Search This Blog

Tuesday, January 1, 2013

TASWA IMEPOTEZA DIRA NA MUELEKEO WAKE


Takribani siku tatu zilizopita nikiwa kama Mwandishi wa Habari za Michezo nchini Tanzania (jina langu kapuni) nilihudhuria Mkutano Mkuu wa chama cha Waandishi wa Habari nchini maarufu kama TASWA uliofanyika huko mkoani Pwani wilaya ya Bagamoyo katika hoteli ya kifahari ya Kiromo View Resort.

Mkutano Mkuu wa TASWA ulikuwa maalum kwa Wanachama wa TASWA kupata fursa ya kupokea na kujadili Ripoti ya Utendaji ya Chama, Mapato na Matumizi, Maendeleo ya chama na masuala mbalimbali yanayohusu Waandishi wa habari za michezo na maendeleo ya michezo kwa ujumla

Nashukuru kwamba mkutano uliisha salama na waandishi wa habari wamerudi kwenye vyombo vyao kuendeleza gurudumu la kuhabarisha hadhira yetu, lakini kuna mambo kadhaa ningependa kuyazungumzia kuhusu chama chetu cha TASWA.


Kwanza naomba niweke wazi kwamba naamini kama ilivyo katika sekta nyingine hapa nchini, TASWA nayo imeingiwa na mdudu wa matumzi mabaya ya madaraka. KWANINI?

1: SUALA LA MICHANGO YA MKUTANO MKUU
Katika maandalizi ya mkutano mkuu wa TASWA wadau mbalimbali walijitokeza kutoa michango yao kuweza kufanikisha ufanyikaji wa mkutano mkuu. Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Zantel ilitoa kiasi cha milioni 6 za Kitanzania, TSN Supermarket wakatoa Milioni 4, Dioniz Malinzi wa BMT akachangia Milioni 4, Msama Promotion wakatoa 1.5m na Subhash Patel akachangia Milioni 10.

Jumla zikawa Milioni 25.5, lakini pia mdhamini wa Coastal Union Bin Slum baada ya kuombwa na mdau mmoja wa Soka kuchangia mkutano huo alitoa jumla ya Shilingi Milioni Moja ambayo taarifa za uhakika nilizonazo ilienda kuchukuliwa na mmoja ya viongozi wa Taswa,lakini mpaka hii leo haijulikani TASWA hiyo pesa waliifanyia kitu gani.

Ingawa mdhamini huyo wa Coastal hakutaka kutajwa kwenye vyombo vya habari lakini ili kuweka sawa rekodi za mapato na matumizi ni vema uongozi wa Taswa ungebainisha mchango huo kwa Wanachama ili kuondoa migongano ya mawazo kama ilivyo sasa ambapo baadhi ya wanachama wanadai kuna michango mingine ambayo ilitolewa na wadau lakini haikuletwa kwenye hesabu rasmi za chama kama tetesi zinavyoonea.


2: CHAMA HAKINA OFISI RASMI

Taasisi yoyote yenye dira na muelekeo sahihi ni muhimu kuwa na ofisi maalum, mahala ambapo zinafanyika shughuli zote za taasisi hiyo. Na moja ya ahadi kubwa za uongozi uliopo sasa wa TASWA ilikuwa ni kuweza kufanikisha upatikanaji wa ofisi katika kipindi cha miezi 6 tu ya uongozi wao, lakini sasa ni takribani mwaka wa pili sasa unaenda hakuna chochote kuhusu ahadi hiyo, na juzi kwenye mkutano badala ya kutuambia namna ya watakavyotekeleza ahadi zao za uchaguzi wamekuja na mpango mwingine wa Saccos. Saccos sio jambo baya lakini shughuli za Saccos hiyo zitakuwa zinafanyika wapi, bar au ndio ofisi za mifukoni.



Chama hakina ofisi, lakini kwa bahati nzuri kuna wadau wapo tayari kukisaidia hiki chama, watu wamechanga mpaka kiasi cha zaidi ya Milioni 25, cha ajabu uongozi unatumia Mamilioni haya katika kukodisha hoteli ya kifahari ambayo inachaji chumba laki moja kwa ajili kuwalaza wajumbe wanaodhuria mkutano mkuu wa chama. Fikiria kama hizo fedha zingetumika katika kutafuta jengo la japo la kupangisha kwa ajili ya ofisi za chama, na kiasi kidogo kilichobakia ingepatikana sehemu ya nzuri ya bei rahisi na mkutano ungefanyika vizuri tu.

Lakini kutokana na chama kuendeshwa bila dira yenye mlengo ulio sahihi haya ndiyo matokeo yake taasisi ya wasomi wenye ueledi wa kutosha inafanya shughuli kihuni kwa ofisi za mifukoni mwa viongozi. Ndio maana mafanikio ya kujivunia ya chama hiki yamebaki katika kuandaa Media Day Bonanza tu, tukitumbua Mamilioni ya udhamini kutoka kwenye makampuni mbalimbali kwa shughuli zisizo na tija.


Katika mkutano mkuu mgeni rasmi Ridhiwani Kikwete alisema kitu cha msingi sana, iweje chama ambacho ni moja ya nguzo kuu za michezo hapa nchini hasa kwa upande wa soka kinakosa uwakilishi ndani ya Shirikisho la Soka nchini TFF - tunahitaji kuwa sehemu ya TFF ili kuweza kutoa mchango wa moja kwa moja katika kukuza soka la nchi hii.

Kuna vitu vingi vya kuzungumzia katika kuhakikisha tunawekana sawa na kupeana changamoto zenye mrengo wa kuleta utendaji bora ndani ya chama chetu cha Waandishi wa Habari za Michezo lakini kwa leo naishia hapa kwani bado naipitia ripoti ya mapato na matumizi ya chama. 
NAWASILISHA.   

3 comments:

  1. Duuuhhhh kwl hii kali mnavyowasema viongozi wa mpira wa miguu wa vilabu na vyama ili hali hata na nyinyi kumbe wababaishaji kwl mpira wa bongo kuendelea kazi.

    ReplyDelete
  2. Mawazo mazuri ila umeyawakilisha sehemu isiyostahili... kwa kuwa ulikuwepo kwenye mkutano. Ulipaswa kuzungumza pale kwenye mkutano na sio hapa.

    ReplyDelete