Search This Blog

Monday, February 25, 2013

KOCHA WA YANGA AGOMA KUMLAUMU JERRY TEGETE KWA KUKOSA MABAO DHIDI YA AZAM FC

KOCHA wa Yanga, Ernest Brandts amemkingia kifua mshambuliaji wake Jerryson Tegete baada ya mashabiki wa klabu hiyo kumshutumu kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga wakati wa mchezo dhidi ya Azam FC.
 

Yanga iliifunga Azam bao 1-0 katika pambano la mzunguko wa pili wa Ligi Kuu lililopigwa mwishoni mwa wiki kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
 

Katika mchezo huo, Tegete alijikuta akipigiwa kelele na mashabiki wa klabu yake huku baadhi yao wakitaka atolewe kwa madai alikuwa akipoteza nafasi za wazi za kufunga.
 

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Brandts alisema kuwa, hawezi kumlaumu Tetege kwa kushindwa kupachika bao kwenye mchezo huo kwa vile kilichotokea ni bahati mbaya ambayo inaweza kumkuta mchezaji nyota yeyote.
 

"Siwezi kumlaumu Tegete kwa kushindwa kupachika mabao kwa sababu wakati mwingine ni mambo ya bahati mbaya ambayo yanaweza kumkuta mchezaji nyota yeyote,"alisema Brandts.
 

Alisema,"Tegete huyu huyu ndiye aliyefunga mabao mawili katika mchezo uliopita na amekuwa anaonyesha juhudi kubwa mazoezini, mimi nasema mambo ya bahati mbaya tu kukosa mabao."
 

Katika hatua nyingine, Brandts alisema kuwa ushindi alioupata dhidi ya Azam unamaanisha
kwamba ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu upo
karibu yao.
 

"Ushindi huu dhidi ya Azam una maana kwamba ubingwa upo karibu yetu, tunachotakiwa kufanya sasa ni kuhakikisha tunaifunga Kagera Sugar katika mchezo ujao ili tuwe katika mazingira mazuri zaidi ya kutimiza kile tunachokifikiria,"alisema Brandts.
 

Katika hatua nyingine baadhi ya mashabiki waliofika kwenye uwanja huo, walimtaka mshambuliaji wa timu ya Yanga, Jerryson Tegete kuwa makini uwanjani kama anataka kupata namba ya uhakika katika kikosi hicho kutokana na kukosa mabao ya wazi kwenye mchezo dhidi ya Azam.
 

Walisema Tegete alikosa umakini kwenye mchezo huo jambo lililofanya aikoseshe timu yake mabao ya wazi. “Yaani huyu Tegete ni haki yake kutoitwa Stars, ona sasa anavyotukosesha mabao ya wazi kabisa hayuko makini kabisa huyu,”alisema Yusuph Salum shabiki wa Yanga.

4 comments:

  1. Kukosa mabao ni sehemu ya mchezo. Lakini mkumbuke pasi ya mwisho kwa Niyonzima aliyofunga bao ilitoka kwa TEGETE. Mbona hilo hawasemi. Tuwe na Shukrani wana yanga. Watanzania tumekuwa watu wa kulaumu tu kila siku. TEGETE AMEBADILIKA SANA. ANAJITUMA. BADALA YA KUMLAUMU, TUMPE SAPOTI.

    ReplyDelete
  2. Tegete saivi anajituma,, kukosa magoli ni kasoro lakini haimuondolei mazuri yake anayoifanyia YANGA SC,, anaweza kumiliki mpira vizuri na anotoa pasi za magori.. TEGETE unaweza sana,, but kumbuka wapi ulikuwa umekosea. Wale jamaa zako wa TABATA SEGEREA, akina CHADO, POTI, achana nao,, bangi sio nzuri.

    ReplyDelete
  3. Dogo mizigo mikubwa anairukia ndo maana akili inakuwa haipo kabisa mchezoni............

    ReplyDelete
  4. Tegete anachosa/anaudhi sana kakosa nafasi mbili za wazi kwa kumpasia golikipa.Anahitaji kupewa nafasi zaidi ya tano kufunga goli moja! Kwenye mechi za kimataifa unapata wapi hizo nafasi zote.Tutabaki hapahapa na ushabiki wa simba na yanga.

    ReplyDelete