TIMU ya soka ya Simba jana ilitoka sare ya bao 1-1 na Tusker ya Kenya
katika mechi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyopigwa kwenye Uwanja
wa Amaan, Zanzibar.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kuanzia saa moja usiku, Simba ilikuwa ya
kwanza kupata bao dakika ya 18 kupitia kwa Haruna Moshi 'Boban'
aliyeunganisha wavuni krosi kutoka kwa Ramadhani Chombo 'Redondo'.
Tusker ilisawazisha dakika ya 39 kwa bao lililofungwa na Khalid Aucho na
kuzifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Licha ya kila timu kufanya mabadiliko kipindi cha pili na pia
kushambuliana kwa zamu, hakuna iliyoweza kuongeza bao na hivyo kuzifanya
zigawane pointi moja kila moja.
Kwa matokeo hayo, Tusker inaongoza kundi hilo kwa uwiano mzuri wa mabao
ya kufunga na kufungwa, kufuatia kila moja kuwa na pointi tatu baada ya
kucheza mechi mbili.
Hii ni mara ya pili kwa Simba kukutana na Tusker katika muda wa wiki
moja. Katika mechi ya kirafiki kati ya timu hizo iliyochezwa wiki
iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilichapwa mabao
3-0 na Tusker.
Katika mechi iliyochezwa jioni, Jamhuri ya Pemba iliichapa Bandari mabao 2-1.
No comments:
Post a Comment