STOPPILA Sunzu anaaminika kuwa miongoni mwa
mabeki bora barani Afrika kutokana na mchango wake kwa mafanikio ya TP
Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na timu ya Taifa ya Zambia,
Chipolopolo.
Beki huyo wa timu ya Taifa ya Zambia, ambaye ni mdogo wake
mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu, amepata mafanikio makubwa kisoka
katika siku za karibuni.
Unaweza kutumia ule msemo maarufu kuwa huyu jamaa `kila anachogusa basi kinageuka dhahabu' kutokana na mafanikio haya.
Kumbuka ndio shujaa huko kwao Zambia kwani ndio aliifungia nchi yake
penalti ya mwisho iliyowasaidia kutwaa Kombe la Afrika baada ya kuibuka
na ushindi mabao 10-9 kwa penalti dhidi ya Ivory Coast mwanzoni mwa
mwaka huu.
Yalikuwa ni mafanikio makubwa kwa soka la Zambia kwani kumbuka
ilikuwa imeshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mara 15 bila ya
mafanikio.
Baada ya fainali zile, Stoppila alitajwa katika kikosi bora katika
mashindano yale yaliyofanyika katika nchi za Gabon na Equatorial Guinea.
Pia Stoppila amefanya makubwa na klabu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo kwani amekuwa nguzo ya timu hiyo kutwaa mara
mbili mfululizo taji la Ligi ya Mabingwa Afrika katika miaka ya 2009 na
2010.
Pia ilipofika fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia mwaka 2010.
Stoppila pia alishika nafasi ya pili katika kuwania tuzo ya
Mwanasoka Bora wa Afrika anayecheza barani humu wakati wa sherehe
zilizofanyika Accra, Ghana, wiki iliyopita.
Kufuatia mafanikio ndio maana Stoppila anatakiwa Ulaya na anakwenda Uingereza kujiunga na Reading inayoshiriki Ligi Kuu England.
Stoppila alikuwa Tanzania akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya
Zambia 'Chipolopolo' na kucheza dakika 45 za mwishoni akiwa na jezi
namba 13 kwenye mechi ya kirafiki na Taifa Stars kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Stoppila anafanana kwa sura na kaka yake, Felix kwa rangi ni maji ya
kunde, mrefu na ana umbo linalomfaa kucheza soka sehemu yoyote duniani.
Watanzania walipata bahati ya kumshuhudia nyota huyo 'kitasa' ambaye
hataki mchezo anapokuwa katika himaya yake kutokana na uwezo wake wa
kucheza kwa kutumia akili.
Anajua anachokifanya hana majivuno wala majigambo ndani au nje
uwanja licha ya kuwa na mafanikio makubwa kisoka katika siku za
karibuni.
Ujio wake uliifanya Mwanaspoti imtafute ili kufanya mahojiano naye ya kina naye alifunguka kila kitu.
Safari ya Ghana
Stoppila aliwasili Ijumaa iliyopita tofauti na wenzake ambao walitua
nchini Jumatano iliyopita kwa ajili ya mechi na Taifa Stars.
Alichelewa kutokana na kwenda Ghana alikokuwa amehudhuria sherehe za
Tuzo za Mwanasoka Bora wa Afrika ambako alishika nafasi ya pili nyuma
ya nyota wa Al-Ahly ya Misri, Mohamed Aboutrika kwenye kuwani tuzo ya
wale wanaosakata soka barani Afrika.
Hata hivyo, pamoja na kukosa tuzo hiyo bado alipata mafanikio kwani
kikosi cha Zambia ndio kilitajwa kuwa ndio timu bora ya Afrika kwa mwaka
2012.
"Kitendo cha Zambia kupata tuzo hiyo ni mafanikio makubwa kwa upande wangu na zawadi kwa Wazambia na Waafrika wote kwa ujumla.
"Nafikiri mafanikio yote haya yanatokana na kujituma na kushirikiana vizuri na wenzangu," anaongeza Stoppila.
Amepania kung'ara Ulaya
"Nakwenda kuchezea Reading na nategemea kuondoka Zambia kwenda
Uingereza baada ya siku chache na nikifika huko nitakwenda kukamilisha
mkataba," anaeleza Stoppila.
Stoppila, hata hivyo, mara ya kwanza alitajwa kuwa anakwenda
kujiunga na Arsenal ingawa amekwama baada ya klabu hiyo kutaka kumfanyia
majaribio.
"Sitaenda kucheza Arsenal kwa sababu wanataka kuniona nikicheza mechi zaidi. Kocha Arsene Wenger anataka kuona uchezaji wangu.
"Ninategemea mambo yatakwenda vizuri Reading ingawa kwa sasa akili
yangu ni kuisaidia Zambia kuibuka kidedea huko Afrika Kusini,"anasema
Sunzu.
Sunzu anaeleza amefurahia nafasi ya kwenda kucheza England kwani malengo yake mara zote yamekuwa kucheza Ulaya.
"Hii ni nafasi muhimu katika maisha yangu ya soka. Nitajituma ili kila kitu kiende sawa."
Kutetea ubingwa wa Afrika huko Afrika Kusini
Pamoja na kufungwa na Taifa Stars bao 1-0, Jumamosi iliyopita
kwenye Uwanja wa Taifa, Sunzu anasema hilo haliwachanganyi kwa sababu
wana kikosi imara na cha ushindi.
Zambia inajiandaa kutetea taji lake wakati wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Afrika Kusini mwaka 2013.
"Mashindano ya Afrika Kusini yatakuwa magumu lakini tumejiandaa vya
kutosha kuhakikisha tunashinda mechi zote na kutetea ubingwa
wetu,"anasema Stoppila.
"Kwa sasa tuko vizuri na hatuogopi timu yoyote tutakayokutana nayo huko Afrika Kusini.
"Wengi waliocheza mechi ya Stars ni yosso. Wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza wako Afrika Kusini na klabu zao.
"Kocha alitumia mchezo huu kuwajaribu yosso. Mimi mwenyewe nilicheza nikiwa na maumivu.
"Tumetoka Ghana bila kupumzika. Niliingia uwanjani nikiwa na maumivu ya mguu na misuli lakini nikacheza tu."
Historia
Stoppila amechanganya damu kwani baba yake mzee Felix Sunzu ni Mkongomani aliyezaliwa Jimbo la Katanga na mama yake ni Mzambia.
Alikulia Zambia ambako ndiko wazazi wake waliweka makazi katika mji wa Ndola kabla hawajahamia kwenda Chilambo nchini humo.
Stoppila ni wa tatu kuzaliwa kati ya watoto saba na Felix wa Simba ndiyo wa kwanza, Leticia wa pili, Stoppila wa tatu.
Jackson ambaye anaichezea Konkola Blades pamoja na Boniface
wanafuatana wakiwa wa nne na wa tano, Ngossa ni wa sita na Chrementine
wa saba.
Yeye ni baba wa mtoto mmoja aliyempa jina lake la Stoppila hata hivyo, hakutaka kufafanua zaidi maisha yake.
STOPPILA FELIX SUNZU
Amezaliwa: Juni 22, 1989
Mahali: Ndola, Zambia
Urefu: Ft 6 na inchi 3
Nafasi: beki ya kati na kiungo mkabaji
Klabu: Konkola Blades 2005�2008,
Zanaco 2008�2009,
LB Chateauroux 2008�2009,
TP Mazembe 2009�
Taifa: Zambia
SOURCE: MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment