Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig ametamka kuwa silaha yake kubwa kwenye mchezo wa Yanga ni kasi ya wachezaji
wake, ingawa amekiri wanatakiwa kuwa makini kwa dakika zote 90 za mchezo.
Mfaransa huyo alisema jijini Dar es Salaam kuwa tayari wamepoteza ubingwa wa ligi pamoja na nafasi ya pili ambayo
ingeweza kuifanya timu hiyo ishiriki Kombe la CAF mwakani.
"Hatuna nafasi tena ya kushinda taji la ligi kwa msimu huu wala kumaliza katika nafasi ya pili ambayo ingetupa fursa ya kushiriki Kombe la CAF mwakani.
"Kilichobaki ni kulinda heshima yetu kwa kuwafunga mabingwa (Yanga) katika mchezo wetu wa mwisho hiyo Mei 18. Timu yangu ya Simba ina wachezaji wengi vijana ambao wana kasi kubwa kuwazidi Yanga." alisema kocha huyo aliyerithi mikoba ya Mserbia Milovan Cirkovic aliyetupiwa virago na klabu hiyo mwaka jana.
Kocha huyo aliongeza; "Yanga ni timu nzuri hakuna mtu anayepinga hilo, lakini haiwezi kumudu kasi ya wachezaji
wangu vijana.
"Nimewaona katika mechi kadhaa za ligi, wanacheza vizuri ingawa sitaki kuamini kwamba watashinda mbele ya vijana wangu imara."
Liewig alisema katika kambi ya kujiwinda na mchezo huo ataongeza muda wa programu yake ya mazoezi kuhakikisha kikosi chake kinakuwa katika hali nzuri ya ufiti kabla ya kukutana na watani hao wa jadi katika soka la Tanzania Bara na kuharibu sherehe za ubingwa huo.
No comments:
Post a Comment