Search This Blog

Thursday, May 16, 2013

HARUNA CHANONGO WA SIMBA, ZAHORO PAZI WAITWA TIMU YA TAIFA VS MOROCCO

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen leo (Mei 16 mwaka huu) ametaja kikosi cha wachezaji 26 watakaoingia kambini kujiwinda kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech, Morocco.

Katika kikosi hicho, Kim ameita wachezaji wapya sita ingawa baadhi yao wamewahi kuchezea timu hiyo, huku akiacha wengine watatu aliokuwa nao kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Morocco ambapo Taifa Stars ilishinda mabao 3-1.

Wapya aliowaita katika kikosi hicho kitakachoingia kambini Mei 20 mwaka huu, saa 1 jioni kwenye hoteli ya Tansoma jijini Dar es Salaam ni Ally Mustafa, Vicent Barnabas, Juma Luzio, Haruna Chanongo, Mudhathiri Yahya na Zahoro Pazi. Wachezaji aliowaacha ni Shabani Nditi, Nassoro Masoud Cholo na Issa Rashid.

Kikosi kamili cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ambacho kabla ya kwenda Morocco kitapita jijini Addis Ababa, Ethiopia kucheza mechi ya kirafiki Juni 2 mwaka huu dhidi ya Sudan ni kama ifuatavyo;

Makipa ni nahodha Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar) na Waziri Salum (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mudathiri Yahya (Azam) na Salum Abubakar (Azam).

Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).

Kocha Kim amesema kikosi kitakachoingia kambini kitakuwa na wachezaji 24 ambapo Samata na Ulimwengu watajiunga na timu jijini Marrakech, lakini wachezaji atakaondoka nao Dar es Salaam kwenda Addis Ababa ni 22 ambapo ataacha kipa mmoja na mchezaji mmoja wa ndani.

Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa Stars mechi ya kirafiki Juni 1 mwaka huu dhidi ya Algeria, Libya au Misri. Lakini baadaye Algeria ikasema itacheza na Togo, wakati Misri ilitaka mechi hiyo ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo ambalo lisingewezekana kwa Stars kwani ina mechi ya mashindano Juni 8 mwaka huu.

Kwa upande wa Libya mechi hiyo ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni 2 mwaka huu. Lakini baadaye Libya ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli ambapo TFF ilikataa kutokana na sababu za kiusalama.

No comments:

Post a Comment