Search This Blog

Sunday, July 28, 2013

MAKALA: UDHAIFU WA LA LIGA - UIMARA WA LIGI KUU YA ENGLAND - NA KWANINI YANGA WANAWEZA KUWA SAHIHI KUKATAA DILI LA KUONYESHA MECHI ZA LIGI KUU KWENYE TV



Hili haliwezi kuja na mshtuko kwa mtu yoyote anayefuatilia ligi kuu ya Hispania kwa miaka kadhaa iliyopita, lakini La Liga imejitengenezea mfumo ambao taratibu unaiua ligi hiyo. Hivi karibuni wakati nchi ikiingia katika kipindi cha anguko la uchumi lilosababisha madeni makubwa na upungufu mkubwa wa ajira, pia klabu kadhaa za soka za nchi hiyo zimeingia kwenye matatizo ya kifedha yanayotishia uhai wao kwenye ramani ya soka.

Lakini pamoja uongozi mbovu na mipango tasa ya maendeleo ilyonayo baadhi ya vilabu, moja ya sababu kubwa ya vilabu vya Hispania kuwa kwenye hali mbaya ya uchumi imeletwa na namna wanavyojadili mikataba yao ya kuuza haki za matangazo ya TV.

Tofauti na Premier League, Serie A, Bundesliga na Ligue 1, hata ligi kubwa michezo mengine huko Amerika ya Kaskazini kama vile   (NFL, NBA, MLB, NHL), La Liga ni tofauti sana - klabu zinafanya biashara ya kuuza haki za matangazo ya TV binafsi - kila timu kimpango wake. Mfumo huu unafanya kazi kwa baadhi ya vilabu nchini Spain - klabu mbili, Real Madrid na FC Barcelona, klabu kubwa duniani ambazo zinatajwa kuvuna kiasi kinachofikia $180 million kwa mwaka kutoka dili za mauzo ya haki za matangazo ya TV ambazo wanajadili wao binafsi.

Lakini ukilinganisha namba hizi na zile wanazopata klabu inayofuatia kupata fedha nyingi ambayo ilishika nafasi ya 3 msimu uliopita, Atletico Madrid kunakuwa na pengo kubwa sana. Atletico ilipokea kiasi cha $61 million kutoka kwenye mauzo ya haki za TV. Kutokea hapo namba za kiasi cha fedha wanachopkea vilabu vingine zinazidi kwenda chini; Rayo Vallecano ilimaliza nafasi ya nane msimu uliopita ilipata kiasi cha $18 million kutoka kwenye dili za haki za matangazo ya TV, wakati timu uliyoshika nafasi ya 15 Granada iliweka kibindoni $16 million - fedha ndogo kuliko anayodaiwa Lionel Messi na serikali ya Spain kwa kukwepa kodi. 

Jambo ambalo lilipelekea kupata ahueni kwa wengi wiki baada ya serikali ya nchi hiyo kusema kwamba itasukuma haraka mchakato wa kupata sheria mpya mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu - sheria ambayo itaipa Liga de Futbol Profesional (LFP), Chama kinachosimamia ligi za soka za Spain - mamlaka ya kuweka mfumo wa ugawanyaji sawa wa mapato ya haki za Television kwa namna inavyofanyika kwenye ligi nyingine kubwa duniani. Serikali pia itafanya kazi na LFP katika kuhakikisha vilabu vinalipa kiasi cha   $1.3 billion mpaka 2016 ili kupunguza deni wanalodaiwa, wakitoa amri kwa vilabu 42 vinavyoshiriki kwenye La Liga na Segunda kukata matumizi yao kwa kiasi cha $130 million msimu ujao. Hii ni hatua nzuri ambayo italeta afya ya ushindani katika moja ya ligi bora duniani - ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na vilabu viwili Real na Barca. 

Premier League ndio mfano mkuu wa namna mgawanyo wa kiuchumi unavyofanyika kutokana na fedha inayopatikana kupitia uuzwaji wa haki za matangazo ya TV. Ligi hiyo imeendelea kuwa maarufu kuliko zote duniani - pia ndio mfano mzuri wa namna vilabu vyote vinavyoweza kunufaika na fedha za kutoka kwenye matangazo ya TV - kiasi cha kuchafanya hata timu inayoshuka daraja inufaike kwa kiasi kikubwa kama ilivyo kwa bingwa. Msimu uliopita, Queens Park Rangers, ambao wameshuka daraja, walipata fedha nyingi za kutoka kwenye dili za haki za matangazo ya TV kuliko zile walizopata Bayern Munich na Borrusia Dortmund ukichanganya. Tena kwa mwaka huu fedha hizo zinaweza kuongezeka kwa timu nyingine itakayofuata mkondo wa QPR kwa sababu Premier League inatagemea kuingiza zaidi ya  $8 billion kutoka kwenye uuzwaji wa haki za matangazo ya TV katika kipindi cha miaka mitatu. 

Mfumo ambao La Liga wanataka kuondokana nao nahisi unaweza ukaja hapa Tanzania. Hivi karibuni kamati ya ligi imeingia mkataba na Azam Media Group kurusha matangazo ya mechi za Ligi Kuu ya Tanzania bara kwa mkataba ambao utafanya vilabu vyote vinashoriki ligi kupata mgawanyo sawa wa mapato. Lakini baada ya hilo kufanyika zimeibuka taarifa kwamba klabu bingwa ya Tanzania Yanga imekataa kuafikiana na mpango huo, ikitoa sababu kwamba yenyewe ni klabu kubwa haiwezi kulipwa fedha sawa na timu nyingine (Yale yale ya FC Barcelona na Real Madrid), lakini pia wakatoa sababu kwamba hakukuwa na utangazaji wa tenda ya dili hilo kwa makampuni mengine?

Yanga wanaweza kuwa sawa kabisa kwenye sababu zao walizotoa - hasa hili kutokukubali kulipwa sawa na vilabu vingine. Kivipi? Ngoja tuangalie mfano wa ligi kuu ya England.

Mgawanyo wa mapato yanayotokana na mauzo ya haki za matangazo ya TV wa ligi kuu ya England upo kama ifuatavyo.

* Asilimia 50 ya fedha zote zinazopatikana kutoka kwenye mauzo ya haki za matangazo ya TV - hugawanywa sawa kwa vilabu vyote - yaani kama imepatikana millioni 10 basi kila timu itapa laki 5 miongoni mwa vilabu 20.

*Asilimia 25 - Hugawanya kutokana na kiwango cha timu kwenye msimamo wa ligi. Kwa maana ya mshindi wa kwanza wa ligi lazima apate kiasi kikubwa kuliko aliyeshika nafasi ya mwisho. Hii ni inaleta hali kushindana zaidi kwenye ligi kwa maana ya timu kushindania kupata mgawo mkubwa kwa kushika nafasi za juu kwenye ligi.

*Asilimia 25 iliyobakia inagawanywa kulingana na uonyeshwaji wa mechi za vilabu husika. Kwa sababu sio mechi zote zinazoonyeshwa live. Hivyo vilabu hupata mgawo wa hizi asilimia 25 kutokana na namna mechi zao zilivyooneshwa kwenye TV.

Huu ndio mfumo sahihi ambao unaifanya ligi kuu ya England kuwa mfano wa kuigwa - unaifanya ligi hiyo kuwa na ushindani mkubwa. Tanzania inapaswa tufuate mfumo huu katika hili suala la haki za matangazo ya Television.

By Aidan Seif Charlie

9 comments:

  1. Aidan
    Very interesting analysis, tatizo ni uongozi mbovu, nakubaliana na Yanga tenda itangzwe na makampuni ya Television yaje na offer. Sasa Rage kupewa million 100, mtu mzima anacheka na kujisahau? Simba wana safari ndefu huyu ni janga kwa ustawi wa timu.

    ReplyDelete
  2. Timu za bongo kwa mbwembwe ni balaa! Hivi yanga nayo ni timu kubwa kweli,au wanatafta umaarufu tu! Timu kubwa haijawah hata kufika 1/2 fainali ya mashndano ya CAF! Chkuen hela hiyo toka kwa Azam!

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hivi wewe unaongea kufurahisha au umetumwa? Yanga ina wapenzi wengi Kulikoni timu yeyote, ikijipanga inaweza kuwa timu tajiri saana. Milioni 100 za Azam ni $67000 ni hela ya kuwalipa Yanga?

      Delete
    2. Kaka hapa hawaongelei ukubwa wa kushindana mashindano Afrika kama huelewi mada kaa kimya waache wenye mawazo yao wewe baki kusoma tu. Mtoa mada kaja wakati muafaka Tanzania hatuwezi kuendelea kwa kujiona tupo cheap sana. watu wanakuja na vimawazo vyao wanavipenyza kiujanja ujanja vinapita bila kufuata taratibu. Yanga wako sahihi kabisa. unapoona Simba na Yanga kila ratiba zinafunga msimu ni kwa sababu ya kulipa madeni yote ya nyuma. Hapa hakuna uchawi TFF wanazitegeme mno hizi timu, ukienda mechi zingine nje ya simba na yanga mgawo wa timu unakuwa hadi shilingi 3,000. Hazina ya mashabiki ndio zinazifanya samba n Yanga kuwa kubwa nchi hii

      Delete
  3. kwani iyo bodi ya ligi haina viongozi wa yanga mpaka wana saini mkataba na kabla ya kusaini klabu hazikupelekewa presenation ya kuukubali au la mkataba wa maonyesho ya tivi jamani tubadilike twendeni shule tuache ujanja ujanja kwenye mambo ya msingi tunaitengeneza ligi ipi ya ushindani wakati ashanti anajua anachukua hela anayopata bingwa yeye akishuka daraja wakati huohuo.

    ReplyDelete
  4. kamati ya mpito itasainije miaka 3? wasubirie uongozi mpya mambo yafanyike na mjitahd kuepuka ushabiki na kejeli, tujenge soka letu jama.

    ReplyDelete
  5. Kwa Tz cjui loading..........

    ReplyDelete
  6. Kuna wakati kama huna la kusema, ukibaki kam msomaji ni busara ya hali ya juu. Analysis imetolewa, jenga hoja kutokana na analysis sio ushabiki. Binafsi nakubaliana na Yanga baadhi ya vipengele hasa khs tenda na Bodi ya mpito kuingia mkataba wa miaka mitatu. Jamani tuimarishe michezo kwa kuwa wazalendo si washabiki. kwani kwa kuimarisha ligi yetu ndo hata fursa za kushiriki mashindano ya Africa, CHAN, na baadae World cup ndo tunaweza kufika, lakini kwa ujanja ujanja huu, hatutafika hakika. Big up Shafii

    ReplyDelete