Kamati
ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana
Mei 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam kupokea na kupanga utekelezaji wa
maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuhusu
uchaguzi wa shirikisho.
Kikao
hicho cha dharura chini ya Uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga
kitakuwa na ajenda hiyo moja tu katika kuhakikisha utekelezaji wa
maelekezo ya FIFA unafanyika haraka ili uchaguzi ufanyike ndani ya muda
uliopangwa.
FIFA
katika maelekezo yake imetaka kwanza ziundwe Kamati ya Maadili na
Kamati ya Rufani ya Maadili kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi
wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF. FIFA imeagiza uchaguzi uwe
umefanyika kabla ya Oktoba 30 mwaka huu.
KILA LA KHERI AZAM KOMBE LA SHIRIKISHO
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam
katika mechi yake ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika
itakayochezwa Morocco kesho (Mei 4 mwaka huu).
Mechi
hiyo ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano hiyo itachezwa jijini
Rabat kuanzia saa 11 jioni kwa saa za Morocco. Timu hizo zilitoka suluhu
katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili
zilizopita.
Azam
iko nchini Morocco kwa karibu wiki nzima sasa ikijiandaa kwa mechi hiyo
chini ya Kocha wake Stewart John Hall. Msafara wa Azam nchini humo
unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Eliud Mvella.
25 WARIPOTI KAMBINI YOUNG TAIFA STARS
Wachezaji
25 kati ya 30 walioitwa na Kocha Kim Poulsen kwenye kikosi cha pili cha
Taifa Stars (Young Taifa Stars) wameripoti kambini ambapo mazoezi
yalianza tangu jana jioni (Mei 2 mwaka huu).
Kocha
Kim amewaitaka wachezaji katika kambi hiyo ya siku tano ili kuangalia
uwezo wao katika maeneo kadhaa kwa lengo la kupata baadhi ambao anaweza
kuwajumuisha kwenye kikosi cha Taifa Stars siku za usoni.
Wachezaji
watano walioshindwa kujiunga katika kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli
ya Sapphire jijini Dar es Salaam ni Aishi Manula, David Mwantika, Himid
Mao, Samih Nuhu na Seif Abdallah ambao wako Morocco na timu yao ya Azam.
KAMATI YA MASHINDANO KUPITIA MAANDALIZI RCL
Kamati
ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana
Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kupitia maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa
Mikoa (RCL) iliyopangwa kuanza Mei 12 mwaka huu.
Tayari
mikoa 18 kati ya 27 kimpira imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya RCL
itakayotoa timu tatu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) msimu ujao (2013/2014).
Kamati
hiyo chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati
ya Utendaji ya TFF itapokea taarifa ya maandalizi ya ligi hiyo kutoka
Idara ya Mashindano ya TFF na kufanya uamuzi juu ya mikoa ambayo
haijawasilisha mabingwa wao.
Ligi
hiyo itachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, na ratiba (draw)
itapangwa wakati wowote. Ada ya kushiriki ligi hiyo kwa kila klabu ni
sh. 100,000 na usajili utakaotumika na ule ule wa ligi ngazi ya mkoa.
Hakutakuwa na usajili mpya wa wachezaji.
No comments:
Post a Comment