CHAMA Cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimezizawadia timu zake tatu za Red Coast,
Abajalo na Friends Rangers zilizofanikiwa kucheza Ligi ya Mabingwa inayotarajiwa
kuanza Mei 12 mwaka huu.
Makabidhiano
hayo yalifanyika jana Alhmaisi (Mei 9) jioni kwenye ofisi za chama hicho,
zilizopo makutano ya mtaa wa Mafia na Bonde, ambapo Red Coast waliokuwa
washindi wa kwanza walikabidhiwa Sh 700, 000, huku Abajalo wao wakizawadiwa Sh
600, 000 na Friends Rangers wakijipatia Sh 500, 000.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Almas Kassongo (kushoto), akimkabidhi Mwenyekiti wa Red Coast, Jumanne Ayubu Sh 700, 000 ikiwa ni mchango wa chama hicho kusaidia timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa inayotarajiwa kuanza Mei 12 mwaka huu |
Kwa mujibu
wa Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, lengo la timu hizo kukabidhiwa fedha
hizo ni kuzihamasisha ili ziweze kujiandaa na hatimaye kufuzu kucheza Ligi
Daraja la Kwanza msimu ujao.
Mwenyekiti
wa DRFA, Almas Kassongo, ndiye alikabidhi fedha hizo kwa wawakilishi wa timu
hizo huku akisema licha ya kiasi hicho cha fedha kuwa kidogo, lakini itakuwa
chachu ya kupata mafanikio.
Viongozi
waliohudhuria makabidhiano hayo kutoka DRFA ni Mkurugenzi wa Ufundi, Joseph Kanakamfumo,
Afisa Tawala, Said Pambalelo, Mjumbe wa
Kamati ya Ufundi na Mashindano, Daudi Kanuti na Mweka Hazina Ally Hassani.
Wawakilishi
wa timu ni Mwenyekiti wa Red Coast, Jumanne Ayubu, Meneja wa Friends Rangers,
Shaaban Marsila na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Abajalo, Abbasi Ngau.
Wakati huo
huo, kamati ya ufundi ya DRFA kesho Jumamosi Harbours Club Kurasini, itakutana
na Viongozi wa soka la Wanawake (TWFA), Viongozi wa soka la Vijana na Kamati ya
Waamuzi ili kupanga utaratibu wa ligi na pia kuandaa kozi ya makocha.
No comments:
Post a Comment