Wadhamini wa klabu ya Young Africans Sports Club kampuni ya TBL kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro leo imekabidhi vifaa kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama kombe la Kagame inayotazamiwa kuanza Juni 18 mwaka huu nchini Sudan.
Akikabidhi vifaa hivyo Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema, ‘‘ Bila ubishi Yanga na Simba ndio klabu kubwa za mpira Tanzania na zote zimefika katika fainali za mchuano wa Kombe la Kagame kwa mara ya 19 sasa, haya ni mafanikio makubwa kwa hizi timu, kama wadhamini wakuu wa timu hizi, Kilimanjaro Premium Lager inaziunga mkono Simba na Yanga katika harakati zao kucheza tena fainali za michuano hii ya kusisimua na ya kihistoria.
Aliongeza kuwa Kombe la Kagame ni mashindano makubwa Africa mashariki na kati, na ni jukwaa bora kwa wachezaji wetu kuonyesha vipaji vyao dhidi ya wachezaji wa viwango vya juu katika kanda hii lakini pia ni jukwaa zuri kwa wale wanaounda timu za taifa kuchagua wachezaji.
“Ushirikiano huu baina ya Bia ya Kilimanjaro na klabu hizi ni mizizi inayotokana na maadili katika kazi, kufanya kazi kama timu na ile kiu ya mafanikio. Na mafanikio ya ushirikiano huu ni pamoja na kushuhudia mara kwa mara timu hizi mbili zikitoa wachezaji kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) ambao wamekuwa na matokeo mazuri chini ya udhamini wa Bia ya Kilimanjaro.
Tutaendelea kusaidia timu hizi, na kuhakikisha tunapeleka mpira wa nchi hii kwenye kilele cha mafanikio.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro pia aliwataka Simba na Yanga kuhakikisha wanaiwakilisha nchi yetu vizuri katika mchuano huu mkubwa wa vilabu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kuwasihi kuchukua ushindi na kurudi na kombe la 12 la Kagame kwa mashabiki wanaosubiria kwa hamu
Akiongea
kwa niaba ya klabu ya Yanga, Katibu Mkuu Lawrence Mwalusako
aliwashukuru TBL kupitia kinywaji chake cha Kilmanjaro kwa udhamini
wanaoutoa kwa timu yake, kwani wanajivunia kuwa na wadhamini bora ambao
wanawafanya kuweza kufanya vizuri katika michezo na kuahid kuendeleza
kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.
No comments:
Post a Comment