Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema
kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo wa kushindana katika mashindano
yoyote, kwani tayari kimeiva.
Akizungumza
na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es
Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye mechi
zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast
kimethibitisha hilo.
“Kiwango
mlichoonyesha katika mechi hizo kila Mtanzania anayewafuatilia
amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya
kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais Tenga na kuwataka kupigana kwa
ajili ya Tanzania.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kesho (Julai 13 mwaka
huu) saa 9 kamili alasiri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itacheza na
Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania
tiketi ya kucheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika
Kusini.
Rais
Tenga amesema TFF, mdhamini Kilimanjaro Premium Lager, Kamati ya
Ushindi na Watanzania kwa ujumla wanawaunga mkono kwani wamekuwa
wakiboresha kiwango chao kila wanavyozidi kucheza mechi tangu wake chini
ya Kocha Kim Poulsen, Mei mwaka jana.
Wakati
huo huo, Rais Tenga ameahidi kumpatia tiketi ya kwenda Uganda kwenye
mechi ya marudiano mshabiki Wiseman Mwakyusa Luvanda anayetembea kwa
miguu kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kesho.
“Kama
ni kweli anakuja kwa kutembea, huyu ameonyesha kiwango kikubwa cha
uzalendo kwa timu ya Taifa, nitampatia tiketi ya kwenda Kampala
kuishangilia Taifa Stars kwenye mechi ya marudiano,” amesema Rais Tenga.
…POULSEN, MICHO WATABIRI MECHI KALI
Makocha
wa timu hizo Kim Poulsen wa Taifa Stars na Sredojvic Micho wa The
Cranes wamesema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwa vile kila mmoja
amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.
Wakizungumza
na Waandishi wa Habari leo, makocha wote waliezea ubora wa wapinzani
wao, lakini wakasisitiza kuwa wanaingia uwanjani kuhakikisha wanashinda
ili kujiweka katika mazingira mazuri kwa ajili ya mechi ya marudiano
itakayochezwa Kampala wiki mbili zijazo.
Kim
alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa ubora wa viwango vya FIFA katika
ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni changamoto kwao ingawa
wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.
Naye
Micho aliyefuatana na nahodha wake Hassan Wasswa alisema Taifa Stars
imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini ya Kim, na itakuwa na wachezaji
tisa wa kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia
wakati kwa upande wake atakuwa na wachezaji wawili tu.
No comments:
Post a Comment