YANGA inashuka leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kumenyana
na Azam FC katika mchezo wa kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha
wa Azam, Stewart Hall amesema kurejea kwa majeruhi Brain Omony na Kipre
Balou kumempa faraja kubwa na kutamba kushinda mchezo huo na kukalia
kiti cha usukani wa ligi.
"Nafikiri Omony na Balou wana mchango
mkubwa kwenye timu. Uwepo wao unaongeza chachu ya timu kufanya vizuri."
anasema kocha huyo.
Kwa upande wake kocha wa Yanga, Ernest Brandts
amesema Azam ni moja kati ya timu bora kabisa kwenye ligi hivyo
anatarajia kupata upinzani mkali.
"Azam ni timu nzuri. Ina wachezaji wenye vipaji na uwezo wakucheza kwa maelewano makubwa." anasema kocha huyo.
"Nilikuwa
shuhuda wakicheza na JKT Ruvu nakushinda mabao 4-0. Nafikiri ni timu
nzuri. Mchezo utakuwa mgumu. Siwezi kutabiri lolote."
Timu
hizo mbili zina pointi 36 isipokuwa Yanga inaongoza ligi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Azam inashika nafasi ya pili, lakini yenyewe imecheza mechi 17 wakati vinara Yanga ikicheza 16.
Endapo Yanga itapoteza mchezo huo itakuwa imejiweka kwenye nafasi ngumu ya kutwaa taji hilo kwa msimu huu.
Yanga na Azam zimekutana mara tano tangu msimu wa 2011/12 katika mashindano tofauti.
Katika mechi hizo Yanga imeshinda mara mbili kama ilivyo kwa Azam FC.
Yanga iliifunga Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali Kombe la Kagame na mechi ya ligi mzunguko wa kwanza kwa mabao 2-0.
Azam
yenyewe iliifunga Yanga mechi mbili za ligi msimu uliopita kwa mabao
1-0 mchezo wa kwanza na ule wa marudiano ikiilaza 3-1 na kutokea vurugu
kubwa baada ya Haruna Niyonzima kupewa kadi nyekundu na mwamuzi Israel
Nkongo ikiwa ni kadi yake ya pili ya njano kwa kosa la kumchezea rafu
beki Aggrey Morris wa Azam ambaye amesimamishwa pamoja na Said Morad,
Erasto
Nyoni na Deogratius Minishi kwa tuhuma za kuchukua rushwa kwenye mchezo
wa Simba.
Vita nyingine itakuwa kati ya washambuliaji Kipre Tchetche wa Azam na Didier Kavumbagu kama atanzishwa kikosi cha kwanza.
Jamaa
hawa ndio vinara wa kufunga mabao kwenye ligi. Tchetche amefunga mabao
10 huku Kavumbagu akizamisha tisa na kuziweka timu zao katika nafasi
mbili za juu.
Kazi ipo kesho tusubiri
ReplyDelete