Search This Blog

Saturday, February 16, 2013

TENGA AWATAKA WALIOKATWA UCHAGUZI WA TFF KUFUATA TARATIBU ZA KUTAFUTA HAKI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewataka waombaji uongozi ambao hawaridhiki na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kutafuta haki yao kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo (Februari 16 mwaka huu) mchana, Rais Tenga amesema  TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu unaoeleweka kwa wadau wake.

“Wote tunafahamu taratibu ambazo tumejiwekea juu ya wagombea wetu wanachaguliwaje. TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu unaoeleweka. Hii ni kuanzia wilayani. Kama kuna tatizo zipo njia za kufuata.

“Katika mchakato wa uchaguzi wengine wanafanikiwa, wengine wanaachwa. Wameachwa kwa sababu zilizotolewa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi. Ambaye haridhiki anafuata taratibu tulizojiwekea. Atafute haki yake kwa mujibu wa taratibu,” amesema.

Rais Tenga amesisitiza kuwa kikatiba hana uwezo wa kuingilia uamuzi unaofanywa na kamati ambazo ameziunda, kwani utawala bora ni kusimamia kanuni ambapo wanaofanya uamuzi lazima waweke wazi sababu za uamuzi waliofikia.

Amesema ambao hawakubaliani na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF dhidi yao wana njia tatu za kufuata. Njia hizo ni kuiomba Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ipitie uamuzi iliofanya (review), kuandika Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuomba liingilie au kwenda Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS).

“Hata ukiweka ngazi nne, mtu akiathirika ataona ameonewa tu. Kwa Katiba yetu hapa (Kamati ya Rufani ya Uchaguzi) ndiyo mwisho. Hakuna chombo kingine. Ukiwaomba FIFA waingilie, watakuja na tutawaeleza mchakato wote ulivyokwenda. Tunapenda kuwahakikishia hawa (waathirika) kuwa kwa maslahi ya mpira wa miguu tutasaidia katika hilo wapate haki,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa tayari waathirika wawili wa uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wameomba marejeo (review) kwenye kamati hiyo hiyo.

Amesema TFF imelazimika kuzungumzia suala hilo kwa sababu limekuwa likizungumzwa kinazi zaidi wakati taratibu ziko wazi, hivyo kwa maslahi ya mpira wa miguu ni vizuri taratibu zikafuatwa.

“Nawaomba washabiki wa mpira wa miguu, tumejenga chombo hiki (TFF) kwa muda mrefu. Bado tunaomba watu watusaidie, kwa hiyo matusi hayawezi kubadili kitu. Tunachowahakikishia ni kuwa, mtu anapoomba msaada tutampa kutafuta haki yake.

“Hizi ni kamati huru, lazima ziheshimiwe. Ukianza kuziingilia utakuwa umeua mpira wa miguu. Uongozi ni utumishi, tusionekane tunagombana. Huu si ubunge, mbunge anachaguliwa anakwenda kulipwa mshahara. Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF halipwi mshahara. Tusirudi kwenye matusi, tulishaondoka huko,” amesema.

Kuhusu mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika kwa njia ya waraka, Rais Tenga amesema yamefanyika kwa mujibu wa taratibu, na haikuwa siri. Maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ilikuwa ni lazima, kwani mengi yalikuwa ni maagizo kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Amesisitiza kuwa mabadiliko hayo yamefuata taratibu na hakuna udanganyifu katika hilo, kwani ridhaa ya kutumia waraka iliombwa, na Mkutano ni watu ambao ndiyo wamepitisha mabadiliko hayo.

“Mkutano Mkuu ni watu, si kikao. Katika dunia ya leo mikutano inafanyika kwa tele conference, si lazima watu wakutane sehemu moja,” amesema na kuongeza kuwa mabadiliko hayo yalipitishwa kwa kura 70 dhidi ya 33 zilizokataa.

Kuhusu Kanuni kusainiwa kabla ya Katiba, Rais Tenga amesema tarehe ya kuanza kutumika Katiba ni siku ridhaa ilipopatikana, na si siku mhuri wa Msajili ulipopigwa. Mabadiliko ya Katiba yalipita Desemba 15 mwaka jana, Kanuni zilisainiwa Januari 7 mwaka huu.

5 comments:

  1. Ndugu Rais pole sana kwa kazi ngumu unayoifanya ya kuhakikisha TFF inaye mtaka ndio ataingia na kurithi kiti chako.Hiyo ndio kauli ambayio watanzania wengi walikuwa wakiisubiri.Hakika majawabu yako yanaonesha kabisa unaufahamu sahihi wa mchakato mzima wa suala hili la uchaguzi..Nadhan sasa mtakubaliana na mm ambapo juzi kupitia mtandao huu nilisema mtuhumiwa namba moja ni Rais wa TFF,cz yy anafahamu kilakitu kinachoendelea,tafsiri nyepesi ni kwamba yy ndie mwezeshaji wa kuhakikisha anayemtaka anapokea kijiti chake cha uongozi,na mwisho nilimmshauri asijivunjie heshima aliyojijengea kwa watanzania..Kwa kilichotokea,Rais waTFF anaouwezo wa kuzishauri kamati juu ya maamuz yyte yenye utata na yenye maslahi kwa taifa,haingii akilini kuungamkono madudu yaliyotokea kana kwamba hana akili ya kutambua udhaifu..Narudia tena Rais ndiye mtuhumiwa namba moja kwa hili sakata,na kubwa zaidi anajiharibia heshma na uaminifu aliojenga kwa watanzania..Tahadhari,kwenye ukweli uongo hujitenga..Mungu ubariki Tanzania,Mungu ibariki TFF..

    ReplyDelete
  2. ki ukweli tenga hana jipya katika dunia ya leo na hasa watanzania tupo milioni 43 leo mnatuwekea mtu mmoja agombee peke yake bila bila kupigwa huo ni umbulula kabisa tff ni sehemu nyeti sana na pia ndo imekamata mapenzi ya watanzania wote so naaungana na wanbura kabisa ili swala la kimahakama zaidi bora tufungiwe tu na hao fifa lakini huu uchaguzi ni magumashi matupu

    ReplyDelete
  3. Hivi hawa kina tenga wanatudharau sana watanzania na kutuona cc ni wajinga?katiba yao inasema mabadiliko ya katiba yatafanyika AT GENERAL ASSEMBLY.Unaposema assembly ni lazma watu wakutane wala haina tafsri nyingine hata mtoto wa form one anajua maana ya assembly jaman.
    Utawala bora upi tenga ulioweka hyo miaka yote minane?
    Watanzania tuache kudanganywa eti utawala bora.....miaka minane utawala bora?
    Halafu unabadili katiba kwa email?

    ReplyDelete
  4. KAMA KWELI TENGA ANATAKA KUBAKI NA HESHIMA NINAHAKIKA ANUWEZO WA KUIVUNJA KAMATI ALIYOICHAGUA ILI IIUNDWE KAMATI ITAKAYO SIMAMIA HAKI.VINGINEVYO ATAONEKANA AMEPANDA MIGOGORO ILI AENDELEE KUWEPO WAKATI KESI ZIKIENDELEA.

    ReplyDelete
  5. Hizo ni propaganda za Tenga na watu wake,tunamuheshimu sana Bw Tenga wa yale yote aliyoyafanyia taifa ktk uongozi wake wa miaka 8. ila kubadili katiba wakati chaguzi zimefikia karibu haingi akilini kwa mtu mwenye akili timamu cyo maagizo kutoka fifa wala caf huo ni mipango yake kuumbeba mtu fulani itafikia kipindi itawalazimu watanzania washindwe kwenda viwanjani kuishangilia team yetu ya taifa au vilabu vyetu, anatakiwa awe mzalendo ktk hili na aondoke kwa amani na cyo kuwachagulia watanzania mtu AU watu wa kuongoza TFF.

    ReplyDelete