Search This Blog

Tuesday, April 23, 2013

FALSAFA YA SOKA LA KIDACHI TARATIBU YAANZA KUONEKANA MITAA YA JANGWANI……

YANGA imeifunga JKT Ruvu mabao 3-0 katika mchezo namba 106 wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mchezo huo, mashabiki wa Yanga walifurahia matokeo hayo kutokana na ukweli kwamba, timu hiyo yenye pointi 56 inahitaji pointi moja tu iweze kutangaza ubingwa kwani timu inayoifuata ambayo ni Azam FC ina pointi 47.

Azam imebakisha mechi tatu na ikishinda zote itakuwa imefikisha pointi 56 ambazo Yanga inazo sasa. Yanga imebakisha mechi mbili tu dhidi ya Coastal Union na Simba. Hivyo sare tu inatosha kuipa Yanga ubingwa msimu huu. Wakati mashabiki na wanachama wa Yanga wakifurahia timu yao kuelekea kutwaa ubingwa, kuna kitu kilikuwa kimetokea katika mechi za jana dhidi ya JKT Ruvu, nacho ni soka la kuvutia ambalo kitaalam tunaweza kuita ni TOTAL FOOTBAL lililokuwa likichezwa na Yanga.


FALSAFA YA SOKA LA KIDACHI ILIIUA JKT
Katika mchezo wa jana, Yanga ilicheza ‘total football’ katika muda mwingi wa mchezo huo kiasi cha kuichanganya JKT Ruvu ambayo angalau kipindi cha kwanza iliweza kuizuia Yanga.

Tangu alipowasili katika klabu ya Yanga akitokea APR ya Rwanda, Kocha Ernie Brandts amekuwa akitilia mkazo ufundishaji wa soka la Kiholanzi, nchi anakotokea.

Ndani ya total football, kila mchezaji anawajibika ipasavyo na wachezaji wote wanacheza mahala popote ili mradi lengo la timu litimie. Kwa muda mrefu total football imekuwa ikitumiwa na Uholanzi na kuvitetemesha vigogo vya soka.

Tunaposema kila mchezaji anacheza namba yoyote mbali ya ile aliyokabidhiwa kucheza siyo kwa kujichezea tu, bali mchezaji anapaswa kuwajibika ipasavyo kuweza kutimiza lengo la timu.

Mchezaji anapokuwa katika mfumo wa total football ni lazima awe na vitu vifuatavyo, KWANZA awe na skills yaani uwezo wa kuwa na mbinu za kumuwezesha kuufanya mchezo uendelee katika mazingira yoyote yale.

Hapa unaweza kuona jinsi viungo Athuman Idd Chuji, Haruna Niyonzima na Frank Domayo walivyokuwa wanaweza kuwa na mbinu mbalimbali za kuendesha mpira bila ya matatizo.

Tazama bao la tatu lililofungwa na Nizar Khalfan, mpira ulianzia kwa Kelvin Yondani kisha kwa Niyonzima nyuma kabisa ya lango la Yanga, lakini kiungo huyo aliyekuwa anacheza kama winga wa kushoto, aliweza kurudi nyuma kabisa kufuata mpira kisha akaanzisha shambulizi lililozaa bao bora tena yeye akiwa ndiye ametoa pasi ya mwisho.

Kitu cha PILI katika total football ni pasi, lazima timu icheze kwa pasi kuanzia nyuma kwa mabeki hadi kwa washambuliaji wake. Hata Barcelona wanacheza hivyo na ndiyo maana leo hii wanasifika kwa mchezo huo.

Katika bao la tatu pasi ilianzia kwa beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani ambaye alipeleka mpira kwa Niyonzima, naye akaondoka na mpira kwa kutumia mbinu za kawaida kabisa akacheza pasi ‘one-two’ na Domayo, kisha Twite na Msuva na kufanya hivyo hadi alipofika katika lango la JKT Ruvu kwa Niyonzima tena kisha Domayo akapiga shuti lililogonga nguzo ya goli kisha Nizar akafunga bao.

Kitu cha TATU katika total football ni jinsi timu inavyotembea kwenda mbele. Vitu vyote vitatu lazima vifanye kazi ili mfumo huu uweze kuleta faida katika timu.

Yanga ilicheza kwa kutumia mbinu, kisha pasi zikapigwa na mwisho move ilikuwepo kwa timu nzima ndiyo maana mpira uliweza kuanza golini kwao na ukafika kwa JKT Ruvu bila shaka yoyote.

Tukirudi katika mfano wetu wa bao la tatu, utaona jinsi Niyonzima alivyokuwa aki-move na mpira huku akiuweka vituo kwa Domayo na Chuji ambao nao walikuwa wakienda naye sawa kwa kumfuata hadi katika lango la JKT Ruvu na kufunga bao.

Timu ilionekana ‘imeiva’ katika kutekeleza mfumo huu wa total football kiasi cha kuichachafya ngome ya JKT Ruvu itakavyo na kuweza kupata mabao matatu muhimu kwao
.
    Erns Brandts akimpa maelekezo kiungo Frank Domayo...

RINUS MICHELS NDIYE ALIYEMPA FALSAFA HII BRANDTS?
Katika soka la Kidachi,Total Football ndiyo inayotamba na ndiyo maana siku zote timu ya taifa ya Uholanzi inaonekana ni moto wa kuotea mbali.

Rinus Michels mwasisi wa TF na ndiye aliyeeneza hii falsafa nchini mwake Uholanzi pamoja na nchi ya Hispania alipokwenda kwenye Klabu ya Fc Barcelona na kuiongoza kushinda taji la ligi ya nchi hiyo mnamo mwaka 1974.

Rinus Michels alimrithisha Johan Cruyff ambaye aliuendeleza kwenye vilabu vya Ajax na Barcelona akiwa kama kocha,

Falsafa hii ndo imekuwa siri kubwa ya mafanikio ya FC Barcelona tunayoishuhudia leo hii ikitandaza soka la hali ya juu.

http://thefootballasylum.com/wp-content/uploads/2011/08/t02_nl_jubel_michels_1988_enpropertyoriginal.jpg
Rinus Michels akiwa na kombe la mataifa ya Ulaya mnamo mwaka 1988

Tukumbuke ya kwamba, katika fainali za Kombe la Dunia za 1978, Brandts alikuwepo katika kikosi cha Uholanzi chini ya kocha mwingine nguli Ernst Happel kilichocheza fainali hizo huko Argentina. Kikosi cha Ernst Happel kilifika fainali na kufungwa na wenyeji Argentina mabao 2-1,Ndani ya kikosi hicho kulikuwa na wachezaji zaidi ya wanane waliokuwepo kwenye kikosi kilichoundwa na Rinus Michels mwaka 1974 na kufungwa kwenye mchezo wa fainali na mwenyeji iliyokuwa Ujerumani Magharibi, mfano majina kama mapacha Willy van de Kerkhof na René van de Kerkhof,Johan Neskeens,Ruud Krol, Rob Rensenbrink, Arie Haan hao ni baadhi ya majina yaliyokutana na Ernst Brandts kwenye kikosi cha Uholanzi cha mwaka 1978 kilichoendeleza falsafa ya Rinus Michels,

Namnukuu Rinus Michels mnamo mwaka 1988 alipoiongoza Uholanzi kutwaa kombe la mataifa ya ulaya ‘’ nimekirithisha FALSAFA yangu kizazi cha kati ya 1965-1980, hata kama sitakuwepo duniani siku moja naamini kitalisambaza neno langu kwa vizazi vijavyo ‘’

Miongoni mwa vizazi hivyo yumo Ernst Brandts ambaye naamini ameileta FALSAFA ya nguli Rinus Michels nchini Tanzania kupitia mitaa ya Jangwani.

Wakati Cruyff akiipeleka FALSAFA hiyo huko Catalunya kwenye klabu ya FC Barcelona ambayo hata akija kocha gani, bado mfumo huo utaendelea kutumika.

Gwiji huyo wa Uholanzi alipandikiza total football kwa wachezaji chipukizi waliokuwa wakijifunza soka katika kituo cha michezo cha La Masia ambako Lionel Messi na wenzake kibao wa kikosi cha kwanza cha Barcelona wapo.

Ni wazi kwamba, mafaniko ya total football kwa Cruyff ndiyo yaliyomsukuma Brandts kutumia mfumo huo katika Yanga na leo hii Yanga inafaidika na hali hiyo
.
    Johan Cruyff ...Ndiye siri ya mafanikio ya FC Barcelona ya leo...

YANGA KIWANGO KIMEPANDA, BRANDTS AMEFANIKIWA
Kwa soka lililochezwa katika mechi ya jana, ni wazi  kiwango kimeongezeka na pia Brandts amefanikiwa kuingiza falsafa ya mpira wa kidachi ndani ya kikosi cha Yanga.

Tazama siku hizi uchezaji wa Cannavaro, si yule aliyekuwa akiokoa kwa kubutua mpira juu au bora liende mbele kwa kuutoa katika lango lake.

Cannavaro sasa anaweza kuanziwa mpira, akatulia, akapiga pasi kisha akapanda na move, hivyo siku hizi anaisadia timu kwa kiasi kikubwa ndiyo maana anafunga hata mabao muhimu kwa timu yake.

Katika mechi ya jana, kuna muda Yanga ilipata faulo jirani na lango la JKT Ruvu, Cannavaro alienda kucheza faulo ile na ilibaki kidogo afunge kwa kichwa mpira wa adhabu hiyo uliopigwa na Domayo.

Sasa Cannavaro anajua mpira unaokuja auzuie vipi na hata kukaa kwenye maeneo husika kwenye muda muafaka (Positioning) na hata apige vipi mpira ili uweze kufika kwa mlengwa, hata namna ya kufunga kwa kutulia pia anajua. Cannavaro ana mabao matano katika Ligi Kuu ya Bara kama ilivyo kwa straika wa Simba, Felix Sunzu.

Hata beki mwingine wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani naye kiwango kimeongezeka chini ya Brandts na sasa ameongeza ufanisi zaidi (Focus) katika kumiliki mpira na kuanzisha mashambulizi.

2 comments:

  1. Yeah total football inaanza kuonekana, ukiangalia game mbiliza jkt oljoro na ruvu falsafa hiyo ilionekana kwani magoli yalifungwa kwa movement na timu ilikua ina move kwa mpango unaonekana, na katika game ya ruvu jkt Yondan alikua anapanda kiasi kuna baadhi ya move zinapoishia akawa anaonekana kama mshambuliaji pale move inapoishia.

    CHALLENGE; je yanga watamvumilia huyu kocha??? maana uvumilivu hua ni mdogo kwa vilabu vyetu kwa kutaka mafanikio ya haraka.....

    ReplyDelete