgongolwa kutoa uamuzi wake,
tumedhamiria kupigania haki yetu mpaka mwisho” alisema.
Alisema kuwa kiasi gani cha fedha watakachoidai
Simba iwalipe ni siri, kwani daima wao huwa hawapendi kuweka hadharani
masuala ya fedha, hasa za kumuuza mchezaji.
Itang’are alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo
alithibitisha kuongea na Pamba na kuahidi kulifanyia kazi. “Pamba ni
ndugu zetu, miaka ya nyuma walitupa wachezaji wengi kama Hussein Marsha,
John Makelele, George Masatu, Juma Amir na wengine, na kwa hili sidhani
kama tutashindwana,” alisema Itang’are.
Wakati Simba inakabliwa na kikwazo kuhusiana na
Mwombeki, Yanga inaelekea kupeta kwa mchezaji, Mrisho Ngassa kutokana na
ukweli kuwa Simba hajawasilisha taarifa nyingine zaidi ya mkataba tu.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment