Search This Blog

Tuesday, July 30, 2013

MAWAKALA WA SOKA WA FIFA NA WAAMUZI WA VPL KUFANYA MTIHANI

Mtihani wa uwakala wa wachezaji (players agent) na uwakala wa mechi (match agent) wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Alhamisi ya Septemba 26 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kutakuwa na jumla ya maswali 20 kwenye mtihani huo, 15 yanatoka FIFA kuhusiana na kanuni za kimataifa za mpira wa miguu na matano yatatoka TFF kuhusiana na kanuni mbalimbali zinazotawala mchezo huo nchini.

Kwa ambao wangependa kufanya mtihani huo utakaokuwa katika lugha ya Kiingereza ambayo ni moja kati ya lugha nne rasmi za FIFA wanatakiwa kujisajili TFF kwa ada ya dola 50 za Marekani ambapo watapewa utaratibu na maeneo ambapo mtihani huo unalenga.

Mtihani huo utafanyika saa 4 kamili asubuhi, na muda wa kufanya mtihani hautazidi dakika 90.

Mpaka sasa Tanzania ina mawakala watano wa wachezaji wanaotambuliwa na FIFA. Mawakala hao ni John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully.

WAAMUZI VPL KUFANYA MTIHANI WA UTIMAMU WA MWILI
Waamuzi wote wa daraja la kwanza (Class I) wanaotaka kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2013/2014 wanatakiwa kuhudhuria mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) utakaofanyika katika vituo viwili.

Mtihani huo utafanyika Agosti 12,13 na14 mwaka huu katika vituo vya Dar es Salaam na Morogoro. Kituo cha Mwanza kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Manyara, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora.

Kituo cha Dar es Salaam kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Njombe, Pwani, Ruvuma na Tanga.

Washiriki wote wanakumbushwa kuwa ni lazima wafuate utaratibu huo wa vituo, na si vinginevyo. Pia waamuzi waliofungiwa (sio maisha) wanatakiwa kushiriki katika mtihani huo.

RATIBA LIGI DARAJA LA KWANZA AGOSTI 14
Ratiba ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2013/2014 inayoshirikisha timu 24 zilizo katika makundi matatu zikicheza kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini) inatarajiwa kutolewa Agosti 14 mwaka huu.

Kundi A linaundwa na timu za Burkina Moro ya Morogoro, JKT Mlale (Ruvuma), Kimondo SC (Mbeya), Kurugenzi Mufindi (Iringa), Majimaji (Ruvuma), Mkamba Rangers (Morogoro), Polisi (Iringa) na Polisi (Morogoro).

African Lyon (Dar es Salaam), Friends Rangers (Dar es Salaam), Green Warriors (Dar es Salaam), Ndanda (Mtwara), Polisi (Dar es Salaam), Tessema (Dar es Salaam), Transit Camp (Dar es Salaam) na Villa Squad (Dar es Salaam) zinaunda kundi B.

Timu za kundi C ni JKT Kanembwa (Kigoma), Mwadui (Shinyanga), Pamba (Mwanza), Polisi (Dodoma), Polisi (Mara), Polisi (Tabora), Stand United (Shinyanga) na Toto Africans (Mwanza).

Tunapenda kukumbusha kuwa dirisha la usajili kwa madaraja yote ni moja ambapo usajili wa hatua ya kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti 3 mwaka huu wakati hatua ya pili ni Agosti 14 hadi 29 mwaka huu. Dirisha dogo litafunguliwa Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment