Search This Blog
Friday, March 15, 2013
MADUDU YA LIGI KUU, MECHI ZINAONYESHWA LIVE TIMU HAZILIPWI. CHAMAZI INAONGOZA KWA DHULUMA
LIGI Kuu ya soka ya Tanzania Bara inaendelea wikiendi hii katika viwanja tofauti tofauti, lakini kuna jambo moja linalokwenda ndivyo sivyo. Matangazo ya haki za televisheni ya ‘live’ yanayoendelea hayaendi inavyotakiwa.
Kama utagundua, mechi kadhaa za Azam FC zimekuwa zikionyeshwa ‘live’ kwenye Uwanja wa Chamazi bila kuzingatia baadhi ya mambo muhimu ikiwemo timu pinzani kulipwa haki za matangazo hayo bila kuzingatia uenyeji kama ilivyo kawaida.
Kwa muda mrefu klabu za Simba na Yanga zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mechi zake hazirushwi ‘live’ bila kuwepo makubaliano maalum kutoka kwa chombo husika au kampuni yoyote inayotaka kufanya hivyo.
Sasa hali ni toifauti kwani mechi za Azam zinaonyeshwa live kutoka Uwanja wa Chamazi unaomilikiwa na timu hiyo iliyo chini ya makampuni ya S. S Bakhressa, mbaya zaidi bila kufuata haki za matangazo kwa klabu pinzani.
MFANO HAI
Jumatano ya Februari 20, 2013 kwenye Uwanja wa Chamazi, JKT Ruvu ilikuwa mwenyeji dhidi ya Azam na matokeo yakawa Azam mshindi kwa mabao 4-0. Mchezo huu ulionyeshwa live na televisheni ya StarTV.
Inavyotakiwa, kabla ya mchezo huo ni lazima Azam, JKT na Kamati ya Ligi inayosimamia Ligi Kuu ya Bara zikubaliane juu ya uonyeshwaji huo wa moja kwa moja.
Mambo hayo yote yanatakiwa yawemo katika mkataba huru unaowezwa kuona na pande zote muda wowote inapohitajika kufanyika hivyo.
STAR TV INALIPWA NA AZAM
Azam kwa kuzingatia kwamba inahitaji zaidi kutangaza bidhaa zake kupitia timu yake ya soka, imelazimika kuwa inailipa StarTV kiasi cha fedha kisichopungua Sh. 5 milioni ili mechi yake moja iweze kurushwa live na kituo hicho.
“Azam huwa wanatulipa ili tuweze kuonyesha mechi zao moja kwa moja. Kwa kweli mambo yanakwenda vizuri maana kwao inawasaidia kwa kujitangaza zaidi na sisi tunaingiza fedha kupitia matangazo hayo kuwa yamelipiwa na wao siyo sisi kuwalipa wao,” kilisema chanzo chetu kutoka StarTV.
Kwa kauli hii, ina maana StarTV haifanyi mazungumzo na klabu inayocheza Chamazi na Azam bali jukumu hilo linabaki kwa Azam wenyewe na klabu husika. Hapa kuna tatizo kwani, Azam haina haki ya 100% ya kurusha live mechi zake zinazochezwa Chamazi hata kama itakuwa mwenyeji.
AZAM YAKIRI KUILIPA STAR TV
Mmoja wa viongozi wa Azam ambaye hakupenda jina lake kutajwa, amesema kila mchezo wao unapokaribia hufanya mawasiliano na StarTV kisha kuwalipa kiasi cha fedha kisichopungua Sh. 5 milioni na mechi zao kuonyeshwa live.
“Sisi tunazungumza na StarsTV kisha tunawalipa gharama za kuonyesha mechi live, ambazo huwa kuanzia Sh. 5 milioni, bada ya hapo mechi inachezwa,” alisema kiongozi huyo na alipiulizwa kuhusu malipo ya klabu pinzani, alijibu:
“Hayo ya kuwalipa klabu pinzani mimi siwezi kukujibu lolote kwani hilo ni suala la watu wa timu moja kwa moja. Nadhani kama kungekuwa na tatizo wangetuzuia,” alisema kiongozi huyo.
JKT RUVU HAIKULIPWA
Baada ya kujiridhisha na maelezo ya Azam na StarsTV, mtandao huu uliwasiliana na mmoja wa viongozi wa JKT Ruvu ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake kwa sababu maalum, ambaye alisema timu yake haikulipwa haki za mechi kuonyeshwa live Februari 20, 2013 kwenye Uwanja wa Chamazi.
“Ndugu yangu, sikudanganyi mimi sikuona malipo yoyote kutokana na mechi ile kuonyeshwa live. Sijuhi labda kwa viongozi wenzangu yawezekna wao wamelipwa lakini kwa utaratibu wetu hapa, tungekuwa tumewasiliana na fedha kuletwa klabuni. Hivyo fedha hiyo ni kama haikulipwa,” alisema kiongozi huyo.
YANGA ILIKATAA MTEGO WA AZAM
Jumamosi Februari 23, 2013, Yanga ilicheza na Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Azam ilitaka mchezo huo uonyeshwe live na kulipa Yanga Sh. 10 milioni, lakini Yanga walikataa.
Katika mchezo huo ulioisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Haruna Niyonzima, mashabiki zaidi ya 36,000 waliingia uwanjani na kuingiza kiasi cha Sh. 250 milioni.
Yanga walikuwa wajanja zaidi kwa kuiona thamani yao na kukataa kiasi kidogo cha Sh. 10 milioni ambacho walitaka kulipwa ili mechi yao irushwe live.
KAMATI YA LIGI HAIJUI
Kwa kawaida, mechi yoyote inayotakiwa kuonyeshwa live, ni lazima makubaliano yake yafikiwe na timu zote mbili na kamati ya ligi. Vyombo vyote hivyo vina mgao wake wa fedha.
Mtandao huu ulipowasiliana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia kuhusu hali hiyo, alisema hayupo ofisini na ndiyo kwanza anarejea jijini Dar es Salaam, hivyo apewe muda wa kuwasiliana na wenzake ili kujua kilichotokea.
Lakini Karia alisema, kimsingi klabu zote mbili zinapaswa kukubaliana juu ya uonyeshwaji wa mechi na pia kamati nayo inapaswa kujua hali hiyo pia kufahamu kaisi cha fedha kitakachoingia kwao.
MGONGANANO WA MASLAHI BINAFSI
Mtandao huu, haukuweza kuzungumza na Mwenyekiti wa Azam ambaye ni pia ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Said Mohamed kwani jambo hili lipo katika mgongano wa maslahi.
Mgongano huo wa maslahi kwa Said Mohamed unakuja kwamba, yeye ndiye anayepaswa kukubaliana kimaslahi kama mtendaji wa Azam na wakati huohuo akiwa kama kiongozi wa kamati ya ligi.
Hata kama kamati ya ligi ina wajumbe wengine, lakini Said Mohamed anachukua nafasi kubwa kama makamu mwenyekiti na pia kiongozi wa Azam, hivyo uaminifu unaweza kuwa mdogo kwa suala hili.
VIONGOZI HAWAJUHI HAKI ZA KLABU ZAO
Mara kadhaa unaweza kwenda uwanjani na kukuta mambo yanatendeka kinyume na matakwa au kanuni zinavyotaka. Mfano halisi ni hili la matangazo ya live.
Klabu inaweza kufika uwanjani na kukuta mechi inaonyeshwa live na wasiwe na wasiwasi wowote bila kujua kama wanapoteza haki yao ya kimsingi siku hiyo. Nayo ni kulipwa kwa kitendo cha wao kuonekana moja kwa moja.
Kote duniani na hata hapa bara, mechi yoyote ya live ni lazima timu zote mbili zilipwe haki zao tena kwa makubaliano maalum. Hapo kila timu itaangalia thamani yake na kukubaliana na fedha wanayotaka kulipwa.
Kwa Ligi Kuu ya Kenya, timu zote hupata kiasi kisichopungua Sh. 150 milioni (kwa thamani ya fedha ya Tanzania) kutokana na kituo cha Supersport kuonyesha mechi zao live. Hicho ni kiasi kikubwa katika kuiendesha klabu na kuweza kushindana kikamilifu.
Kumbuka hata wakati ule GTV ilipokuja nchini na kuingia mkataba wa kuonyesha live beedhi ya mechi za ligi kuu, kila klabu iliambulia kiasi cha fedha kwa kitendo chao cha kuonekana live.
KWA NINI MECHI ZA CHAMAZI TU?
Azam inacheza mechi zake za ligi kuu katika viwanja vingi chini, lakini mpango huu wa kuonyesha mechi zake live unatumika zaidi katika uwanja wa Chamazi, labda kwa sababu zifuatazo;
Kwamba, ni mbali ambako hata watu mbalimbali wadadisi wa mambo hawawezi kubaini tatizo na hata kuwashtua viongozi wa timu nyingine juu ya haki yao ya msingi ya kulipwa fedha hizo. Ukweli ni kwamba, watu wengi huwa hawaendi katika mechi za uwanja huo zinazochezwa katikati ya wiki.
Kitendo cha Azam kuwa mwenyeji wa uwanjani, kinawafanya timu pinzani kutokuwa na ujasiri wa kuuliza mambo mbalimbali ya yanayoendelea uwanjani hapo kwani unaweza kuziona kamera zaidi ya mbili uwanjani na ukadhani labda ni moja kati ya mipango ya Azam ya kurekodi mechi zake.
Ikumbukwe ya kuwa, ufahamu ya kujua kwamba mechi hii inaonyeshwa live au tofauti haupo kwa kila kiongozi wa timu za ligi kuu.
MSIMAMO WA MTANDAO HUU
Tunaipongeza Azam kwa kutaka kuonyesha live mechi zake zote inazocheza kwenye Uwanja wa Chamazi, lakini ni muhimu kwao kufuata kanuni kwa kuzilipa timu inazocheza nazo ili kufuta manung’uniko.
Viongozi wa klabu zote za ligi kuu kuacha kuona kila kitu ni kawaida kutokea kwani kuna wakati wanapoteza haki zao za msingi na kujikuta wakiendelea kulia na ukata wakati mianya ya fedha wanaiacha bila kujielewa.
Tunaiomba kamati ya ligi kufanya kazi kikamilifu kwa kuzingatia haki na kanuni za mambo yote yahusuyo ligi hiyo. Pia ifanye kazi kwa kwenda viwanjani na kusimamia mambo yote ya msingi kama haya ya mechi kuonyeshwa live.
Tuna imani hiki tulichokiandika kitafanyiwa kazi na kila upande uweze kupata haki zake stahiki.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
ndo maana, inaposemwa azam imekuja kuleta mapinduzi ya soka nchini nashangaa na kukataa ni walewale hawaizidi yanga wala simba ktk mipango ya mapinduzi ya soka, automatically ukicheza na yanga au simba utapata fedha na kujipangia maendeleo kwa muda ukicheza na azam ni dhiki na dhulma kwenda mbele na mafisadi startv
ReplyDeleteDauda,huu uchonganishi kaka,soka la bongo bado liko chini na hakuna mtu anakubali kudhamini lionyeshwe,hivo azam wako tayari wao waingie gharama kuonesha mechi zao
ReplyDeletekweli kabisa tatizo bongo roho mbaya ndioinatusumbua
DeleteTatizo lako ni kuona yale ya Ulaya yanafanyika Tanzania, kitu ambacho hakiwezekani kufanyika kwa siku moja hata ulaya walianza huku ndio wakafika hapa walipo hii ni kutokana na kanuni za maisha ILI UPATE PESA NI LAZIMA UPOTEZE PESA.
DeleteKwa kipindi hiki ambacho hakuna wa kudhamini mwache anayeweza aanzishe ili kuleta hamasa na msisimko baada mambo yote yatakukuwa sawa.
KUMBUKA hata ulaya HAKUNA HAKI (FAIRNESS) kwenye mgao wa mapato ya TV AD kwani Klabu kama Real au Barca wanalipwa vizuri kuliko Getafe kutokana na Umaarufu wa klabu ambao umejengwa kwa Gharama kubwa na kwa muda mrefu.
well done shaffih
ReplyDeleteHabari hii ni uzushi Mkubwa na uongo, Star TV iliilipa JKT Ruvu Sh. 1,000,000 toka kwenye Malipo yake na pia inaandaa Malipo ya Polisi pindi itakapolipwa na wadhamini. Kupingwa klabu Kama JKT kulipwa 1,000,000 kwa Mechi ambayo mgao wa gate collection haufiki hapa 100,000 ni uzandiki. Waandishi tuwe tunafanya reference kabla ya kukurupuka kuandika makala za uchochezi
ReplyDeleteNimeona patrick kahemele kasema hii habari ni ya uwongo kupitia ukurasa wake wa facebook www.facebook.com/patrickkahemele
ReplyDeleteSIKU ZOTE UKIMWAMSHA ALLIYE LALA UTALALA WEWE. ARAFAT BADO UPO KATIKA USEMI HUO.
ReplyDeleteKILA MWENYE HAKI APEWA HAKI YAKE, SHAFII HAMCHONGANISHI MTU ILA ANATIMIZA WAJIBU WAKE.
HAYA MAMBO YA KIUJANJAUJANJA MPAKA LINI? ANAEKUELIMISHA HAKI YAKO HUYO MTU WA MAANA SANA KWAKO KULIKO ANAYE TAKA UWE MJINGA KILA, NAKUOMBA ARAFAT ONDOKA KATIKA DHULMA HIYO. HATA WANA FALSAFA WALISEMA "YOU CAN FOOL SOME PEOPLE SOME TIME, BUT YOU CAN'T FOOL THE PEOPLE ALL THE TIME" SHAFII PENYE UKWELI SEMA NA HAYO NDIO MAADILI YA KAZI YAKO.
Shafii
ReplyDeleteHakuna maendeleo yanayokuja bila let go
Umekuwa Predisposed kweli
Na huo uwanja wa Chamazi ni wa Timu gani?
Duh mshikaji hapa umetokota, umetumwa nini uje kuvuruga maendeleo ya azam, tafuta vya kuandika vyenye maana na msingi ili kuleta maelndeleo sio blabla kama hizi.....
ReplyDeleteJamaa wamekujbu kupitia FB yao....
ReplyDelete''Azam FC
UONGOZI WA SSB na Azam FC
umesikitishwa na makala
iliyotolewa na Blogu ya
Shaffihdauda eti, klabu zimekuwa
zikidhulumiwa na SSB na Azam
FC kwa mechi zao kurushwa Live
na Star TV.
Tungependa ieleweke kuwa Azam
FC ingependa kuona mashabiki
wake nchini na nje ya nchi
wakiiona mechi live na ndiyo
maana tumekuwa tukilipia
matangazo hayo, pia tunadhani
hili ni jambo jema la kuungwa
mkono na wadau.
Pia tungependa ifahamike kuwa
kwenye kipengele cha mkataba
kati ya SSB na Star TV, kuna
kipengele kinachoilazimisha Star
TV kutoa sehemu ya pato lake na
kuvilipa vilabu ambapo kwa mechi
moja klabu hupata shilingi milioni
moja (1,000,000)
Kwa mechi zinazochezwa
chamazi, klabu hupata mgao wa
kiingilio wa chini ya shilingi laki
tatu hivyo nyongeza ya milioni
moja kwa mechi kurushwa live ni
pesa ya kutosha angalau kwa
kuanzia
biashara ya haki ya matangazo ya
TV lazima ianzie mahali flani na
Azam FC inajaribu kuonesha njia
kwa klabu ndogo ndogo ambapo
hii ni fursa kwa Star TV na Klabu
husika kujaribu kuboresha hali hii
badala ya kupiga majungu.
Tunashukuru kuwa kumekuwa na
uungwaji mkono mkubwa sana
toka kwa klabu.
Ubaya wa habari yenyewe ni pale
walipoinukuu klabu ya JKT Ruvu
kuwa ililalamika kwa
shaffihdauda.com, huu ni uongo
na uzandiki mkubwa kwani JKT
Ruvu walishapokea malipo yao
kupitia kwa katibu wake Bw.
David Ngaga ambaye alipokea
pesa na kusaini vocha ya malipo
ya Sh. 1000,000/-. Angalau
wangeitaja Polisi Moro kwa kuwa
malipo yao yalikuwa yakiandaliwa
na kwa makubalano nao
yatafanyika siku ya Jumanne
19/03/2013
Tungependa kutoa rai kwa
waandishi wa habari kufanya
uchunguzi wa taarifa zao kabla ya
kukurupuka na kuibuka na
makala zenye hisia za migogoro,
uchochezi na majungu.''
Tuache uswahili,Mechi ikichezwa Chamazi watu huwa hawaingii haswa kwa kujua simba au yanga mechi zao hazipangiwi huko. sasa ni bora Azam wajitangaze kwa gharama zao ili ijulikane na hata hivyo vilabu vidogo vitajulikana then biashara baadaye,mf mechi ya AZAM South Sudan tulionyeshwa.AZAM endeleeni na mkiweza walipeni STAR TV tuone Liberia,msikate tamaa.
ReplyDeletehivi kaka Shaffih Dauda mimi na kukubali katika kazi unayo ifanya na nakupa pongezi kwa kazi yako unayo ifanya ya kutupasha habari za michezo....lakin kwa hili la Azam kuonyesha match zao LIVE inabidi tulicheck in a positive way kwa sababu baada ya kutoa habari yako pia nimeona Azam wakitoa taarifa juu ya habari hiyo....haikai vizuri kuita dhuluma wakati kwa hali ya kawaida tu mapato yanayopatikana katika match baina ya Azam na hizo timu mnazoziita ndogo baada ya makato yote klabu hazipati mapato zaidi ya laki moja zote huambulia chini yapo...sasa kitendo cha Azam kuwalipa Star TV na pia klabu nyingine kupata Milioni moja hamdhani ni bora kuliko kuambulia elfu hamsini...maongezi baina ya kamati ya ligi na Star TV kuhusu TV RIGHTS yalivunjika kwa sababu ambazo bado hazieleweki...mimi nadhani alichozungumza katibu mkuu wa Simba Sports Club katika sports round up clouds fm kwamba inaweza kutumika ku push maongezi ya kuhusu TV RIGHTS na kufanikisha zoezi hilo NA SIO SAHIHI KUHITA DHULUMA bali ni timu ambayo imeamua kujitokeza na kutuonyesha njia na pa kuanzia....UPANDE WA PILI wakati nasikiliza kipindi chenu cha sports round up nimemsikia wallace kiria(mwenyekiti wa kamati ya ligi) akisema TV RIGHTS za ligi zipo upande wa TFF sasa hapo sijaelewa kwa nini isiwe wao (kamati ya ligi) kwa sababu wao ndio wanao negotiate. Huku mkurugenzi wa masoko wa TFF hakikwepa kujibu juu ya suala hilo...sasa Azam wanania nzuri unafikiri wangefanyaje zaidi kufanya hivyo...tatizo kubwa ni kwamba Club Kongwe zetu zinatuyumbisha sana wao wanajiwaza wao tu huku wakifurahia Club nyingine zitaabike hivyo kuwarahisishia wao kutamba hapa nchini pasipo kuwepo kwa manufaa kwa taifa..(Amini nakuambia kuna viongozi bla bla pamoja na siasa wa hizi timu kongwe wanaichukia Azam FC na kutamani ipotee kabisa katika ramani ya soka) hivyo ndugu zanguni wapenda maendeleo ya soka la ukweli na sio bla bla tuwe makini na kum-support mtu au club yeyote inayotuonyesha njia sahihi...mimi hapo mwanzo nilivyokuwa nikisoma katika magazeti viwango vya timu zetu zinavyo cheza ni tofauti kabisa hali halisi kabisa unavyoona pale uwanjani..kwa sasa match za club huwa napambana nisikose kuangilia ni ile ya Azam na Mtibwa ama JKT Ruvu..na sasa Timu ya taifa (taifa stars) na huko ndiko kuna soka jamani tuachane na hawa babaishaji....lets THINK POSSITIVELY
ReplyDeleteshafii hapo umepotea, huwezi challenge watu ambao wako serious na kazi ivo, ujue wameamua kufanya ivo sababu ya mizengwe ya hiyo kamati ya ligi hivo wameamua kuwaachia mizengwe yao wao wanasepa kivyao
ReplyDeleteSoka letu bado haliuziki,linahitaji kutangazwa kwanza then ndiyo tufikirie pesa.Azam amekuja kutangaza soka letu pamoja na startv lkn startv mkawatilia zengwe mpk wakubaliane na klabu sasa soka halionekani na hamna aliye na interest nalo.Tangaza kwanza biashara ikubalike then uchukue mapato.Vilabu vinataka pesa wakati havina mipangilio mizuri.Mimi nawaunga mkono azam na startv pamoja na Dstv lkn sisi tunaangalia pesa kwanza.Wachezaji wakiona ligi inaonekana kwenye kioo wanaongeza juhudi na matangazo na wafadhili wanaongezeka then baada ya hapo ndiyo tuangalie pesa kutokana na matangazo hayo na siyo sasa ukata uliopo kwenye vilabu unasababaisha tuangalie pesa bila vipaumbele vya kutuletea pesa hapo baadaye.
ReplyDeleteHahaha shafii shafii shafii huyo shafii jamani anajulikana kwa majungu na chuki binafsi kwanza mpira hajui anajifanya anajua kila kitu tatizo watanzania tuna usimba na uyanga tu zimefanya nini mpaka sasa?azam bidha bora timu bora
ReplyDeleteWewe Shafii ni mnafiki, usie jua nini maana ya uandishi wa Habari. Ume nishangaza sana kwa hili ulilo andika, siku tegemea kwa mtu kama wewe kukurupuka na kuandika habari usizo zijua. haya sasa azama wame kujibu kwenye page yao ya Facebook, Soma uelewe na uache kukurupuka. Club ya Azam kuonyesha match ni jambo la kuigwa na maendeleo kwa Soka letu, ni mfano kwa Simba na Yanga ambazo zime shindwa. Tatizo leo waandishi wa habari kama wewe mme kaa kushabikia Simba na Yanga ambazo hazina maana kwa sasa.
ReplyDeleteUME CHEMKA KAKA KWA HILI NA WALA HATU KUUNGI MKONO KABSA.
HONGERENI AZAM.
shaffih, wewe ni mmoja kati ya watu wanaojiita wadau muhimu wa mpira wa Tanzania. Na umekua ukipiga kelele kwamba klabu nzatu zinakosa ubunifu nje ya uwanja. Leo AZAM wanajaribu kufanya kitu chenye manufaa kwa soka la Tanzania na kwa klabu, unakuja juu kwamba kuna dhurma inafanyika kwa timu zingine. Habari hii umeandika kinazi na haijengi. Inaleta taswira na picha mbaya, inaharibu taswira ya soka la Tanzania na klabu ya Azam. Inamvunja moyo Bwana Bakhressa na wengine wenye malengo ya kuwekeza kwenye mpira. Habari yako imeandikwa kinazi na imekosa vitu muhimu ambavyo vingetoa hitimisho lenye maana kwa soka la Tanzania. Haya ni mambo muhimu yaliyokosekana
ReplyDelete1. Mapitio ya Mkataba wa Makubaliano kati ya Azam na Star TV - Hukutafuta mkataba angalau ujue vifungu vya mkataba, uone ni kwa kiasi gani timu zingine zinaweza kufaidika na onyesho hilo la mpira kwenye luninga. Badala yake, ukakimbilia kuandika maneno ya midomoni kwa watu ambao pengine kwa nafasai zao hawakuhusika katika mkataba huo
2. Hukuzungumza na Mwenyekiti wa Azam ili kujua ukweli kwa sababu rahisi ya 'mgongano wa mawazo'. Inakuwaje unaandika habari pasipo kupata ukweli kutoka kwa Azam wenyewe? Kama Bwana Said (mwenyekiti wa Azam) angekua na maslahi wakati wa mazungumzo, ungeandika ili wadau waone, na sio wewe kukimbilia kutoa hitimisho wakati hukufanya kazi yako kwa usahihi. Ni woga wako na nia ya kutafuta umaarufu wa haraka vilivyokufanya uikimbilie kuandika habari hii pasipo kuwatafuta viongozi wa Azam wakujibu hoja kabla hujaiandika.
3. Toka AZAM waanze kuonyesha mechi zao kwenye luninga, ni zaidi ya timu moja imehusika katika matangazo hayo, ilikuwaje ulifanya mahojiano na JKT Ruvu peke yake? Kwa suala ambalo ni nyeti kama hili, ulitakiwa kuzifuata klabu zote zilizoonekana kwenye luninga, ufanye mahojiano na viongozi katika nyadhifa zao za uongozi na sio kirafiki. Je, inakuwaje kama Klabu zingine zaidi ya JKT Ruvu zitaibuka na kukanusha habari yako kuhusu dhurma? (Japo Azam wanasema tayari JKT Ruvu walishalipwa). Huoni kama unaharibu fani ya watu?
Nilichojifunza kutokana na habari hii ni kwamba hujui misingi ya kuandika habari za uchunguzi, pia hujui miiko ya uandishi. Habari haikamiliki mpaka pande zote zinazohusika ziwe zimehusishwa. Endelea kutafsiri habari za ulaya kutoka goal.com, sky news, BBC sport na mitandao mingine na kutoa maelezo kwenye picha...kidogo kazi hiyo unaiweza, lakini si habari za maana.
AZAM, mpaka sasa ni timu ambayo inatuonyesha watanzania ni nini tunatakiwa kufanya ili mpira wetu usogee mbele. Hizo timu kubwa mbili zimekuwepo kwa zaidi ya miaka 60, lakini hazina lolote la kujivunia. Leo anakuja mkombozi, mnaojiita wadau mnaanza kurusha mawe ili utawala wa timu mbovu uendelee.
Hatutaki watu kama ninyi kwenye mpira wetu. Mnaongozwa na hisia zaidi kuliko ukweli. Habari hii haifai kuwepo hapa. Iondoe ili angalau ufiche aibu uliyoitafuta kwa kutaka umaarufu kirahisi