Search This Blog

Thursday, May 9, 2013

MADUDU YA KAMATI YA MASHINDANO KWA LIGI ZA MIKOA, JINA LA TIMU BINGWA LATUMWA KABLA YA LIGI KUISHA


Ramadhani Nassib ( kushoto )- Mwenyekiti wa kamati ya Mashindano

MAPEMA wiki hii Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitoa ratiba ya mechi za mabingwa soka wa mikoa ya kisoka watakaopambana kupata timu tatu zitakazofuzu kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu huu.
Hakika hatua hii ya TFF kupitia Kamati ya Ligi imeweza kwenda na wakati kwa mujibu wa mipangilio yao, lakini nyuma ya jambo hili kuna mambo kadhaa yaliyotendeka na kulitia doa shirikisho la soka nchini.
Hadi ratiba inapangwa kuna baadhi ya mikoa ambayo haikuwa imepata mabingwa kutokana na sababu kadhaa ambazo kwa kiasi fulani ndizo zinazoendelea kuua mpira wa miguu nchini japokuwa zinaonekana ndogo ndogo.
Kwa mujibu wa TFF, uharaka wa kupangwa kwa ratiba hii umekuja baada ya Kamati ya Mashindano ya TFF chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, kubainia kwamba ucheleweshwaji wake unaweza kuathiri usajili wa timu zitakazopanda kucheza ligi daraja la kwanza.
Kutokana na uharaka huo, baadhi ya mikoa ilishindwa kuwasilisha majina ya mabingwa wake hadi Jumapili iliyopita ya Mei 5 nayo ni; Dodoma, Geita, iringa, Lindi, Mtwara, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Tanga.
Mikoa hiyo ilishindwa kupata mabingwa wake kwa wakati kutokana na mambo yafuatayo;


UCHELEWESHWAJI WA KANUNI ZA LIGI

Vyama vingi vya mikao ya soka vilichelewa kupata kanuni za ligi za mikoa hivyo kushindwa kuendesha michuano hiyo kwa wakati.

Muhusika hapa ni Kamati ya Mashindano ya TFF ambayo leo hii imelazimisha kwa mikoa kumaliza ligi zao mapema wakati yenyewe ilichelewesha kanuni za michuano hiyo. Sasa mikoa bila ya kuwa na kanuni, ingeendeshaje ligi? Hili ni tatizo.

Endapo mikoa ingepata kanuni za ligi mapema, nayo ingeanzisha ligi zao mapema na leo zingepata wawakilishi wanaofaa.

HALI YA KIJIOGRAFIA

Wilaya za Dar es Salaam za Ilala, Kinondoni na Temeke zote (hizo zina majina ya Dar es Salaam 1, Dar es Salaam 2 na Dar es Salaam 3) zinahesabika kama mikoa ya soka kama ilivyo, Tabora, Lindi, Mtwara na Simiyu; uendeshaji wa ligi za mikoa hiyo lazima uwe tofauti.

Kwa mfano timu ya mkoa wa Dar es Salaam 1, inaweza kucheza mechi yake leo kwenye Uwanja wa Mwalimu Nyerere pale Magomeni halafu keshokutwa ikacheza Uwanja wa Tandika Mabatini na isiathirike, kutokana na hali nzuri ya miundo mbinu ya kuiwezesha timu kufika uwanjani.

Ukichukulia mkoa kama Tabora, ambao una wilaya za Irambo, Igunga, Sikonge na Nzega; hali ni tofauti kwani kutoka wilaya moja hadi nyingine ni safari kubwa tena inayoweza kuchukua hata siku moja nzima.

Hii ina maana kwamba, Dar es Salaam 1 haiwezi kumaliza ligi sawa na Tabora. Hali ni hivyo hivyo hata kwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Shinyanga na Simiyu.





Blassy Kiondo -Makamu Mwenyekiti


UKATA, UHABA WA VIWANJA
Ukitoa Dar es Salaam ambapo viwanja vingi vina uzio unaoweza kutumiwa kuingiza mashabiki kwa kulipa viingilio na kuvifanya vyama husika kuendesha ligi kikamilifu.

Katika baadhi ya mikoa ikiwemo Simiyu, viwanja vyenye hadhi ya kuchezewa ligi hiyo ni vichache ambavyo pia vingi havitoi fursa ya kuingiza kipato kutokana na ukweli kwamba hvina uzio.

Matokeo yake, mechi nyingi zinachezwa katika kiwanja kimoja na mzunguko wa ligi kuwa mkubwa ukichangiwa na umbali kutoka ilipo timu moja na nyingine.

Ukitoa mipira 20 kutoka TFF, vyama vingi vya soka vya mikoa vinajiendesha ‘kimaghumashi’ kutokana na kutokuwa na chanzo cha maana cha mapato.

Tunapozungumzia ukata tunaweza kutumia mfano wa timu ya Small Kids ya Rukwa iliyoshushwa daraja kutoka daraja la kwanza baada ya kushindwa kutokea uwanjani kutokana na ukata. Iwapo timu ya daraja la kwanza inakabiriwa na ukata, hali itakuwaje kwa timu ya daraja la nne?



Matokeo yake;

MECHI ZACHEZWA ASUBUHI NA JIONIKuna taarifa kwamba, baadhi ya mikoa mabingwa wake walipangwa kutokana na maelekezo ya baadhi ya viongozi wa kamati ya mashindano na TFF kwa ujumla huku ligi zikiwa zinaendelea.

Baadhi ya mikoa ililazimika kucheza mechi asubuhi na jioni ili tu kupata bingwa, tena kwa njia zisizo halali lengo likiwa kuwafurahisha viongozi wa kamati waliotaka majina ya timu katika tarehe waliyotaka wao.

MAJINA YA MABINGWA YALITUMWA KABLA YA TIMU KUTWAA UBINGWA
Mbaya zaidi viongozi wa mikoa walilazimishwa kutuma jina la bingwa huku mechi zikiendelea hivyo kulazimika kupanga matokeo ili wasije kuumbuka mwisho wa siku.

Hakika viongozi wengi wa vyama vya soka vya mikoa walikuwa katika hali ngumu kwani wapo ambao usalama wao waliuweka shakani hasa kutokana na kulazimisha timu ambayo jina lake limetumwa Dar es Salaam kama bingwa, kuhakikisha inashinda.

Wapo baadhi ya viongozi ambao tayari wameshajiwekea doa katika utawala wao kwa kujikuta wakishiriki mchezo huu wa kutuma majina kabla ya bingwa kupatikana.

Mbaya zaidi hata waamuzi wa baadhi ya mechi walikuwa wanakwenda katika vituo vya mechi hizo za ligi za mikoa kwa maelekezo ya kamati ya mashindano bila ya kamati hiyo kuwasiliana na vyama vya mikoa.



KITAKACHOENDELEA….Timu za mikoa ya Dar es Salaam zitaendelea kufanya vizuri na hata mikoa mingine inaona kilichopo ni kampeni ya wazi kwa TFF na Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kuhakikisha mkoa huo unapata tmu nyingi za ligi kuu, ili kujiingizia kipato kwa njia ya fedha za milangoni.

TFF inatambua fika kwamba timu za Dar es Salaam ndizo zinazoiingizia kiasi kikubwa cha fedha za milangoni katika mechi zake, lakini kuna jambo ambalo wanalifanya kimakosa lakini hawajui.

Mechi za timu ya taifa, Taifa Stars nazo zikichezwa bado DRFA inanufaika peke yake kama chama cha mkoa. Hii si halali. Taifa Stars ni timu ya taifa, hivyo pato linalokwenda DRFA lilipaswa kupelekwa kwa mgawanyo kwa mikoa yote.

Kwa mfumo wa sasa, DRFA itakuwa na uwezo wa kuingiza timu nyingi katika Ligi Daraja la Kwanza kila mara kwani hata kama zikikwama kama chama kinaweza kuokoa jahazi tofauti na mikoa mingine.

MSIMAMO WETU;
Kamati ya Mashindano inaweza kuchukua jambo hili kama changamoto na kulifanyia kazi. Nia yetu ni kuona soka la Tanzania linapiga hatua.

No comments:

Post a Comment