GUMZO lililotawala medani ya soka nchini ni pambano la funga
dimba ya Ligi Kuu ya Bara litakalowakutanisha watani wa jadi Simba na Yanga Jumamosi
ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Mechi hiyo itafanyika huku Yanga ikiwa tayari imeshatwaa
ubingwa wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 57 ambazo haziwezi kufikiwa na
timu nyingine yoyote inayoshiriki michuano hiyo. Mchezo huu utakuwa wa kulinda
heshima tu kwani Simba haiwezi hata kutwaa nafasi ya pili.
Mashabiki wa Yanga wamejiaminisha kwamba mechi hiyo itakuwa
ya kulipa kisasi cha kipigo cha mabao 5-0 ambacho ilikipata katika mechi ya
mwisho msimu uliopita. Yanga wanajipa imani hiyo kutokana na mzozo ‘ulioko’
ndani ya Simba.
Siku chache baada ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi
hii, Simba haikuwa ikipata matokeo ya kuridhisha kiasi cha kutafuta mchawi.
Uongozi ukawasimamisha wachezaji wake kadhaa kwa madai ya kuhujumu timu.
Wachezaji waliosimamishwa ni Haruna Moshi ‘Boban’, Felix
Sunzu, Amir Maftah, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Paul Ngalema, Ramadhan Chombo
‘Redondo’ na Abdallah Juma. Lakini baadaye Kazimoto na Sunzu walisamehewa na
kurejeshwa kundini.
Baada ya kuwasimamisha wachezaji hao ikaanza kuwatumia
vijana kama Haruna Chanongo, Christopher Edward, Abdallah Seseme, Ramadhan
Singano ‘Messi’, William Lucian, Miraji Adam, Hassan Khatib na Jonas Mkude.
TAZAMA KINACHOITWA KIKOSI CHA WATOTO
Hivyo kikosi cha sasa cha Simba mara nyingi hujumuisha
wachezaji; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Haruna Shamte, Shomari Kapombe,
Mussa Mudde, Amri Kiemba, Mrisho Ngassa, Messi, Felix Sunzu, Mkude na Haruna
Chanongo.
Mashabiki wa Yanga wanabeza wanakiita kikosi hicho cha
watoto, hivyo wanajipa imani timu yao inaweza
kuinuka na ushindi wa mabao mengi wakiwa na ndoto ya kurudisha mabao 5-0
waliyofungwa katika mechi kama hii mwaka jana.
Uchambuzi unaonyesha Simba haina watoto. Katika kikosi hicho
kinachoitwa cha watoto, unaweza kuona wachezaji watatu tu chipukizi au wasio na
majina makubwa ambao ni Messi, Mkude na Chanongo.
Wachezaji wanane waliobaki ambao ni Kaseja, Chollo, Shamte,
Kapombe, Mudde, Kiemba, Ngassa na Sunzu, wote ni wazoefu na wanaoweza kubadili
matokeo wakati wowote ule. Mbali ya wachezaji hao, Simba ina Kazimoto ambaye
yuko kikosini japokuwa tangu arudishwe amecheza mechi chache.
Hata hao chipukizi watatu ambao kuna uwezekano mkubwa
wakawepo kikosi cha kwanza cha Simba, ni
wazoefu kwani wapo katika kikosi hicho kwa msimu wa pili sasa. Kikosi hicho
kinaweza kutoka sare na Yanga au hata kushinda.
Wachezaji wanaoweza kuihofia Yanga ni chipukizi ambao msimu
huu wanaichezea kikosi cha kwanza cha Simba kwa mara ya kwanza wakiwemo Lucian,
Miraji na Khatib ambao hata hivyo kuna uhakika mdogo mno wa wao kuwemo kikosi
cha kwanza.
YANGA WAKIJIAMINI, WAMEISHA
Wakati Yanga wataingia uwanjani wakijiamini, Simba kwa
upande wao wataingia dimbani kufanya mambo mawili; kwanza kuthibitisha uwezo
wao, pili kuwatibulia Yanga ili washerehekee kukabidhiwa kombe na kichapo juu.
Tatizo kubwa la kikosi cha Simba kwa sasa linaweza kuwa ni
saikolojia kwa wachezaji baada ya kukosa hata nafasi ya tatu; pia kutoelewana
miongoni mwao. Hata kufanya vibaya kwa Simba katika mechi za kwanza za mzunguko
huu, kulisababishwa zaidi na uongozi.
Simba ilifanya vibaya katika mechi zake za Kanda ya Ziwa,
kwani ilikubali kipigo cha bao 1-0 na Kagera Sugar kisha ikatoka sare ya mabao 2-2 na Toto African ya
Mwanza. Huo ulikuwa wakati ambao baadhi ya wanachama wa timu hiyo walikuwa
wakipambana kumtoa madarakani Mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage.
Katika mzozo huo Makamu mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’
akajiuzulu. Mwingine aliyejiuzulu ni mjumbe wa kamati ya utendaji na mwenyekiti
wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope, lakini sasa amerudi kundini.
Ghafla ‘watoto’ wa Simba chini ya Mfaransa, Patrick Liewig
wakaanza kutoa darasa, wakailambisha JKT Mgambo 3-1, huku Yanga ikitoka sare na
Coastal Union katika mchezo wake wa mwisho kabla ya kuivaa Simba keshokutwa.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts na benchi lote la ufundi la
Yanga, wanapaswa kutoruhusu mawazo ya mashabiki na baadhi ya viongozi
wanaoibeza Simba.
MAKALA HII IMECHOTWA KATIKA GAZETI LA MAWIO IMEANDIKWA NA
ELIUS KAMBILI
No comments:
Post a Comment