Amlima aling’ara zaidi miaka ya 1990 akiichezea Bandari Mtwara kisha Yanga.
Amlima aliyezaliwa mwaka 1967 mkoani Lindi, kwa sasa anajishughulisha na kazi ya ukocha katika timu ya vijana chini ya miaka 15 ya mkoa wa Mtwara, lakini bado anamudu kucheza soka ingawa si katika hali ya ushindani.
Kama alivyokuwa katika miaka ya 1990, Amlima wakati nazungumza naye mara nyingi anaonekana akitabasamu huku akitikisa mguu wake na kukumbuka vitu alivyowahi kufanya wakati akicheza soka.
Akicheza katika nafasi ya ushambuliaji, Amlima alimudu kucheza kama kiungo mshambuliaji kuanzia katikati na pembeni katika pande zote mbili, lakini anajivunia zaidi uwezo wa kufunga aliokuwa nao wakati wake.
SAFARI YAKE YA SOKA
Amlima alianza kucheza soka la kueleweka katika klabu ya Halmashauri ya Lindi mwaka 1985 kisha baada ya miaka minne akajiunga na timu iliyokuwa ikimilikiwa na Mamlaka ya Bandari mkoani Mtwara maarufu kama Bandari Mtwara mwaka 1989.
Amlima aliichezea Bandari hadi mwaka 1994, japokuwa kuna wakati alikuwa akiondoka na kurejea klabuni katika harakati za kuboresha maisha yake.
Wakati anajiunga na Bandari Mtwara, Amlima aliikuta timu hiyo ikiwa daraja la pili lakini kwa kushirikiana na wenzake aliweza kuipandisha hadi daraja la kwanza mwaka 1990.
Ikumbukwe kwamba, wakati huo hakukuwa na Ligi Kuu hivyo daraja la juu katika soka ilikuwa ni daraja la kwanza.
AITWA TIMU YA TAIFA KUTOKA DARAJA LA PILI
Mwaka 1990 wakati akishiriki Ligi Daraja la Pili Ngazi ya Taifa, Amlima aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa sambamba na wachezaji wengine wa timu za daraja la kwanza wakiwemo wakina Hussein Masha.
Hii inaweza kuwa historia kwa Amlima kwani tofauti na sasa ambapo kikosi cha timu ya taifa huitwa vijana ili kupata uzoefu hata kama hawana timu za ligi kuu, Amlima alijiunga na timu akitokea daraja la pili na kupata nafasi moja kwa moja.
“Nakumbuka kocha alikuwa Mzee Masour Magram na Paul West, hawa waliniamini na kunipa nafasi kikosini japokuwa mwanzo sikuamini kama ni mimi nacheza timu ya taifa,” anasema Amlima huku akicheka akionyesha kukumbuka jambo hilo.
‘ASAJILI’ TIMU TATU ZA SIMBA, YANGA NA MAJIMAJI LAKINI AKWEPA ADHABU YA FAT
Unaweza ukashangaa lakini ndiyo ukweli wenyewe, Amlima wakati aking’ara na Bandari Mtwara hasa katika ufungaji wa mabao, mwaka 1992 klabu za Simba, Yanga na Majimaji ziliona uwezo wake na kumuwania kumsajili.
Kwa kuwa Amlima alikuwa anahitaji sana fedha, alifanya makubaliano ya usajili na klabu zote hizo tatu, ambapo Simba na Yanga zote kwa pamoja zilikubali kisha zikamlipa Sh. 1,000,000 (Milioni Moja),ili zimsajili.
“Majimaji niliwaonea huruma kwa ni timu ya kutoka kwetu kusini (Songea), hivyo nikakubaliana nao wanipe Sh. 600,000 (Laki Sita) ili nijiunge nao, nikazichukua hizo fedha, halafu nikakaa kimya,” anasema Amlima.
Amlima anasema alichukua fedha hizo na kuanza kuzitumia lakini ndani ya kichwa chake alijua wazi kwamba hana mpango wa kuchezea hata timu moja katika msimu unaofuata.
“Nakumbuka nilipochukua fedha ya Simba, moja kwa moja nikaenda Kariakoo na kununua bati 60 ambazo hadi leo zinazuia nyumba yangu isiingize maji ndani na hizo nyingine za Yanga na Majimaji nikajihimarisha katika mambo mengine,” anasema Amlima.
Amlima anasema, msimu wa ligi ilipoanza, aliichezea Bandari Mtwara na kuziacha Simba, Yanga na Majimaji katika mataa na hata Chama cha Soka Tanzania (FAT), kilimuhidhinisha kucheza Bandari.
“Hata Simba, Yanga na Majimaji zilipolalamika kuhusu jambo hilo, FAT haikuwasikiliza na mimi nikachezea Bandari kama kawaida,” anasema Amlima.
USIKOSE KUSOMA SEHEMU YA PILI YA MAKALA HII ILI UJUE NI KWA VIPI AMLIMA ALIWAZIDI UJANJA SIMBA, YANGA NA MAJIMAJI
anko amlima alifanikiwa kukwepa adhabu ya fat , kwanza kipindi kile hatukuwa na chama cha soka bali kilikuwa chama cha wacheza ngoma , huo ni mtazamo wangu ngoja tumsikie mwenyewe atakavyo elendelea kusimulia
ReplyDelete