UKATA na migogoro isiyoisha
baina ya viongozi na wanachama ndiyo ilichangia baadhi ya timu kufanya vibaya
na nyingine kushuka hadi daraja la kwanza.
Timu pekee ambazo
hazikuathiriwa na migongano kati ya viongozi na wanachama au viongozi na
wachezaji ni zile zinazomilikiwa na mashirika kama Kagera Sugar na Mtibwa
Sugar, na zinazomilikiwa na majeshi.
African Lyon, licha ya kuwa na
wadhamini pamoja na Coastal Union, Toto
African na matajiri wa udhamini Simba na Yanga zilikumbwa na migogoro
iliyoziathiri kwa namna moja au nyingine.
Yanga, pamoja na kutambia Kocha
Tom Saintfiet wa Ubelgiji, ilianza ligi kwa kutoka suluhu na Prisons na
ilipochapwa 3-0 na Mtibwa Sugar akatimuliwa akaajiriwa Mholanzi Ernie Brandts,
aliyeiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara baada ya kufikisha pointi 60.
Simba ilianza kwa shangwe,
lakini ilipotoka sare kadhaa na kuambulia vichapo, wanachama wa tawi la Mpira
Pesa wakaujia juu uongozi, baadhi ya viongozi wakaachia ngazi na kocha Mserbia
Milovan Cirkovic akafukuzwa akaajiriwa Mfaransa Patrick Liewig ambaye
alifurukuta na kuiwezesha kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45. Bila
migogoro huenda Simba ingemaliza nafasi nzuri zaidi.
Azam FC isiyo na mashabiki
wengi, ilianza msimu ikiwa chini ya Mserbia Boris Bujak 'Buka' lakini ghafla
alitimuliwa na nafasi yake ikajazwa na kocha wake za zamani Mwingereza Stewart
Hall aliyeisaidia kushika nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 54. Vilevile
timu hiyo ilivurugana na wachezaji watatu ikidai wamepokea rushwa.
Kwa tathmini, timu hizo zenye
ukwasi wa fedha ndizo kwa mara nyingine zimeshika nafasi tatu za kwanza. Msimu
uliopita Simba ilikuwa bingwa ikafuatiwa na Azam na Yanga.
Wakati Simba na Yanga zilikuwa
na uwezo wa kutimua makocha na kuajiri wengine, Toto African ya Mwanza ilikosa
uwezo huo ikabaki ikipigania kutoshuka daraja. Ukata ulipoielemea Toto ilibaki
ikilalamikia ugumu wa ratiba na waamuzi hadi imeshuka daraja la kwanza.
African Lyon ilianza ligi ikiwa
na mikakati ya kujinasua kwenye ukata lakini ilikwama. Kwanza
kampuni ya Zantel iliyotaka kuidhamini iliwekewa kauzibe na pili kocha
Muarentina Pablo Ignacio Velez aliyeajiriwa kuiboresha kikosi alitupiwa virago.
Timu ikabaki chini ya msaidizi
wake Jacob Otieno naye aliposhindwa ikaachwa kwenye mikono isiyo salama ya
Salum Bausi aliyeshuka nayo. Coastal Union chini ya Hemed Morocco ilianza
vizuri na hata kutamba kuwania nafasi tatu za juu, lakini imeishia nafasi ya
sita huku mchezaji wake Nsa Job akikabiliwa na tuhuma za kupokea mlungula
kutoka moja ya klabu kubwa.
Timu ndugu za Kagera Sugar na
Mtibwa Sugar, zote zikimilikiwa na kampuni ya Super Doll, zimejitokeza kuwa
kiboko cha vigogo baada ya kutoa vichapo kwa nyakati tofauti. Kagera chini ya
Abdallah Kibadeni ilishika nafasi ya nne ilhali Mtibwa chini ya Mecky Mexime
iliishia nafasi ya tano.
Kagera Sugar na Mtibwa Sugar
hazina ukata lakini pia hazina mafungu makubwa kwa ajili ya kufanya usajili wa
wachezaji ghali wanaoweza kuzisaidia kutwaa taji la Ligi Kuu.
Katika kipindi chote cha ligi,
hayakusikika malalamiko wala manung’uniko ya hali ya kambi kutoka timu za Jeshi
la Kujenga Taifa kama Ruvu Shooting, Oljoro
JKT, Mgambo na JKT Ruvu.
Aidha, hayakusikika malalamiko
kutoka Prisons iliyo chini ya Jeshi la Magereza wala Polisi Moro iliyo chini ya
Jeshi la Polisi hadi imeshuka daraja.
Hata hivyo, ushiriki wa
kusuasua na uwezo mdogo wa kusajili wachezaji wenye majina makubwa umeziathiri.
Kisheria, timu hizo hazipaswi kusajili wachezaji nyota kutoka nje ya nchi.
Timu hizo, ambazo kwa muundo ni
kwa ajili ya kutoa burudani kwenye majeshi, zimekuwa zikitoa mchango mkubwa
katika Ligi Kuu japokuwa kwa ushindani wa wastani tu. Ni mara chache sana
zimekuwa na uwezo wa kuzifunga timu kubwa za Simba, Yanga na Azam ila humudu
kutoa sare.
Mara nyingi ushindani fulani
huonekana zinapokutana zenyewe. Wakati fulani zimekuwa na matokeo mazuri kwenye
viwanja vya nyumbani na nyingine kama Mgambo imeponea chupuchupu.
Polisi Moro, Toto na African
Lyon zimeshuka daraja na kwa utaratibu zimepisha nafasi kwa Ashanti United ya
Ilala, Mbeya City na Rhino ya Tabora zilizopanda daraja. Nazo zisipokuwa na
mafungu ya kusajili wenye uwezo au zikiendekeza migogoro kwa muda mrefu
zitajikuta zikirejea daraja la kwanza.
MAKALA HII IMETOLEWA KATIKA
GAZETI LA MAWIO, IMEANDKWA NA ELIUS KAMBILI
No comments:
Post a Comment