Search This Blog
Thursday, March 21, 2013
KIKWETE AZIPONDA SIMBA, YANGA HUKU AKIIPA SHAVU KUBWA AZAM FC.
KLABU kubwa za soka nchini zikiwemo Simba na Yanga, zimetakiwa kuachana na ukiritimba katika uongozi ili ziweze kupata maendeleo na kuinua soka la Tanzania.
Rai hiyo imetolewa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete wakati akizindua kituo cha michezo cha Azam Complex kilichopo Mbande Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kikwete alisema kwa kujenga kituo hicho, Azam iliyoanzishwa mwaka 2004 imezishinda klabu kongwe zilizoanzishwa muda mrefu na hadi leo hii hazina viwanja vya mechi zake.
Azam Complex ipo chini ya timu ya soka ya Azam ambayo ni moja kati ya makampuni ya S. S Bakhresa, kampuni kubwa inayomiliki kampuni za utoaji huduma za usafiri na uzalishaji wa vyakula na vinywaji.
“Azam ni timu iliyoanzishwa mwaka 2004 tu, lakini leo hii ina mafanikio makubwa na kuwa mfano wa kuigwa kwa klabu nyingine. Siri kubwa ya mafanikio haya ni nia thabiti ya uongozi na watendaji wake.
“Hawa hawana gozigozi katika utawala tofauti na klabu kubwa za hapa nchini na mimi nawaambia Azam sasa ni timu kubwa na inazisumbua sana hizo mnazoziita timu kubwa,” alisema Kikwete.
Alisema uongozi wa Azam una nia ya kuendeleza soka la Tanzania ndiyo maana umeanzisha kituo hicho ambacho kitazalisha wachezaji wazuri watakaolisaidia taifa siku za usoni.
“Leo hii ninyi mna kituo cha kukuza vijana, wenzenu Simba na Yanga hawana kitu kama hiki, wamekalia ukiritimba tu siku zote na ndiyo maana hawafanikiwi,” alisema Kikwete.
Kabla ya kutoa hotuba yake, Kikwete alitembelea maeneo kadhaa ya kituo hicho ikiwemo viwanja vitatu vya soka ambavyo viwili kati yake havijakamilika, bwawa la kuogelea, hosteli za wachezaji na canteen ya kisasa.
APONDA UCHAWI KATIKA SOKA
Kikwete alitumia nafasi hiyo kuponda klabu zinazoendekeza ushirikina katika soka na kusema kwa kufanya hivyo kunarudisha nyuma maendeleo ya soka nchini.
“Mimi nashangaa sana eti hadi leo hii, timu haina mipango ya maana na viongozi wake wamekalia kuamini mambo ya uchawi tena wanatumia fedha nyingi kutekeleza hazima hiyo, hawa huwa hawafiki mbali na ni ujinga kuamini hivyo.
“Katika Karne hii, uchawi hauna nafasi kabisa zaidi ya mipango thabiti ya kuinua soka. Kama wanaamini uchawi unasaidia basi wawakusanye wachawi wote wa Tanzania halafu wawaingize uwanjani wacheze, tuone kama watafanikiwa.
“Kama uchawi ungekuwa na nguvu, basi Afrika tungechukua Kombe la Dunia tangu zamani na lisingeondoka hapa,” alisema Kikwete na kufanya umati kuangua kicheko.
AWATOLEA MACHO VIONGOZI WABABAISHAJI
Kikwete alisema viongozi wengi wa klabu wanaingia madarakani kwa ubabaishaji mkubwa huku wakitumia rushwa kwa wanachama wasio waaminifu na matokeo yake wanashindwa kupata mafanikio.
“Kila siku migogoro ni sehemu ya maisha ya klabu hizo mnazoziita kubwa. Hawapigi hatua, hawana mbinu za uongozi na wengi wao wapo katika uongozi ili wanufaike na siyo wainufaishe timu, hawa hawafai,” alisema Kikwete.
KIKWETE ‘ANAIPENDA’ ARSENAL
Katika hali ya kushangaza, mara kadhaa Kikwete alikuwa akitoa mifano ya soka la Ulaya na aliitaja sana Arsenal badala ya Barcelona hali iliyowafanya watu mbalimbali kuamini Kikwete ana mapenzi na timu hiyo.
“Tazama wenzenu timu za Ulaya kama Barcelona ilivyokuwa na mifano mizuri ya kuthamini soka la vijana, wale walimkuza (Cesc) Fabregas kisha Arsenal ikamchukua na baadaye akarudishwa Barcelona, hii inaonyesha Arsenal (badala ya Barcelona) ina mfumo mzuri wa kukuza vijana.
“Hiki kinachofanywa na Arsenal (akimaanisha Barcelona) aahh…. Nini Barcelona kinafaa kuigwa na timu zote na Azam imeonyesha nia ya kuiga hali hiyo. Barcelona walimsimamia (Lionel) Messi hadi akafikia mafanikio ya leo hii,” alisema Kikwete.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment