Mshambuliaji mzambia, Felix Sunzu, ameizidi ujanja
Simba baada ya kufanikiwa kuishawishi kwamba anaumwa na ikamwachia aende
zake, lakini habari mpya ni kuwa ameibukia TP Mazembe ya DR Congo
ingawa baba yake anajaribu kukataa.
Sunzu ambaye aliondoka nchini hivi karibuni kwa kisingizio kwamba
Simba imwache anaumwa moyo, mdogo wake Stopila Sunzu ambaye alikuwa
akiichezea Mazembe nafasi ya ulinzi wiki hii atatua Arsenal ya England
kwa majaribio.
Mchezaji huyo alifanya mazungumzo ya kina na Simba akiwa sambamba na
baba yake mzazi na Wekundu wa Msimbazi hao wakamruhusu akaondoka.
Lakini gazeti maarufu la michezo la Kickoff, toleo la Zambia
limeripoti kwamba alikuwa na dili mbili moja ya Zanaco na nyingine TP
Mazembe.
Dili ya Zanaco imeshindikana wiki iliyopita kutokana na dau lao kuwa
dogo na kwamba Jumamosi aliondoka kwenda Lubumbashi, DR Congo kwa ajili
ya mazungumzo ya mwisho ya mkataba na uwezekano wa kusaini ni mkubwa.
Baba yake Sunzu alipoulizwa jana Jumatatu kwa njia ya simu alisema
kwa kusitasita: Hatufanya makubaliano na Mazembe kuna uwezekano wa
kurudi Simba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope,
aliiambia Mwanaspoti kwa simu jana Jumatatu kutoka Uingereza akisema: Sisi tulimuangalia tukaona kwamba ni mgonjwa na hawezi kutufanyia kazi
yoyote katika kipindi cha ligi kilichobaki ndio maana tukamuachia aende
zake.
Hizo habari za kusajiliwa Mazembe hatujazipata rasmi lakini kama
akisaini itabidi atulipe mshahara wa miezi sita aliyokuwa amebakiza
kwenye mkataba wetu, kwa kuwa yeye ndiye aliomba kusitisha mkataba.
Katika hatua nyingine, beki Stopila Sunzu atatua Arsenal wiki hii
baada ya kukamilisha taratibu za kupata hati yake ya kusafiria.
Mmoja wa viongozi wa Shirikisho la Soka la Zambia (FAZ) alisema: Ni
kweli Sunzu (Stopila) anakwenda Arsenal, lakini hajaondoka, amekwenda
Lubumbashi kukamilisha mambo yake.
Kama Stopila akikamilisha dili hiyo atakuwa Mzambia wa pili kucheza
Ligi Kuu England baada ya Emmanuel Mayuka anayecheza Southampton.
Source
No comments:
Post a Comment