• YANGA v COASTAL; MWENYEJI HAOGOPI GIZA
• Na Baraka Mbolembole
Yanga iliifunga, timu ya Ashanti United katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu, siku ya jumamosi iliyopita kwa mabao 5-1, katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu nchini, wataikaribisha timu ya Coastal Union ya Tanga katika mfululizo wa ligi hiyo.
Coastal ambao walianza na ushindi wa mabao 2-0 ambao waliupata siku ya ufunguzi wa msimu, wapo katika nafasi sawa na Yanga kuelekea mchezo wa jioni ya leo. Kocha wa Yanga, Ernest Brandts huenda asiwatumie nyota wake wa nafasi ya kiungo, Athumani Idd ' Chuji' na Haruna Niyonzima ' Fabregas' kutokana na kusumbuliwa na maumivu, pia mlinzi wa kati, Kelvin Yondan tayari imethibitishwa kuwa hatoweza kucheza, hali hiyo inaweza kumtatiza Brandts katika mipango yake, lakini ana uhakika wa urejeo wa Frank Domayo katika kiungo, huku Salum Telela akiwa ameonesha kiwango cha juu katika michezo ya karibuni hali ambayo inatia matumaini kwa kocha huyo ' mkali wa mbinu'.
Kwa upande wa timu ya Coastal, wao wanajipa ubingwa kabla ya kucheza mechi. Msimu uliopita walianza vizuri na kushinda ' kidogo kidogo' na wakaonesha mwanga katika miezi miwili ya mwanzo mwa msimu, lakini taratibu wakaanza kuishiwa nguvu hasa kipindi ambacho ratiba ilikuwa ikiwapeleka ' midomoni mwa mabingwa', Yanga, na Simba, huku wakiwa wameanguka vibaya katika mtihani wao wa kwanza msimu uliopita, mbele ya timu ya Azam FC, walipofungwa kwa mabao 4-1.
Muda sasa umepita, na Coastal wamebadilika kwa namna nyingi sana, kimtazamo na kimipango ni timu yenye dhamira hasa, lakini vitu hivyo haviwezi kuwapa ubingwa kama wataishia kupoteza michezo muhimu kama huu wa leo dhidi ya Yanga. Mechi yao ya mwisho kukutana timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika uwanja wa Taifa, Mei mosi, mwaka huu, na Yanga walishinda kwa mabao 2-0, Oktoba, mwaka jana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.
Lakini muda umekwenda sana toka wakati ule hadi sasa, na kocha Hemed Morocco ameweza kuongeza nguvu kwa kuwasajili wachezaji wazoefu msimu huu. Hatakuwa na kiungo, na nahodha wake Jerry Santo ambaye ana majeraha, kiungo mshambuliaji, Abdi Banda ambaye alifunga bao la shuti la umbali mrefu katika ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Oljoro hatotumika katika mchezo huo kutokana na sheria za usajili wa mkopo kumfunga kucheza dhidi ya timu yake inayomlipa mshahara, lakini bado timu hiyo inao wachezaji wa kutosha ambao wanaweza kuwarudisha, Yanga nyuma. Haruna Moshi, Razaq Khalfan, Suleiman Kassim ' Selembe' wote wapo fiti na tayari kwa mchezo wa jioni hii. Lakini wanatakiwa kutambua kuwa wanakwenda kucheza na ' Yanga, inayofunguka'.
Kitu kizuri kutoka kwa kila timu ni kwamba, timu zote zina wachezaji wenye sifa zinazofanana kiuchezaji kuanzia katika maeneo ya kiungo. Salum Telela na Razaq ni viungo ambao wamekua pamoja katika uchezaji wao katika timu za Taifa za vijana, na baadae Yanga, achilia mbali wakiwa shule ya Sekondari Makongo, wana nguvu, pumzi na uwezo wa kupiga pasi za mbali, ni wepesi wa kuifuata mipira kutoka kwa walinzi na kuisukuma timu mbele, Razaq alipata wakati mzuri kuliko Telela katika uchezaji wa nafasi hiyo, kwa kuwa Telela alikuwa akitumika kama mlinzi wa pembeni zaidi, hadi alipokuja kugunduliwa ni kiungo mzuri miaka miwili iliyopita na kocha Kostadin Papic , lakini anaweza kutumia ukubwa wa jina la timu yake na kumfunika Razaq.
Kocha, Brandts bila shaka atafanya kila namna kuona kiungo, Niyonzima akiwepo kikosi jioni ya leo, ili kuleta balansi sawa ya upangaji mashambulizi, na uwepo wa Niyonzima ni jibu zuri kwa upande wao mbele ya Coastal ambayo, inaye kiungo mahiri mchezesha timu, Haruna Moshi Boban. Wote wawili ni wakali katika upigaji wa pasi za kupenyeza, kumiliki mpira na kuongoza mchezo, tofauti yao ni kwamba Niyonzima ni kiungo muhamasishaji ambaye anaweza kuifufua timu hata ikiwa katika wakati mgumu uwanjani, kitu hiki hana Boban, japo anabaki ni mchezaji mwenye maarifa zaidi katika mchezo wa leo. Wote wawili ni ni bora katika kufunga mabao ‘ yasiyotarajiwa’, ni wachezaji ambao wanapokuwa uwanjani timu nzima hujengwa kupitia wao.
Domayo? Ni kiungo mzuri sana katika mashambulizi ya ‘ counter attack’, ni kiungo wa kisasa ambaye hana ‘ madoido’ mengi mchezoni, mpigaji mzuri wa pasi za mbali zenye macho, si mfungaji mzuri, lakini stahili yake ya uchezaji inamfanya kuwa mfungaji wa mabao muhimu kwa timu ni faida kuwa naye hasa pindi timu inapokutana na viungo staili ya Boban. Lakini sifikirii kama ataweza kufanya kila kitu na kuihamasisha timu kipindi mambo yakiwa ‘ mrama’ uwanjani. Boban ni rahisi kupotea moja kwa moja mchezoni, lakini ni kazi kubwa sana kumkabili wakati anapoamua kucheza kwa walau asilimia 60 tu za kiwango chake.
Kuna haja ya mabeki wa Coastal na benchi lao la ufundi kuongeza umakini, ufundi, na mbinu za kuwakabili washambuliaji, Jerry Tegete, Didier Kavumbagu, na Hussein Javu, tunaposema timu inafunguka ni kuona soka la mashambulizi kutoka kwao, Jerry ni mviziaji na mfungaji mzuri kwa kutumia miguu, ‘Kavu’ ni mchezaji mwenye sifa za kuitwa mshambuliaji namba moja, ana uwezo wa kupokea mipira ya juu na kuimiliki na hata ile ya chini imekuwa si tatizo kwake, lakini kucheza dhidi ya walinzi kama Crispian Odula na Juma Nyosso, si rahisi kupata nafasi ya kufanya kila ulichobarikiwa nacho, ni walinzi ambao ‘ wana usongo’ muda wote na bahati kwa Coatal kuwa walinzi wao hawapendi kufungwa.
Ni kitu kizuri sana hicho, kutopenda kufungwa, lakini endapo Nyosso atabaki kuwa ni yule yule tu wa siku zote timu itayumba na nyufa zitatokea na hapo ndipo watakapoadhibiwa. Ndiyo, kila mmoja anatambua uwezo wa kipa Shaaban Kado, lakini tusisahau pi kuhusu kipaji cha Jerry na ufungaji wa ‘Kavu’. Daniel Lyanga, anatosha kuimaliza Yanga kwa staili yoyote ile kama Boban atacheza, kama Selembe atamrudisha nyuma, David Luhende na kupiga krosi za juu, ni kijana mdogo lakini tayari ameshazijua nyavu za ligi kuu, ana uwezo wa kufunga kwa vichwa, mashuti na hata kutengeneza nafasi kwa wenzake kuweza kufunga.
Kama Cannavaro na Mbuyu watacheza kama walivyocheza dhidi ya Ashanti bila shaka watamuweka matatizoni kipa wao Ally Mustapha ‘ Barthez’, Lyanga ni mwepesi sana na anajua kujipanga katika wakati sahihi.
NANI MSHINDI; Huwezi kutabiri kirahisi mchezo kama huu, lakini ukitazamana namna Saimon Msuva alivyocheza dhidi ya Ashanti na kutengeneza mabao mawili kwa mipira ya krosi na yeye akifunga bao moja akiuwahi mpira ambao ulikuwa katika eneo la hatari ni wazi Yanga wanaweza kufanya hivyo tena mbele ya Coastal, huyu ni mshambuliaji wa ziada anapokuwa mchezoni, anacheza zaidi pembeni lakini anapoingia katika eneo la hatari anajigeuza na kujivisha sifa za mshambuliaji- mfungaji. Ni mechi kali na nguvu lakini Ushindi wa Coastal upo mikononi kichwani mwa Boban. Na ule wa Yanga upo katika miguuu ya Msuva. Atakayecheza kwa kuisaidia timu atafanikiwa kuipa ushindi timu yake. Yanga si ndiyo wenyeji, basi twendeni Taifa, tusiogope gizaaaa
0714 08 43 08
No comments:
Post a Comment